Viongozi wa Afrika wamemsifu Papa Francis kwa “urithi wake wa huruma” na “kujitoa kwake kwa ujumuishaji,” wakati walipojiunga na dunia kuomboleza kifo chake kilichotokea leo Jumatatu.
Francis, ambaye alijulikana kwa jitihada zake za kufanya mageuzi ndani ya Kanisa Katoliki na aliwahamasisha wengi, alifariki akiwa na umri wa miaka 88.
Papa huyo kutoka Argentina, aliyekuwa na jina halisi Jorge Bergoglio, aliongoza Kanisa Katoliki tangu Machi 2013. Alikuwa Papa wa kwanza kutoka Jesuit, na pia wa kwanza kutoka bara la Amerika.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, alisifu “ushiriki wa kishujaa wa Papa katika bara la Afrika, ambapo aliinua sauti za wasio na sauti, alipigania amani na maridhiano, na kusimama na walioathirika na migogoro na umaskini.”
Rais wa Kenya, William Ruto, alisema kuwa kifo chake ni “pigo kubwa kwa waumini wa Kanisa Katoliki na ulimwengu wa Kikristo.” Aliongeza kwa kusema, “Aliishi maisha ya uongozi wa utumishi kupitia unyenyekevu wake, kujitolea kwake kwa ujumuishaji na haki, pamoja na huruma yake ya dhati kwa maskini na wanyonge.”
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, alituma “rambirambi zake za dhati,” akisema: “Roho yake ipumzike kwa amani ya milele, na urithi wake wa huruma, unyenyekevu, na utumishi kwa binadamu uendelee kuhamasisha vizazi vijavyo.”
Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, alisema kuwa kifo cha Papa ni “pigo kubwa kwa dunia nzima, kwani alikuwa sauti ya amani, upendo na huruma.” Aliongeza kwamba Papa Francis “alifanya kazi kwa bidii kuendeleza uvumilivu na kujenga madaraja ya mazungumzo… na alikuwa mtetezi wa dhati wa haki za Wapalestina, akitaka mwisho wa migogoro.”

Kifo cha Papa Francis kilitokea siku moja tu baada ya kuwafurahisha maelfu ya waumini waliokusanyika mjini Vatican kwa maadhimisho ya Pasaka, alipowasalimu kutoka kwenye roshani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.
“Kaka na dada wapendwa, kwa huzuni kubwa naomboleza kutangaza kifo cha Baba Mtakatifu Francis,” alisema Kardinali Kevin Farrell kupitia taarifa iliyochapishwa na Vatican kwenye kituo chake cha Telegram.
Papa Francis alikuwa amelazwa hospitalini kwa siku 38 akitibiwa nimonia kali, kabla ya kuruhusiwa kutoka hospitalini ya Gemelli mjini Roma tarehe 23 Machi.
Kifo chake kimeanzisha mchakato wa kale wa Kanisa Katoliki, ambapo makardinali hukutana kwa mkutano maalum wa siri (conclave) ili kumchagua Papa mpya.
Francis alichukua nafasi ya Benedict XVI, ambaye alikuwa Papa wa kwanza tangu Enzi za Kati kujiuzulu, na alionekana kuwa tofauti sana na mtangulizi wake huyo ambaye alikuwa mtaalamu wa theolojia kutoka Ujerumani.