Mkuu wa Fedha wa Uganda akabiliwa na mashtaka ya wizi wa dola Milioni 16

Afisa mkuu wa fedha wa Uganda, Lawrence Semakula, pamoja na wengine wanane, wamefunguliwa mashtaka ya udanganyifu na utakatishaji fedha kufuatia wizi wa karibu dola milioni 16 za Marekani zilizokuwa zimekusudiwa kulipia mikopo ya maendeleo, kulingana na nyaraka za mahakama.

Semakula, ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, alikuwa miongoni mwa maafisa tisa waliokamatwa siku ya Jumanne kufuatia uchunguzi wa “kutolewa kwa fedha kwa njia ya udanganyifu” kiasi cha dola milioni 15.7 kutoka Benki ya Uganda.

Semakula na maafisa saba kati yao walionekana mbele ya Mahakama ya Rushwa ya Kampala, Alhamisi, ambapo walikabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, udanganyifu wa kielektroniki, kusababisha hasara ya kifedha kwa serikali, matumizi mabaya ya ofisi, na rushwa.

Mtuhumiwa wa tisa alishtakiwa pia lakini hakufika mahakamani, ambapo mahakama ilitoa wito wa kumtaka afike.

“Naamuru washitakiwa wote wabaki gerezani hadi Februari 18,” alisema Jaji Mkuu Racheal Nakazze, kabla ya kufunga kikao kwa ombi la upande wa mashtaka.

Upande wa mashtaka ulieleza mahakama kuwa Semakula na wenzake wanane walihamisha fedha zilizokusudiwa kulipia madeni ya Uganda kwa Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwenda kwa akaunti zilizopo Japan na Uingereza.

Hata hivyo, wakitaka kuahirisha kesi, waendesha mashtaka walisema uchunguzi bado unaendelea. Jaji Nakazze alisema Mahakama ya Rushwa haikuwa na mamlaka juu ya mashtaka ya utakatishaji fedha, ambayo yatapitiwa katika Mahakama Kuu.

Wote tisa walikana mashtaka dhidi yao.