Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, amesema pingamizi lake la kisheria halina lengo la kutafuta huruma ya umma, bali kutaka haki ipatikane kwa mujibu wa sheria na viapo vya mahakama.
“Kupata huruma unaponewa si kosa, lakini jambo muhimu zaidi ni kupata haki. Siwaombi Waheshimiwa Majaji mnipe haki kwa sababu ya huruma, bali kwa mujibu wa viapo vyenu na kwa mujibu wa sheria,” alisema Lissu jana mbele ya jopo la majaji watatu katika Mahakama Kuu.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akiwasilisha hoja zake akijibu hoja za upande wa Serikali katika pingamizi kwenye kesi ya uhaini inayomkabili, ambapo anapinga mamlaka ya Mahakama Kuu kusikiliza kesi hiyo.
Uamuzi wa pingamizi hilo unatarajiwa kutolewa Jumatatu, Septemba 15, saa tatu asubuhi.
Lissu, ambaye leo, Septemba 11, ametimiza siku 157 tangu apelekwe gerezani, jana Septemba 10, 2025, aliomba kuahirishwa kwa usikilizwaji wa pingamizi hilo ili kupitia kesi mbalimbali ambazo upande wa Jamhuri umetumia kama rejeo la kupinga hoja zake.
Katika maelezo yake, Lissu alisisitiza kuwa hatua ya awali ya committal proceedings katika Mahakama ya Kisutu haikuzingatia misingi ya haki, ikiwemo kupata nyaraka zote zinazotumika dhidi ya mtuhumiwa.
“Kama kweli lengo la committal proceedings ni kuhakikisha haki ya usikilizwaji wa haki (fair trial), basi mtuhumiwa anatakiwa kupewa fursa kamili ya kujiandaa na utetezi wake. Huwezi kufichwa nyaraka, au kupewa taarifa nusu nusu,” alisema.
Akitolea mfano, Lissu alidai kumbukumbu za mahakama (proceedings) zimejaa makosa ya makusudi na si ya bahati mbaya.
“Kama kuna makosa moja au mawili katika kurasa 111, unaweza kusema ni bahati mbaya. Lakini ukikuta makosa ya aina hiyo yamerudiwa mara kadhaa, lazima ujiulize kama si makusudi,” aliongeza.
Aidha, alipinga hoja za Wakili Mkuu wa Serikali, Nassoro Katuga, na Wakili wa Serikali Job Mrema waliodai kifungu cha 183 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinawapa mamlaka ya kuendelea na kesi hiyo. Kwa mujibu wake, kifungu hicho hakiwezi kutumika kwa sababu alikamatwa kabla ya kufikishwa mahakamani.
Kuhusu mashahidi, Lissu alisema majina ya mashahidi wake hayakuorodheshwa katika committal proceedings, jambo linalonyima haki yake kisheria chini ya kifungu cha 264 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Aliongeza kuwa hatua hiyo imesababisha kupoteza haki ya mashahidi wake kuitwa rasmi, kama inavyotakiwa na vifungu vya 281 na 314(2) vya sheria hiyo.
Kuhusu mamlaka ya Mahakama Kuu kusikiliza kesi ya uhaini, Lissu alisisitiza kuwa Mahakama ya Kisutu haikuwa na mamlaka ya kuhamisha kesi hiyo, hivyo mchakato mzima una dosari za kisheria.
“Hadi sasa sina kesi yoyote Mbinga, wala Kisutu. Kwa hiyo, kama mtaifuta kesi hii, basi nitakuwa sina kesi popote na siwezi kupelekwa Ukonga,” alisema.
Kesi hiyo namba 19605 ya mwaka 2025 ilihamishwa kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, baada ya kukamilika hatua ya kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Lissu, mwanasiasa na mwanasheria maarufu, alikamatwa Aprili 9, 2025 huko Mbinga mkoani Ruvuma muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa hadhara ambapo alikuwa akinadi sera ya chama chake ya “No Reforms, No Election” (Bila Mabadiliko Hakuna Uchaguzi).
Chadema inasisitiza kuwa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi ni lazima, wakidai mifumo iliyopo sasa inawanyima wapinzani haki sawa.