Kesi ya waislamu kupinga mamlaka ya BAKWATA kuendelea leo

Leo tarehe 6 Februari 2025 shauri Na. 27603 la mwaka 2024 la Waislamu 12 walioishtaki BAKWATA pamoja na Mamlaka za serikali wakitaka uhuru kwa waislamu kuamua masuala yao kwa mujibu wa sheria, litaendelea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambapo yatasikilizwa mapingamizi yaliyowasilishwa na Mwanasheria mkuu wa serikali.

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini Tanzania, Sheikh Issa Ponda, pamoja na viongozi wengine 11 wa Kiislam, ndio waliofungua kesi hiyo ya kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakipinga mamlaka ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) juu ya maamuzi yanayohusu masuala ya dini.

Kesi hiyo ilifunguliwa tarehe 13 Novemba 2024, ambapo kwa mujibu wa Sheikh Ponda amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na athari kubwa zinazodaiwa kusababishwa na BAKWATA ndani ya Uislamu. Viongozi hao wanadai kuwa baraza hilo limewanyima Waislamu uhuru wa kujiamulia mambo yao, ikiwemo kumiliki rasilimali na kuendesha miradi ya kiuchumi.

Sheikh Ponda amesisitiza kuwa lengo la kesi hiyo ni kuhakikisha Waislamu wanapata fursa ya kujiwekea uongozi wao, kusimamia rasilimali zao, na kuendesha miradi bila kuingiliwa na taasisi nyingine ambazo hazina ridhaa ya jamii ya Kiislamu.