Lissu ajiwakilisha mwenyewe Mahakamani baada ya kunyimwa haki ya kuonana na Mawakili wake Gerezani

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameieleza Mahakama ya Kisutu kuwa ameamua kujiwakilisha mwenyewe katika shauri la uhaini yanayomkabili, akidai kunyimwa haki ya kuonana kwa faragha na mawakili wake tangu alipowekwa mahabusu zaidi ya miezi miwili iliyopita.

Akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Franco Kiswanga kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa kesi, Lissu alisema licha ya kuwa na timu ya mawakili zaidi ya 30 aliowateua kwa hiari yake, hajawahi kuruhusiwa kuonana nao kwa faragha, kubadilishana nyaraka au kupata msaada wa kisheria ipasavyo akiwa gerezani.

“Katika siku 68 tangu niliposomewa mashtaka ya uhaini, sijawahi kupewa fursa ya kukutana na mawakili wangu kwa faragha. Wamekuwa wakifika gerezani, lakini wanaambiwa hawaruhusiwi kuzungumza nami. Hatuna nafasi ya kubadilishana nyaraka wala kuandika lolote,” alisema Lissu.

Akitaja ukiukwaji wa haki zake za kisheria, Lissu aliinukuu Kanuni ya 13 ya *Prison Management Regulations, 1987*, akidai kuwa haki yake ya kupata msaada wa kisheria imekiukwa kinyume na sheria za Tanzania na mikataba ya kimataifa inayolinda haki za washtakiwa.

Lissu aliongeza kuwa hatua yake ya kujiwakilisha inalenga kuwaondolea mawakili wake lawama zisizostahili kutokana na vikwazo vilivyowekwa na mamlaka za magereza.

“Wamenipigania sana. Lakini baada ya siku 68, kama bado hawawezi kuonana nami, sitaki wakili hata mmoja alaumiwe kwa jambo ambalo si kosa lake. Kuanzia sasa, nitajitetea mwenyewe. Nina ujuzi wa kisheria, nimekuwa wakili kwa miaka 22 katika mahakama hii,” alisema.

Mbali na malalamiko kuhusu kukosa msaada wa kisheria, Lissu pia alieleza kunyimwa haki ya ibada akiwa gerezani. Alidai kuwa tangu kufikishwa katika Gereza la Ukonga, hajawahi kuruhusiwa kushiriki ibada za Kikristo zinazofanyika kila Jumapili na siku za sikukuu, jambo ambalo linakiuka haki yake ya msingi ya uhuru wa dini.

“Wafungwa wengine wanaruhusiwa kusali kila Jumapili. Mimi pekee ndiye nimezuiwa, bila sababu ya msingi. Hii ni haki yangu kama binadamu, hata nikiwa mahabusu,” alilalamika.

Lissu ambaye ni kiongozi mashuhuri wa upinzani na mwiba kwa Serikali tawala nchini Tanzania,  alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 akikabiliwa na mashtaka ya uhaini na ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.

Kesi hiyo imeendelea kuvuta hisia kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu ndani na nje ya nchi, hasa kuhusu mazingira ya usalama na haki za watuhumiwa wa kisiasa nchini Tanzania.