Jaji agoma kujitoa katika kesi ya mgogoro wa mali za Chadema

Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo Jumatatu, amekataa kujitoa kusikiliza kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akisema kuwa sababu zilizotolewa na upande wa walalamikaji hazikidhi vigezo vya kisheria vinavyoweza kumlazimu kujitoa kwenye shauri hilo.

Kesi hiyo ya madai imefunguliwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Zanzibar, Said Issa, pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini kutoka visiwani humo  Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu. Wanalalamikia usajili wa bodi mpya ya wadhamini wa chama hicho, wakiitaka mahakama iamue juu ya uhalali wa umiliki wa mali za chama.

Jaji Mwanga amekuwa akisimamia kesi hiyo tangu ilipotajwa kwa mara ya kwanza mnamo Aprili 17, 2025. Hata hivyo, Juni 23 mwaka huu, walalamikaji walimuandikia barua ya kumtaka ajitoe katika kesi hiyo, wakidai upendeleo na mgongano wa kimaslahi.

Katika uamuzi wake, Jaji Mwanga amesema hoja zilizowasilishwa hazina mashiko  kisheria na haziwezi kuathiri uamuzi wake katika shauri hilo. 

Ametaja kuwa madai ya kuwa aliwahi kuhudumu katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar hayatoshi kuwa msingi wa kujitoa, kwa kuwa hazina uhusiano wa moja kwa moja na kesi yenyewe.

Ameongeza kuwa hoja zilizotolewa kuhusu uamuzi wa awali alioutoa wa kusimamisha shughuli za chama kwa muda hazina mashiko ya kisheria ya kumlazimisha kujitoa, na hivyo ataendelea kusikiliza kesi hiyo hadi itakapokamilika kwa uamuzi wa mwisho.

Kauli ya Chadema baada ya uamuzi wa Mahakama

Akizungumza nje ya Mahakama baada ya uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa (Bara), John Heche, alieleza kushangazwa na hatua ya upande wa walalamikaji kujaribu kuchelewesha kesi ambayo chama hicho kinataka imalizike haraka.

“Ni ajabu kwamba upande unaodai unataka haki kwa haraka ndio huo huo unaokwamisha mchakato. Lakini kubwa zaidi, ni kutumia kesi ya madai kama kisingizio cha kuzuia shughuli halali za chama” alisema Heche.

Alidai kuwa vyombo vya dola, kwa kutumia kisingizio cha kesi hiyo, vimekuwa vikiendesha vitendo vya ukandamizaji dhidi ya wanachama wa Chadema, akitolea mfano tukio la kuvamiwa kwa mbunge Aida Kenani na askari polisi katika makazi yake siku ya Jumamosi.

“Lakini jana kama mlivyosikia mbunge wetu Aida Kenani, amevamiwa nyumbani kwake na Polisi kwa madai kwamba kuna zuio la chama kufanya shughuli, polisi wamempiga, wamepiga watu, wamechukua baadhi ya mali zake, wameharibu Camera akiwa nyumbani kwake kwa madai kwamba hii kesi ndio inazuia shughuli za chama kufanywa”– alisema 

Aidha, Heche alisema chama chake kimetuma mawakili kufungua kesi dhidi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nkasi (OCD), akimtuhumu kwa kuvamia makazi ya mwanachama kinyume cha sheria, na kusababisha madhara kwa watu na mali zao.

“Kama kuna hoja kwamba tunakiuka maagizo ya Mahakama, basi tuitwe Mahakamani kwa kosa la Contempt of Court, si kupigwa wala kutishwa,”-aliongeza 

Katika hatua nyingine, Heche amesisitiza kuwa Chadema itaendelea na shughuli zake kama kawaida, akisema zuio la awali la Mahakama lilimlenga Katibu Mkuu pekee, na si chama kwa ujumla wake.

Kesi hii ni sehemu ya mfululizo wa mvutano wa ndani unaoendelea ndani ya Chadema, hususan kuhusiana na uhalali wa Bodi ya Wadhamini na matumizi ya mali za chama. 

Wachambuzi wa siasa wanasema mgogoro huu unaweza kuwa na athari kwa maandalizi ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025, iwapo hautapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Mahakama imepanga kuendelea kusikiliza kesi hiyo Agosti 7, 2025.