Uteuzi wa Asha-Rose Migiro: Ishara ya mwelekeo mpya ndani ya CCM kuelekea uchaguzi?

Chama tawala nchini Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Agosti 23,2025 siku ya Jumamosi, kimefanya mabadiliko makubwa katika safu yake ya uongozi kwa kumteua mwanadiplomasia na msomi nguli, Dk. Asha-Rose Migiro, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho akichukua nafasi ya Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye sasa ni mgombea mwenza wa Rais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. 

Hatua hii imeibua mjadala mpana kuhusu maana yake kisiasa, hasa wakati huu taifa likijiandaa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Dk. Migiro, mwanamke mwenye historia ya kipekee ambaye kitaaluma ni mwanasheria, si mgeni katika jukwaa la siasa za ndani na za kimataifa. 

Aliwahi kushikilia nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika serikali ya awamu ya nne, kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, nafasi ya juu kabisa kuwahi kushikiliwa na Mtanzania katika ngazi za kidiplomasia ya kimataifa.

Kwa sasa, uteuzi wake ndani ya CCM unaonekana kurejesha taswira yake kisiasa baada ya kipindi cha ukimya wa muda mrefu. Wachambuzi wanasema, kwa uzoefu alionao, Migiro anaweza kuwa chachu ya kubadilisha namna chama hicho kinavyokabiliana na changamoto mpya za kisiasa na kijamii.

Mabadiliko ya kiuongozi ndani ya CCM

Mabadiliko ya kiuongozi si jambo geni kwa CCM, chama ambacho kimekuwa kikitawala Tanzania tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977. Hata hivyo, mara nyingi mabadiliko haya huashiria maandalizi ya chama kuelekea uchaguzi. Wakati huu, uteuzi wa Migiro unakuja sambamba na mageuzi mengine ya safu za juu za chama, hatua ambayo wachambuzi wanaiona kama sehemu ya mkakati mpana wa kukabiliana na ushindani unaokua wa kisiasa nchini.

Nafasi ya Katibu Mkuu ndani ya CCM ni nyeti mno, ikibeba majukumu makuu ya uendeshaji wa shughuli za chama, uratibu wa kampeni, pamoja na kudumisha mshikamano wa ndani ya chama kinachoendelea kushindana na vyama vya upinzani vilivyoongeza kasi ya kujipanga.

Hata hivyo safari hii uteuzi wake umekuwa wa mabadiliko mengi ya mara kwa mara, kiasi wengi kujiuliza kunani ndani CCM?. Na mabadiliko haya yametokea chini ya utawala wa Rais Samia ambaye chini yake amefanya mabadiliko karibu mara nne kama Mwenyekiti wa CCM.

Ikumbukwe mwaka 2021, mara tu baada ya kushika kijiti cha uongozi kama Rais kufuatia kifo cha Rais Magufuli, Rais Samia alibadili nafasi ya Katibu Mkuu aliyekuwa akiitumikia wakati huo Dk. Bashiru Ally na kumteua Daniel Godfrey Chongolo, aliyeshikilia nafasi hiyo kuanzia Aprili 30, 2021 – Novemba 29, 2023, kisha Emmanuel John Nchimbi ambaye alihudumu kuanzia Januari 2024 hadi Agosti 2025.

Ujumbe kwa wapiga kura na jamii ya kimataifa

Wachambuzi wengine wanasema uteuzi wa Migiro unaashiria dhamira ya CCM kuonesha sura mpya mbele ya jamii ya kitaifa na kimataifa. Kwanza, Migiro ni mwanamke,  ishara yenye uzito katika nchi ambayo mjadala kuhusu usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika siasa umekuwa ukipigiwa debe kwa muda mrefu.

Aidha, kutokana na historia yake Umoja wa Mataifa, uteuzi huu unaweza kuipa CCM faida ya taswira ya kitaifa na kimataifa kuonesha kwamba chama hicho kipo tayari kuendana na mabadiliko ya dunia na kushughulikia changamoto kwa mtazamo wa kidiplomasia na kitaaluma.

Changamoto zinazomsubiri

Hata hivyo, nafasi anayokalia Migiro si rahisi. Kwa ndani ya chama, atakabiliana na changamoto za kuimarisha mshikamano wa wanachama, kukabiliana na migawanyiko midogo midogo, na kuhakikisha chama kinabaki thabiti wakati wa kuelekea uchaguzi.

Pia, anatakiwa kulinda ushawishi wa chama miongoni mwa vijana – kundi ambalo mara nyingi limekuwa likihusishwa na changamoto za ajira na mabadiliko ya kijamii.

Kwa nje ya chama, anatakiwa kukabiliana na shinikizo la vyama vya upinzani ambavyo vimeongeza kasi ya maandalizi yao, vikijaribu kujipatia imani ya wananchi kwa kutumia hoja za uwajibikaji wa serikali na changamoto za kiuchumi.

Upeo wa fursa

Pamoja na changamoto zinazomsubiri, Migiro ana nafasi kubwa ya kutumia uzoefu wake kuimarisha mfumo wa chama. Kwa mfano, uwezo wake wa kidiplomasia unaweza kusaidia CCM kuimarisha ushirikiano wake wa kikanda na wa kimataifa. Aidha, ushawishi wake katika masuala ya kijinsia unaweza kuongeza mvuto wa chama kwa makundi ambayo yamekuwa yakidai nafasi kubwa katika siasa.