
Rais wa Burundi atoa onyo kuhusu vita vinavyoendelea Mashariki mwa DRC akisema kuwa vita hivyo vinaweza kusababisha vita vya kikanda.
Kikundi cha M23 kinachopatiwa msaada na Rwanda kimechukua udhibiti wa mji wa Goma, ambao ni mji mkuu wa Mashariki mwa DRC, na sasa kinakusudia kusonga kusini.
Huu ni uvamizi mpya katika eneo ambalo tayari limejaa machungu, ambapo takriban watu milioni sita wamepoteza maisha katika miongo mitatu kutokana na migogoro ya kijamii.
Rais Evariste Ndayishimiye alitoa onyo hilo kwenye mitandao ya kijamii leo Jumamosi, akisema, “Kama Mashariki ya Congo haitapata amani, basi hakuna amani katika eneo hili.” Aliongeza, “Ikiwa vita itaendelea hivi, kuna hatari kuwa vita vitasambaa katika kanda hii.” Rais Ndayishimiye pia alisema, Ikiwa Rwanda itaendelea kufanya mashambulizi… najua vita vitafika hata Burundi.
Matamshi haya yalikuja wakati ambapo kikundi cha M23 kilikuwa kikisonga kusini kuelekea mji wa Kavumu, uliopo katika Mkoa wa Kivu Kusini. Mji huu ni muhimu kijeshi kwani una uwanja wa ndege wa kijeshi na ni sehemu ambapo jeshi la Congo limeweka mstari wake wa ulinzi umbali wa kilomita 40 (maili 25) kaskazini mwa mji mkuu wa Kivu Kusini, Bukavu.
Burundi ilikuwa imepeleka vikosi vya jeshi katika eneo la Mashariki mwa DRC kama sehemu ya vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki vinavyosaidia jeshi la Congo. Hata hivyo, vikosi vyote isipokuwa vya Burundi vilikashifiwa na DRC na wananchi wa eneo hilo kwa kushirikiana na majeshi yanayopingana na utawala wa Kinshasa.