Polisi: Dogo Janja alifyatua risasi akijihami Arusha

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio la kupigwa risasi kijana Bakari Halifa Daudi (18) katika eneo la Sombetini, jijini Arusha, linalomhusisha Mgombea Udiwani wa Kata ya Ngarenaro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulaziz Abubakari Chande maarufu kama Dogo Janja.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, tukio hilo lilitokea Agosti 23, mwaka huu, majira ya saa 5:30 usiku, ambapo Bakari alijeruhiwa kwa risasi mguuni.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa wakati Abdulaziz, mkazi wa Levolosi, alipokuwa akishuka kutoka kwenye gari lake, alidai kutishiwa kuvamiwa na Bakari pamoja na mwenzake wakiwa na silaha za jadi. 

Katika hali hiyo, mtuhumiwa alitumia silaha aliyokuwa nayo na kumjeruhi Bakari,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya polisi.

Kamanda Masejo aliongeza kuwa, kufuatia tukio hilo, jeshi la polisi limewakamata watu wawili kwa uchunguzi zaidi, huku likiendelea kufuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika.