Bunge la Ulaya kujadili kesi ya Tundu Lissu Mei 7, 2025.

Bunge la Ulaya linatarajia kukutana tarehe 7 Mei 2025 kwa ajili ya mjadala wa dharura kuhusu kesi inayomkabili Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu. 

Lissu, ambaye amewahi kukamatwa mara kadhaa katika kipindi cha nyuma, kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya uhaini—kosa ambalo linaweza kumhukumu adhabu ya kifo endapo atapatikana na hatia. Kukamatwa kwake kumetokea miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.

CHADEMA imekuwa ikitoa wito wa kufanyika kwa mageuzi katika mfumo wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki nchini Tanzania. Mashtaka dhidi ya Lissu yameibua wasiwasi mkubwa ndani na nje ya nchi, ambapo baadhi ya wachambuzi na watetezi wa haki za binadamu wanaeleza kuwa hatua hiyo ni jaribio la kisiasa la kumzuia mpinzani mkuu kabla ya uchaguzi.

Mjadala huo wa Bunge la Ulaya utafanyika chini ya ajenda ya kujadili masuala ya uhuru wa msingi, haki za binadamu na hali ya demokrasia kwa ujumla chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amekumbwa na tuhuma za kudhoofisha misingi ya kidemokrasia.

Kwa mujibu wa tovuti rasmi ya Bunge la Ulaya, mjadala huo utafanyika kuanzia saa 7:00 mchana hadi saa 4:00 usiku kwa saa za Ulaya. Baada ya majadiliano na kuandikwa kwa azimio maalum lenye kumbukumbu 2025/2690 (RSP), wabunge wa Bunge la Ulaya wanatarajiwa kupiga kura juu ya azimio hilo siku inayofuata, tarehe 8 Mei 2025.