Chadema, Msajili bado vuta nikuvute, wapeleka kesi Mahakamani

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza hatua ya kwenda Mahakamani dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kikimtuhumu kwa kuvuka mipaka ya mamlaka yake ya kisheria, kuingilia masuala ya ndani ya chama na kutafsiri Katiba ya chama kwa namna kinachosema ni ya kibaguzi na nje ya utaratibu wa kikatiba.

Taarifa hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Makao Makuu ya chama hicho, Mikocheni, Dar es Salaam, ambapo alisoma kwa kina maazimio ya Kamati Kuu ya chama yaliyopitishwa tarehe 3 Juni 2025.

Kwa mujibu wa CHADEMA, Msajili wa Vyama vya Siasa amekiuka Katiba kwa kudai kuwa uteuzi wa viongozi wa CHADEMA una dosari za kikatiba, akitaka nafasi hizo kujazwa upya huku akipuuzia mamlaka halali ya vikao vya chama vilivyoteua na kuthibitisha viongozi hao kwa mujibu wa Katiba ya chama.

“Msajili hana mamlaka ya kutafsiri Katiba ya chama chetu. Amekuwa akijipa nafasi ya kuwa chombo cha rufaa, jambo ambalo si sahihi kwa mujibu wa Katiba ya nchi wala ya CHADEMA. Hii ni hatari kwa mustakabali wa vyama vingi na utawala wa sheria,” alisema Heche.

CHADEMA imeeleza kuwa hatua ya kumshtaki Msajili ni sehemu ya jitihada za kudhibiti kile chama hicho kinachokiita “kuwapo kwa matumizi mabaya ya ofisi ya Msajili kuendesha siasa za upande mmoja kwa kuwavuruga wapinzani kupitia nyaraka na maagizo ya kisheria yasiyo na msingi wa kikatiba.”

“Tunaenda Mahakamani sio kwa hasira, bali kwa dhamira ya kuweka rekodi sahihi ya kisheria. Msajili si chombo cha kupokea au kusikiliza malalamiko ya wanachama. Tuna utaratibu wa rufaa wa ndani kwa kila ngazi hadi taifa. Alichofanya Msajili ni kuivamia Katiba yetu,” aliongeza.

Katika mkutano huo, CHADEMA pia ilieleza kuwa hatua ya Msajili imekuwa na athari kubwa ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwa ruzuku halali ya chama, jambo waliloliita kuwa ni “adhabu ya kisiasa isiyo na uhalali wa kisheria.”

Kadhalika Kamati Kuu ya chama imetangaza kuwateua kwa muda viongozi wa nafasi zilizoathiriwa na mzozo huo ili kuhakikisha chama kinaendelea kufanya kazi zake za kisiasa na maandalizi ya operesheni za kitaifa.

Miongoni mwa walioteuliwa ni John Mnyika kuwa Kaimu Katibu Mkuu, Amani Golugwa kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, na Wakili Ali Ibrahim kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu Zanzibar. Viongozi wengine walioteuliwa ni pamoja na Wakurugenzi wa Fedha, Sheria, Mambo ya Nje, Mawasiliano na Ubunifu wa kidijitali.

-Lalamiko kuhusu uhuru wa kuabudu-

Katika hatua nyingine, CHADEMA imelaani vikali hatua ya Msajili wa Jumuiya na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) kufuta usajili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, ikisema ni ishara ya matumizi ya mamlaka kukandamiza sauti za kiroho na kiraia.

“Hatua ya kulifuta kanisa hilo si tu ni uvunjaji wa Katiba, bali ni hujuma dhidi ya uhuru wa kuabudu. Tunatoa wito kwa viongozi wa dini kuendelea kusimama imara kusema ukweli. Taifa lisipolinda uhuru huu wa msingi, linaingia kwenye hatari kubwa ya kiutawala,” alisema Heche.

CHADEMA pia imetangaza kwamba ndani ya siku 60, Baraza Kuu la chama litaitishwa ili kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo rufaa za wanachama, uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, tathmini ya operesheni za chama, na kujibu hoja zilizoibuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Kama chama cha siasa kinachotegemea misingi ya haki, hatuwezi kunyamaza huku vyombo vya dola vikihujumu uhuru wa kiraia, wa dini, na kisiasa,” alisisitiza Heche.