EU yalaani ukandamizaji wa Demokrasia Tanzania, yataka Lissu aachiwe huru

Umoja wa Ulaya umetangaza msimamo wake dhidi ya kile kinachoitwa kuzorota kwa hali ya haki za binadamu, uhuru wa kisiasa, na demokrasia nchini Tanzania, kufuatia kukamatwa kwa mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, Tundu Lissu.

Wabunge wa Bunge la Ulaya wameelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu mazingira ya kisiasa yanayoendelea nchini Tanzania, wakitaja kuwa hatua dhidi ya Lissu ni mfano wa kile kinachotokea kwa viongozi wa upinzani, wanaharakati wa haki za binadamu, wanahabari, na mashirika ya kiraia. Kwa mujibu wa viongozi hao, mtu yeyote anayeonekana kutishia maslahi ya watawala, hukandamizwa, hutiwa mbaroni au kunyimwa fursa ya kushiriki kwenye siasa kwa haki.

Katika mijadala yao, wabunge hao wamekemea waziwazi uwepo wa vitisho vya adhabu ya kifo kwa Lissu, wakisema kuwa mashtaka ya uhaini na kusambaza taarifa za uongo dhidi yake ni ya kisiasa na yenye lengo la kumzuia kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

“Kesi ya Tundu Lissu si ya kipekee. Inawakilisha namna utawala unavyowatendea wapinzani wa kisiasa, mashirika ya kiraia, waandishi wa habari, jamii za asili na watetezi wa haki za binadamu. Yeyote anayehisiwa kuwa tishio kwa watawala hukandamizwa kimya kimya. Umoja wa Ulaya unaweza na unapaswa kufanya zaidi. Tunapaswa kuweka masharti kwa uwekezaji wowote wa baadaye wa EU nchini Tanzania, masharti yanayolenga kuboresha haki za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria. Ubalozi na ujumbe wa EU nchini Tanzania wanapaswa kufuatilia kwa karibu kesi za wale waliokamatwa kinyume cha sheria, na tuongeze ufadhili kwa mashirika ya kiraia na jamii za asili. Leo, Bunge hili linasimama pamoja na Bwana Lissu na wote walionyimwa uhuru wao kwa njia isiyo ya haki nchini Tanzania. Tunawaambia: hamko peke yenu.” – amesema Catarina Vieira, Mbunge wa Bunge la Ulaya

Umoja wa Ulaya pia umekumbusha kuwa misaada yake kwa Tanzania haipaswi kuchukuliwa kuwa ni ya masharti huru. Wabunge hao wamependekeza kuwa misaada yote ya kifedha na uwekezaji kutoka EU iwekwe katika masharti ya kuhakikisha kunakuwepo na maendeleo ya kweli katika maeneo ya utawala wa sheria, uhuru wa kujieleza, haki za binadamu, na uhuru wa mahakama.

Aidha, wameitaka Tume ya Ulaya na balozi wa EU nchini Tanzania kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi ya Tundu Lissu ili kuhakikisha kuwa inasikilizwa kwa haki na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

“Mashirika ya kimataifa kama Amnesty International, Human Rights Watch na International Democracy Union yamelaani kukamatwa kwa Tundu Lissu, pamoja na kutoa wito wa kuachiliwa kwake na kulaani mashambulizi dhidi ya uhuru wa kisiasa na haki za binadamu. Umoja wa Ulaya unachangia mamia ya mamilioni kwa Tanzania kupitia miradi mbalimbali. Ni lazima tueleze wazi kuwa ushirikiano wowote wa Ulaya na uwekezaji wake lazima uambatane na maendeleo katika maeneo ya utawala wa sheria na haki za binadamu.Tume ya Ulaya inapaswa kufuatilia kwa karibu matukio yanayoendelea, hususan kesi ya Tundu Lissu.”–Reinhold Lopatka, Mbunge wa Bunge la Ulaya

Mbali na Lissu, EU pia imeeleza hofu kuhusu hali ya jumla ya mashirika ya kiraia na jamii za asili nchini Tanzania, yakisema kuwa zinakandamizwa na kukosa uhuru wa kufanya kazi zao kwa ufanisi. EU inasisitiza kuwa ikiwa hali haitaimarika, basi uhusiano wa kimaendeleo kati yake na Tanzania unaweza kupitiwa upya.

Kwa ujumla, Umoja wa Ulaya umetoa wito wa wazi kwa Serikali ya Tanzania kuheshimu misingi ya kidemokrasia, kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, na kusitisha ukandamizaji dhidi ya sauti za upinzani.

Wabunge hao wanamuagiza Rais wake kupeleka azimio hilo kwa Serikali na Bunge la Tanzania pamoja na Umoja wa Afrika. Azimio hilo linatarajiwa kupigiwa kura na wabunge hao leo Alhamisi tarehe 8.