Prof. Mikol Philemon Sarungi, ambaye alifariki dunia tarehe 5 Machi 2025 akiwa nyumbani kwake, alijijengea jina kubwa katika historia ya Tanzania kama daktari, mtaalamu wa mifupa, na kiongozi wa serikali.
Prof. Sarungi, ambaye alizaliwa tarehe 23 Machi 1936 huko Tarime, mkoani Mara, alijitolea kwa hali na mali katika kuboresha sekta ya afya, elimu, na utawala wa nchi.
Kwa miaka mingi, Prof. Sarungi alitoa huduma muhimu ya matibabu kwa Watanzania na alichangia katika kuanzisha na kuendeleza baadhi ya taasisi za afya muhimu nchini.
Alikuwa ni mtaalamu wa mifupa na upasuaji, na aliendelea kupanua maarifa yake kupitia masomo ya juu katika vyuo vikuu vya kimataifa, akiwa na shahada za Uzamili kutoka vyuo vikuu vya Szeged (Hungary), Vienna (Austria), na Shanghai (China).
Prof. Sarungi alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1971 kama mhadhiri, ambapo aliweza kuanzisha na kuongoza idara ya upasuaji. Aliendelea kufanya kazi kama mkurugenzi mkuu wa Muhimbili Medical Centre na alihusishwa na jitihada nyingi za kuboresha huduma za afya nchini.
Zaidi ya taaluma yake, Prof. Sarungi alihusika sana katika siasa, akihudumu kama waziri katika serikali za awamu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa Waziri wa Afya(1990-1992), Waziri wa Mawasiliano na Usafiri(1992-1993), na Waziri wa Elimu na Utamaduni(1993-1995 na pia Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Tiafa.
Aliendelea kuwa na mchango mkubwa katika mfumo wa elimu nchini, hasa kupitia ushiriki wake katika Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Prof. Mikol Philemon Sarungi atakumbukwa si tu kwa mafanikio yake katika sekta ya afya na siasa, bali pia kwa roho yake ya kujitolea na huduma kwa jamii.
Urithi wake utaendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi cha sasa na kijacho, na atakumbukwa kama mmoja wa wahenga waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Itakumbukwa pia Prof Sarungi ni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi tangu mwaka 1971 na pia ni mjumbe wa Chama cha Madaktari Tanzania na Chama cha Madaktari wa Upasuaji wa Afrika Mashariki.