Trump kukutana na marais wa mataifa matano ya Afrika Ikulu ya White House

Rais wa Marekani, Donald Trump, anatarajiwa kuwakaribisha marais wa mataifa matano ya Afrika kwa chakula cha mchana katika Ikulu ya White House siku ya Jumatano, ambapo masuala ya biashara na uwekezaji yanatarajiwa kupewa kipaumbele miongoni mwa mada nyinginezo.

Marais wa Senegal, Liberia, Guinea-Bissau, Mauritania na Gabon — mataifa matano yaliyoko kwenye Pwani ya Atlantiki ya Afrika — wamealikwa na Trump kuhudhuria mkutano huo wa ngazi ya juu.

Maafisa kutoka mataifa hayo wamesema kwamba wanatarajia mazungumzo yatahusu biashara, uwekezaji na usalama, miongoni mwa masuala mengine, watakapokutana katika ukumbi wa chakula wa Ikulu ya Marekani.

Hata hivyo, hakuna maelezo mengi yaliyotolewa kuhusu malengo rasmi ya White House katika kikao hicho.

Mkutano huu unafanyika wakati ambapo serikali ya Trump imekuwa ikijikita kwenye masuala ya ushuru wa forodha na mikataba ya kibiashara, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa madini muhimu kwa viwanda.

Lakini mataifa haya matano hayajatajwa kuwa na utajiri mkubwa wa madini kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jambo linaloweza kuathiri mazungumzo ya kibiashara.

Pia, kikao hiki kinajiri siku chache tu baada ya utawala wa Trump kusherehekea kufungwa rasmi kwa shirika la misaada ya nje la Marekani, USAID, kwa madai kuwa hatua hiyo inaashiria mwisho wa “mfumo wa misaada ya hisani”.

Msemaji wa Rais wa Liberia, Joseph Boakai, Bi Kula Fofana, alisema kuwa rais wao alikubali mwaliko huo kwa matarajio ya kuacha kuwa “mpokeaji wa misaada tu.”
“Lengo letu ni kuelekea kwenye biashara na kuwa na washirika wa kiuchumi watakaowekeza,” alieleza.

Naye msemaji wa Rais wa Gabon, Theophane Biyoghe, alisema mkutano huo ni fursa ya kutafuta ushirikiano utakaolenga “kuendeleza viwanda katika uchumi wetu.”

– Ushindani na masuala ya usalama –

China na Urusi, wapinzani wakuu wa Marekani, wamezidi kuimarisha ushawishi wao katika ukanda huo kwa kuwekeza pakubwa, hasa China ikiwa imewekeza katika mataifa kadhaa miongoni mwa haya.

Urusi, kwa upande wake, imeonyesha uungwaji mkono kwa muungano mpya wa Mataifa ya Sahel (AES), unaojumuisha Mali, Burkina Faso na Niger — mataifa yanayoongozwa na tawala za kijeshi na yanayopakana na baadhi ya mataifa yaliyoalikwa White House.

Masuala ya usalama na biashara ya dawa za kulevya pia yanatarajiwa kujadiliwa.

Mnamo Aprili, Guinea-Bissau ilikabidhi kwa mamlaka ya Marekani ya kupambana na dawa za kulevya (DEA) raia wanne wa Amerika Kusini waliopatikana na hatia ya usafirishaji wa dawa za kulevya. Guinea-Bissau imekuwa ikitambulika kama njia ya kusafirishia kokaini kutoka Amerika Kusini kwenda Ulaya.

Kabla ya kuelekea Washington, Rais wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo, aliueleza mkutano huo kuwa ni “muhimu sana” kwa nchi yake.
“Kiuchumi, huu ni mwanzo wa fursa kubwa kwetu,” alisema, akiongeza kuwa anatarajia nchi yake itafaidika pia na “msaada” ambao Marekani inatoa kwa mataifa mengine.

– Ziara za tahadhari –

Viongozi kadhaa wa dunia wamejikuta kwenye mazingira magumu kisiasa wakati wa ziara zao White House.

Wao ni pamoja na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, aliyekumbwa na mzozo mkubwa wa kisiasa na Trump, pamoja na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ambaye wakati wa ziara yake, Trump alimwonyesha video ya madai yasiyo na msingi kuhusu “mauaji ya watu weupe” nchini humo.

Ingawa matukio hayo yalitokea hadharani mbele ya vyombo vya habari katika Ofisi ya Oval, marais wa Afrika wanaokutana na Trump Jumatano hawatarajiwi kuzungumza na waandishi wa habari.

Msemaji wa White House, Karoline Leavitt, hakutoa maelezo mengi kuhusu mkutano huo, zaidi ya kusema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba Trump atakuwa mwenyeji wa “viongozi wa mataifa matano ya Afrika kwa chakula cha mchana” katika ukumbi wa chakula wa Ikulu.

Hata hivyo, Gabon, Liberia, Mauritania na Senegal ni miongoni mwa mataifa 36 ambayo Marekani inazingatia kuyaongeza kwenye orodha ya marufuku ya kusafiri kuingia nchini humo, kwa mujibu wa waraka wa ndani wa utawala huo uliovuja mwezi uliopita.