Jaji Mkuu wa Kenya atoa wito kwa mageuzi ya Polisi kufuatia vifo vya waandamanaji

Jaji Mkuu wa Kenya, Martha Koome, ameongoza hafla ya kuwaapisha wajumbe wapya wa taasisi kuu za kitaifa, huku akisisitiza haja ya mageuzi ya dhati katika Jeshi la Polisi, kufuatia ongezeko la maandamano ya wananchi na hali ya sintofahamu nchini humo.

Hafla hiyo ya kuapishwa ilifanyika katika Makao Makuu ya Idara ya Mahakama, ambapo Bw. Abdullah Kassim aliapishwa kuwa mjumbe wa Baraza la Mashujaa wa Kitaifa (National Heroes Council),

Bi. Peris Muthoni Kimani, Bw. Benjamin Juma Imai, na Prof. Collete Suda waliapishwa kama makamishna wapya wa Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC).

Katika hotuba yake kwa viongozi hao wapya, Jaji Mkuu Koome alieleza kuwa uteuzi wao unabeba jukumu muhimu katika kuimarisha taaluma, maadili, na uwajibikaji ndani ya idara ya polisi. Aliwasisitizia wajumbe hao kuwa wao ni walinzi wa maono ya Katiba kuhusu jeshi la polisi linaloweka maslahi ya wananchi mbele, lenye utu, na lenye kuwajibika.

Maandamano ya Saba Saba yagharimu maisha ya watu 10

Kauli hiyo ya Jaji Mkuu imejiri kufuatia maandamano ya kitaifa yaliyofanyika Julai 7, 2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saba Saba, ambapo watu kadhaa walipoteza maisha, wengine kujeruhiwa, na wengine kukamatwa.

Katika taarifa iliyotolewa na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR), imethibitishwa kuwa watu 10 walifariki dunia, 29 walijeruhiwa, 2 walitekwa nyara,
na 37 walikamatwa wakati wa maandamano hayo, yaliyofanyika katika kaunti 17 kote nchini.

Wito wa haki, uwiano na uwajibikaji katika utekelezaji wa sheria

Jaji Mkuu Koome aliwahimiza wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kuandamana kwa amani, bila silaha wala vitendo vya uvunjifu wa amani. Wakati huo huo, aliwataka maafisa wa polisi kuzingatia viwango vya kitaaluma, kutumia nguvu kwa uwiano unaofaa, na kuheshimu haki za binadamu wanapokabiliana na waandamanaji.

“Polisi ni lazima watofautishe kati ya waandamanaji wa amani na wahalifu wanaotumia maandamano kuzua ghasia au kufanya uporaji,” alisema Jaji Mkuu, akisisitiza kuwa wahalifu wanapaswa kushughulikiwa kupitia mfumo wa haki, si kwa msako wa jumla unaokiuka haki za wengine.

Mageuzi endelevu ya sekta ya haki 

Uongozi wa Jaji Mkuu Koome umeendelea kuongoza jitihada za mageuzi katika sekta ya haki. Hivi karibuni, amezindua mahakama maalum za kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia katika maeneo ya Kisumu na Siaya, kufuatia ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake (femicide). 

Kwa mujibu wa Koome, uteuzi wa makamishna wapya wa NPSC unapaswa kuchukuliwa kama nafasi ya kuchochea mabadiliko ya kweli katika idara ya usalama, kwa manufaa ya wananchi wote.