CCM yavuna bilioni 2.7 kutokana na ada za fomu za ubunge na udiwani

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekusanya jumla ya shilingi bilioni 2.7 kupitia ada za uchukuaji wa fomu za kugombea ubunge na udiwani kwa uchaguzi mkuu ujao.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Makalla amesema hadi kufikia jana, Julai 2, 2025, zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu ndani ya chama lilikuwa limekamilika ambapo jumla ya wanachama 5,475 walichukua fomu za ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kwa upande wa ubunge wa majimbo yote 272 nchini, watia nia 3,585 walitokea Tanzania Bara na 524 kutoka Zanzibar. Kati ya watia nia hao 4,109 waliojitokeza, wanawake ni 263. Aidha, wanachama 503 walichukua fomu za ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kwa viti maalum vya ubunge kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), wanachama 623 walichukua fomu, ambapo 91 kati yao wanatoka kwenye makundi maalum. Zanzibar walijitokeza wanachama 8 kwa viti maalum vya ubunge na 9 kwa Baraza la Wawakilishi.

Jumuiya ya Wazazi nayo ilishirikishwa ambapo wanachama 55 kutoka Tanzania Bara na watatu kutoka Zanzibar walichukua fomu, huku wanne wakichukua fomu za viti maalum vya uwakilishi, na kufanya jumla ya 62.

Kwa upande wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), wanachama 161 walichukua fomu za ubunge wa viti maalum, kati yao 154 kutoka Tanzania Bara na saba kutoka Zanzibar.

Kuhusu nafasi ya udiwani, Makalla amesema CCM bado haijakamilisha majumuisho rasmi lakini inatarajia watia nia wapatao 15,000 kuwania kata 3,960 nchi nzima, wakiwemo madiwani wa kawaida na wa viti maalum.

Kwa mujibu wa taratibu za chama, gharama za kuchukua fomu za ubunge ni shilingi 500,000 na udiwani ni shilingi 50,000. Kwa takwimu zilizopo, CCM imeingiza jumla ya shilingi bilioni 2.7 kutokana na ada hizo za fomu.