Mwanablogu na mwanaharakati, Ndiang’ui Kinyagia, aliyepotea tangu Juni 21, ametangazwa kuwa amepatikana akiwa hai, familia yake imethibitisha.

Kwa mujibu wa wakili wake, Wahome Thuku, Kinyagia alifanikiwa kufanya mawasiliano na jamaa yake Jumanne jioni kutoka mahali pasipojulika, akithibitisha kuwa yuko mzima kiafya baada ya kujificha kwa hofu ya usalama wake kufuatia taarifa kwamba maafisa wa DCI walikuwa wamtafuta.
DCI ilimhusisha Kinyagia na chapisho la uchochezi lililosambaa kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), likihamasisha maandamano ya Gen Z ya Juni 25. Picha hiyo ilibeba nembo ya taifa na ratiba ya shughuli za kisiasa, ikiwemo maandamano kuelekea Ikulu na uapisho wa “baraza la mpito”.
Ndiang’ui alitoweka mnamo Juni 21, 2025, baada ya kile kinachodaiwa kuwa uvamizi wa maafisa wa DCI nyumbani kwake huko Kinoo. Mashuhuda waliripoti kuwa magari yasiyopungua kumi, yanayoaminika kuwa ya DCI, yalifika nyumbani kwake, wakavunja mlango bila hati ya upekuzi, na kuchukua vifaa vya kielektroniki kama simu, kompyuta, na pasipoti.
Familia yake, mashirika ya haki za binadamu kama Amnesty Kenya, na mawakili wa LSK walitaja kutoweka kwake kuwa kinyume cha sheria na ni mfano wa “kutekwa nyara kwa raia” bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Mahakama Kuu nchini Kenya, kupitia Jaji Chacha Mwita ilitoa agizo kali kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa DCI Mohammed Amin kuwasilisha mahakamani Kinyagia, akiwa hai au mfu.
Agizo hilo lilitolewa kufuatia ombi la habeas corpus lililowasilishwa na Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), baada ya Kinyagia kutoweka mnamo Juni 21, 2025, katika tukio linalodaiwa kuwa ni utekaji nyumbani kwake huko Kinoo.
Jaji Mwita alieleza kutoridhishwa na kutofika kwa maafisa hao wawili mahakamani, akisema: “Siitaji maigizo yenu. Mwasilishe Ndiang’ui Kinyagia, akiwa hai au mfu.” Alisisitiza kuwa haiwezekani kwa raia wa Kenya kutoweka bila dalili yoyote, na kwamba DCI lazima itoe maelezo ya kina kuhusu aliko, hasa ikizingatiwa kuwa maafisa wake walikuwa nyumbani kwa Kinyagia kabla ya kutoweka kwake.
Hata hivyo, DCI ilikana kumzuilia na badala yake kumtaka ajisalimishe kusaidia katika uchunguzi.
Mwanaharakati huyo hata hivyo amesema yuko tayari kufika mbele ya DCI na mahakamani ikiwa atahakikishiwa uwepo wa usalama wake.