Shirika la Haki za Binadamu la Amnesty International limetoa ripoti nzito ikifichua unyanyasaji wa kutisha unaowakumba wanawake kutoka Kenya wanaofanya kazi za ndani nchini Saudi Arabia.
Ripoti hiyo inasema kuwa wanawake hao hukumbwa na hali ngumu ya kazi, unyanyasaji wa kimwili na kijinsia, ubaguzi wa rangi, pamoja na kutengwa kabisa kutoka kwa sheria za kazi nchini humo, hali ambayo inalingana na kazi ya kulazimishwa na biashara haramu ya binadamu.
Ripoti hiyo yenye kichwa cha habari “Locked in, left out: the hidden lives of Kenyan domestic workers in Saudi Arabia” imebaini kuwa wanawake zaidi ya 70 waliokuwa wafanyakazi wa ndani nchini Saudi Arabia walilazimishwa kufanya kazi kwa zaidi ya saa 16 kwa siku bila mapumziko, kunyimwa siku za likizo, na kufungiwa ndani ya nyumba. Wengi wao walinyimwa vyakula vya kutosha, walitukanwa, walidhulumiwa kingono, na kuishi kwenye mazingira yasiyofaa kama kulala sakafuni au ndani ya stoo.
“Nilihisi kama kifungwa” – Joy, mfanyakazi wa zamani wa ndani*
“Ukiingia ndani, hutoki. Hukubaliwi kutoka hata mara moja. Hii ilinifanya nihisi kama niko gerezani,” alisema Joy, mmoja wa waliowahojiwa.
-Mateso ya Kisaikolojia na Kimwili-
Ripoti inafichua pia kuwa waajiri waliwanyang’anya wafanyakazi hawa pasipoti na simu zao, kuwazuia kuwasiliana na familia zao, hali iliyowapelekea kuishi maisha ya upweke na unyonge wa hali ya juu. Wengine walikumbwa na ubakaji wa mara kwa mara na vitisho vya kufunguliwa mashtaka ya uongo walipojaribu kuripoti vitendo hivyo kwa mamlaka au ubalozi wa Kenya.
“Aliamua kufanya alichotaka” – Judy, aliyebakwa*
“Alinibaka na kunitisha nisimwambie mke wake. Alifanya kama ni kawaida yake ya kila siku… Alinibaka mara tano,” alisema Judy, mama wa watoto wawili.
-Ubaguzi wa Rangi wa Kusikitisha-
Wafanyakazi wote walizungumza kuhusu ubaguzi wa rangi wa moja kwa moja kutoka kwa waajiri wao. Walikuwa wakitukanwa kwa maneno kama “hayawani,” “sharmouta” (kahaba), au kutengwa kutumia vyombo vya jikoni tofauti na familia. Hii yote ni matokeo ya mfumo wa kafala, mfumo wa udhamini wa wafanyakazi, unaowafanya kuwa tegemezi kabisa kwa waajiri wao.
“Watoto walinicheka na kuniita nyani” – Niah, mfanyakazi wa zamani*
“Kwa sababu ya rangi yangu, niliitwa ‘mnyama mweusi’. Watoto wao walikuja hadi usoni wakinicheka na kusema mimi ni nyani,” alisema Niah.
-Mabadiliko ya Sheria Yasiyo na Meno-
Licha ya Saudi Arabia kuanzisha mabadiliko ya sheria yanayolenga kuboresha hali ya kazi, wafanyakazi wa ndani bado hawajumuishwi katika sheria za kazi za taifa hilo. Mabadiliko ya hivi karibuni ya mwaka 2023 kuhusu mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wa ndani yamekosa tija kutokana na ukosefu wa usimamizi na utekelezaji madhubuti.
-Amnesty Yatoa Wito kwa Serikali za Kenya na Saudi Arabia-
Amnesty International inazitaka serikali zote mbili, ya Kenya na Saudi Arabia – kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama na haki za wafanyakazi hawa.Hii ni pamoja na kuanzisha mfumo huru wa ukaguzi wa majumbani, kufuta mfumo wa kafala, kuweka sheria madhubuti za kazi kwa wote, na kuwezesha balozi za Kenya kuwa na makazi ya muda kwa waathiriwa pamoja na msaada wa kisheria na kifedha.
“Serikali za Kenya na Saudi Arabia lazima wasikilize sauti za wanawake hawa, ambao kazi yao ndiyo tegemeo la familia zao na mchango mkubwa kwa uchumi wa mataifa yote mawili,” alisema Irungu Houghton, Mkurugenzi wa Amnesty International Kenya.
Kuna wafanyakazi wa ndani takriban milioni 4 nchini Saudi Arabia – wote wakiwa ni wahamiaji kutoka nje, ambapo Wakenya wanakadiriwa kufikia 150,000. Kwa sababu ya ukosefu wa ajira nchini Kenya, serikali imekuwa ikihamasisha vijana kutafuta ajira katika mataifa ya Ghuba, huku Saudi Arabia ikiongoza kwa kutuma fedha nyingi za kigeni nyumbani (remittances).