Chama cha ACT Wazalendo kimesema hakitafuata maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa yaliyobatilisha uteuzi wa mgombea wake wa urais, Luhaga Mpina.
Katika taarifa yake kwa umma, chama hicho kimeeleza kuwa hatua ya Msajili haina mashiko ya kisheria kwa kuwa mchakato wa uchaguzi tayari umeshaanza, huku Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikiwagawia wagombea fomu za kugombea urais. Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, Msajili hana mamlaka ya kuingilia hatua hiyo, zaidi ya kushughulikia malalamiko kwa njia ya pingamizi.
Chama hicho kimeongeza kuwa Mpina ameshakamilisha taratibu zote za kugombea, ikiwemo kula kiapo mahakamani na kuhakikiwa fomu na INEC, na kwamba fomu hizo zinatarajiwa kuwasilishwa rasmi leo kwa Tume hiyo kwa ajili ya uamuzi.
Aidha, ACT Wazalendo imetangaza kuwa itafungua kesi Mahakama Kuu kupinga hatua ya Msajili na kuomba zuio la utekelezaji wa uamuzi huo hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.
Hatua hii inakuja baada ya mwanachama wa chama hicho, Monalisa Joseph Ndala, ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam na Naibu Waziri Kivuli wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, kuwasilisha malalamiko kwa Msajili tarehe 22 Agosti. Ndala alipinga mchakato wa kumpitisha Mpina akisema umekiuka Katiba ya chama, kanuni zake za kudumu pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa.
Ndala alidai kuwa chama kilishindwa kukanusha uvunjifu wa vifungu vya Katiba, ikiwemo Ibara ya 11(e) inayotamka kuwa kila mwanachama ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa kulingana na masharti ya chama.