Wakenya wamiminika mtaani kuadhimisha mwaka mmoja wa Maandamano ya Umwagaji damu

Maelfu ya Wakenya wamejitokeza mitaani leo Jumatano kuadhimisha mwaka mmoja wa umwagaji damu tangu waandamanaji walipovamia Bunge la Kitaifa katikati ya wimbi la maandamano ya kupinga serikali, licha ya hofu ya kukumbana na magenge yanayodaiwa kuungwa mkono na serikali na ukatili wa polisi.

Mwaka jana, takriban watu 60 waliuawa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano yaliyodumu kwa wiki kadhaa, yaliyosababishwa na kupanda kwa ushuru na hali ngumu ya kiuchumi, hasa kwa vijana. Maandamano hayo yalifikia kilele tarehe 25 Juni, wakati maelfu walipovamia jengo la bunge.

Wanaharakati na familia za waathirika waliitisha maandamano ya amani kuadhimisha siku hiyo, ingawa baadhi yao walitaka “kuchukua Ikulu” wakimaanisha makazi rasmi ya Rais William Ruto. Shule nyingi na biashara zilifungwa kwa hofu ya kuzuka kwa ghasia.

Polisi walifunga barabara kuu zinazoingia kwenye eneo la kibiashara la jiji kuu la Nairobi, huku majengo ya serikali yakiwa yamezungushiwa nyaya zenye makali.

Asubuhi ya Jumatano maandamano yalikuwa ya amani kwa kiasi kikubwa, na waandamanaji wengi wao wakiwa vijana wa kiume walikuwa wakipeperusha bendera za Kenya, maua ya waridi, na mabango yenye picha za waliouawa mwaka jana, huku wakipiga kelele: “Ruto lazima aondoke.”

“Tunaandamana kupinga ukatili wa polisi, kupinga ukandamizaji wa serikali, kupinga ushuru wa juu  kila kitu kinachokwenda mrama katika nchi hii,” alisema Anthony, mwenye umri wa miaka 25, ambaye pia alikuwa akiuza bendera.

Hata hivyo, kulikuwa na viashiria vya vurugu jijini Nairobi, ambapo baadhi ya waandamanaji walirusha mawe na polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi. 

Waandishi wa habari walishuhudia waandamanaji watatu wakiwa wamejeruhiwa.

Mwanaume mmoja anayedhaniwa kuwa afisa wa polisi aliyekuwa amevalia kiraia alishambuliwa na umati. Mwaka jana, polisi wasiojulikana walionekana wakifyatua risasi kwa waandamanaji.

“Sisi huwa hatuna vurugu. Ni polisi na magenge ya watu waliolipwa wanayoyaleta. Wakianza kutupiga mabomu ya machozi, ndipo vurugu huzuka,” alisema Alex Mukasa, mwanaharakati mwenye umri wa miaka 28.

Maandamano pia yaliripotiwa Mombasa na kaunti nyingine kadhaa.

 

– ‘Magenge’ –

Hasira imeongezeka kuhusu ukatili wa polisi, hasa baada ya mwalimu mmoja kuuawa akiwa kizuizini mapema mwezi huu.

Kundi la waandamanaji wa amani pia lilishambuliwa wiki iliyopita na genge la vijana waliokuwa wakiendesha pikipiki, maarufu kama “goons”, waliokuwa na mijeledi na marungu, na wanaodaiwa kushirikiana na polisi.

Balozi za mataifa ya Magharibi nchini Kenya, zikiwemo za Uingereza, Ujerumani na Marekani, zilitoa taarifa ya pamoja kulaani “matumizi ya magenge ya kulipwa kuvuruga mikusanyiko ya amani.”

 

– Kukatishwa tamaa –

Wakenya wengi wana hasira na Rais Ruto, ambaye alichaguliwa mwaka 2022 kwa ahadi ya kuleta maendeleo ya haraka ya kiuchumi.

Wengi sasa wamekatishwa tamaa na hali ya kudumu ya uchumi kusuasua, ufisadi, na ushuru wa juu, hata baada ya maandamano ya mwaka jana kumlazimu Ruto kufuta mswada wa fedha usio na umaarufu.

Serikali yake imejitahidi kuepuka kuongeza ushuru moja kwa moja mwaka huu.

Hata hivyo, kutoweka kwa wakosoaji wa serikali mara kwa mara mashirika ya haki za binadamu yameripoti zaidi ya watu 80 kutoweka tangu maandamano ya mwaka jana, wengi wao bado hawajulikani walipo kumemfanya Ruto kushutumiwa kuwa anairudisha Kenya kwenye enzi za udikteta za miaka ya 1980 na 1990.

Ingawa Ruto awali aliahidi kukomesha visa vya utekaji nyara, Jumanne alionekana kutotilia maanani malalamiko hayo, akisema kuwa ataendelea “kuunga mkono polisi.”