Serikali ya Marekani imetangaza upunguzaji mpya wa ufadhili kwa Chuo Kikuu cha Harvard siku ya Jumanne, siku moja tu baada ya Rais wa chuo hicho, Alan Garber, kusema kuwa taasisi hiyo ina “mambo ya msingi yanayoshabihiana” na utawala wa Rais Donald Trump.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Afya na Huduma za Kibinadamu ya Marekani (HHS), mashirika ya serikali yamefuta misaada ya kifedha ya dola milioni 450 kwa Harvard, ikiwa ni nyongeza juu ya dola bilioni 2.2 zilizokatwa wiki iliyopita. Sababu kuu iliyoainishwa ni kile kilichoelezwa kuwa ni “tatizo kubwa la ubaguzi” ndani ya chuo hicho mashuhuri.
Harvard, mojawapo ya vyuo vikuu vinavyoheshimika zaidi duniani, imefungua kesi mahakamani dhidi ya serikali ya Trump, ikipinga kile inachokiita jaribio lisilo halali la kuingilia utendaji na uhuru wa chuo.
Utawala wa Trump umeongeza mashinikizo kwa vyuo vikuu mbalimbali vya Marekani, ukitaja kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi na kupinga mipango ya utofauti (diversity programs) kama sehemu ya juhudi zake. Hata hivyo, hatua hizi zimezua mjadala mkubwa kuhusu uhuru wa kitaaluma na haki za taasisi za elimu ya juu.
Katika barua aliyomwandikia Waziri wa Elimu, Linda McMahon, siku ya Jumatatu, Rais wa Harvard Alan Garber alisisitiza kuwa chuo hicho kimeanzisha mageuzi makubwa kufuatia matukio ya chuki yaliyoshuhudiwa baada ya mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023. “Mwaka huo wa masomo ulikuwa na changamoto kubwa, na umesababisha mageuzi yenye lengo la kutokomeza chuki dhidi ya Wayahudi na aina nyingine za chuki chuoni,” aliandika Garber.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, hati ya kisheria iliyowasilishwa Jumanne inaonyesha kuwa chuo kilishindwa kurejesha hadhi ya msaada wake wa kifedha katika angalau tukio moja. Katika barua ya Mei kuhusu kusitishwa kwa ufadhili kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Afya (NIH), waandishi wa barua hiyo walieleza kuwa “hakukuwa na hatua ya kurekebisha hali iliyowezekana.”
Garber pia alikanusha madai kwamba Harvard inafuata itikadi yoyote ya kisiasa, lakini alikiri kuwa kuna haja ya kuongeza utofauti wa mawazo chuoni, akisisitiza kuwa wanafunzi huchaguliwa kwa msingi wa sifa za kipekee za mtu binafsi, na si kwa misingi ya rangi.
Hata hivyo, Tume Maalum ya Trump ya Kupambana na Chuki dhidi ya Wayahudi ilitoa taarifa kali dhidi ya Harvard, ikikitaja chuo hicho kama “kituo cha unafiki na ubaguzi.” Taarifa hiyo ilisema kuwa uchunguzi wa ndani wa Harvard umebaini kuwa wanafunzi wa Kiyahudi wamekuwa wakikumbwa na matusi, mashambulizi ya kimwili na vitisho vya mara kwa mara.
“Harvard, pamoja na viongozi wake waliogubikwa na makosa haya ya wazi, wanakabiliwa na mlima mrefu wa kupanda kurejesha heshima ya kuwa taasisi halali ya elimu na ubora wa kitaaluma,” ilieleza taarifa hiyo ya serikali.
Kwa sasa, kesi inaendelea mahakamani huku pande zote zikiwa zimejipanga kuendeleza mvutano kuhusu mipaka ya mamlaka ya serikali juu ya vyuo vya elimu ya juu nchini Marekani.