Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO), Joseph Paulo Kaheza amekamatwa akiwa mkoani Geita kwa kile kinachodaiwa kuwa ni vuguvugu la kupigania ajira kwa walimu wa Tanzania.
Joseph amekamatwa wakati ambao umoja huo umekubali mwaliko wa kukutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, kwa ajili ya majadiliano kuhusu ajira za walimu nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa viongozi wengine wa umoja huo wameeleza kuwa “Askari hao wameahidi kukamata viongozi wote wa NETO nchini jambo ambalo tunalilaani vikali kwani sisi sio waahini, ni watoto wa kimasikini tunaoiomba serikali haki yetu ya ajira kutokana na ugumu wa maisha uliokithiri huku mtaani”
Taarifa zinaeleza kuwa kabla ya kukamatwa Joseph alikuwa dukani na mke wake na ilipofika majira ya saa 9 mchana, alikuja kukamatwa na watu ambao hawakujitambulisha kama askari bali walimshika na kumvisha pingu Joseph na kisha kuondoka nae.
Hata hivyo ndugu wa Joseph ambae ni Mjomba wake aliyefahamika kama Barnabas Daud, alifatilia kujua anapelekwa wapi, na ndipo alipojua kuwa anapelekwa kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(RCO).
Hata hivyo alipofatilia kuhusu dhamana ya ndugu yake alinyimwa na alipouliza sababu ya kuendelea kushikiliwa ameelezwa ni kwa sababu ya kuwa sehemu ya NETO
Itakumbukwa kuwa Umoja wa NETO jana uliandika barua ya kukubali wito wa Serikali kwa ajili ya meza ya mazungumzo kuhusu masuala kadhaa waliyoyainisha kama changamoto ya ajira za walimu nchini, hata hivyo katika barua hiyo NETO waliiomba Serikali iwahakikishie ulinzi kutokana na vitisho inavyopokea kutoka kwa watu wasiowafahamu.