Jamhuri Yapangua Hoja za Lissu, Yeye Asisitiza Hati ni Batili

Upande wa Jamhuri umejibu hoja za mshtakiwa Tundu Lissu kwa kuzipangua moja baada ya nyingine, huku Lissu naye akisisitiza kwa msimamo wake kuwa hati ya mashtaka ya uhaini inayomkabili ni batili na haina uhalali wa kisheria.

Jamhuri yapangua hoja za Lissu, yeye asisitiza hati ni batili

Majibizano hayo yaliyochukua takribani saa tano katika Mahakama Kuu leo, yakihusu hoja za kisheria zilizowasilishwa na pande zote mbili.

Licha ya Jamhuri kueleza kuwa hati ya mashtaka iliyoletwa mbele ya Mahakama imeandaliwa kwa mujibu wa sheria Lissu alipinga akiweka bayana kwamba kasoro zilizomo ni kubwa, za msingi na haziwezi kurekebishwa kwa namna yoyote.

Jamhuri: “Pingamizi la Lissu halina msingi”

Wakili wa Serikali Nassoro Katuga akijibu hoja za upande wa mshtakiwa , akianzia kwa kukubaliana na msingi uliowekwa na Lissu kwamba kifungu cha 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinahitaji hati ya mashtaka iwe na maelezo yanayojitosheleza.

Hata hivyo, Katuga alikanusha hoja kwamba hati iliyofikishwa Mahakamani imekosa sifa hizo.

“Hati hii imeandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 138, ambacho kinaruhusu iandikwe kwa lugha inayoeleweka ili mshtakiwa afahamu mashtaka yake. Pingamizi la upande wa mshtakiwa halina msingi wowote wa kisheria,” alisema.

Katuga alifafanua kwamba kifungu cha 39(2)(d), ambacho kiliwekwa kama msingi wa mashtaka, kimeandikwa kwa namna inayoruhusu mashitaka zaidi ya moja kutengenezwa kupitia mbadala wa neno “or”. Hivyo, kulingana naye, mshtakiwa hakuwa sahihi kudai kuwa mashitaka yamebuniwa au hayakujitosheleza.

Maneno yalilenga kutishia Serikali-

Kwa mujibu wa Jamhuri, hoja ya msingi siyo kwamba mshtakiwa alizungumzia uchaguzi, bali kwamba alitengeneza nia ya kutishia Serikali.

“Mshtakiwa alionyesha bayana nia ya kutishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hilo ndilo linaunda kosa la uhaini. Hoja kwamba alikuwa akizungumzia uchaguzi pekee ni kupotosha,” alisema Katuga.

Aidha, alikosoa rejea ya mshtakiwa kwenye kesi ya Khatibu Ghandi akisema, tafsiri alizozitoa hazikuwa sahihi na zilifanyika “kwa kutokujua”. Kwa mtazamo wa Jamhuri, tafsiri ya maneno ambayo yanaweza kuunda kosa la uhaini si suala la awali la kisheria bali ni jambo la ushahidi litakalothibitishwa wakati wa usikilizwaji.

Lissu: “Hati ni batili, maneno hayatengenezi kosa”

Kwa upande wake, Tundu Lissu alijibu hoja za Jamhuri kwa msimamo thabiti, akisema mashitaka yaliyopo mbele ya Mahakama siyo tu ya jinai, bali ni ya kiwango cha juu zaidi kwani ni uhaini, kosa linalobeba adhabu ya kifo.

“Hati ya mashtaka katika kesi za aina hii lazima izingatie kwa ukamilifu masharti ya kifungu cha 135. Mahakama ya Rufani imetamka wazi katika kesi za Isidori Patrice na Spelius Mlokozi kwamba usipofata masharti ya kifungu hicho, hati ya mashtaka inabatilika. Hii iliyopo mbele yenu ni batili,” alisema.

Lissu alipinga hoja za Jamhuri zinazotegemea kifungu cha 138, akisema hakihusiani na suala la msingi la kujitosheleza kwa hati. Alisisitiza kuwa kuzuia uchaguzi si kosa la uhaini chini ya sheria za Tanzania na kwamba “maneno matupu hayawezi kutengeneza kosa la uhaini”.

Akirejea tena kwenye kesi ya Khatibu Ghandi, Lissu alinukuu maamuzi ya Mahakama ya Rufani yaliyosema bayana kwamba “maneno hayatengenezi kosa la uhaini isipokuwa tu pale yanapoelezea kitendo halisi”.
“Hakuna publication, hakuna ushahidi”

Moja ya hoja kubwa za Lissu ilikuwa kuhusu kipengele cha “publication”. Alisema kuwa hakuna ushahidi wowote kwamba maneno aliyoyazungumza yamechapishwa kwenye mitandao ya kijamii au karatasi yoyote.

“Kama kweli kulikuwa na publication, lingetajwa wazi kwenye hati ya mashtaka. Madai kwamba nilichapisha mitandaoni hayana uthibitisho wowote. Hii ni hati batili kutoka mwanzo,” alisema Lissu.

Aliongeza kuwa tafsiri ya Jamhuri kwamba “maneno ni matendo” haikubaliki, akisema tafsiri hiyo inapingana na msimamo wa Mahakama ya Rufani.

Mabishano kuhusu mashahidi na marekebisho

Lissu alikanusha hoja ya kwamba hati ya mashtaka inaweza kusimama peke yake bila maelezo ya mashahidi. “Kwa mujibu wa kifungu cha 262(6), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) anatakiwa kuwasilisha taarifa ya kosa pamoja na maelezo ya mashahidi. Bila hivyo hakuna kesi. Huu ndio msimamo wa sheria,” alisema.

Aidha, Lissu aligusia suala la marekebisho ya hati ya mashtaka, akieleza kwamba kifungu cha 295(1) kinarejea kifungu cha 294(2), ambacho kinataka ruhusa ya Mahakama ili kufanya marekebisho yoyote. “Si jambo la kienyeji. Sheria imeweka utaratibu maalumu,” alisema.

Baada ya majibizano hayo ya pande zote mbili Jaji Dastan Nduguru ambaye anaongoza jopo la majaji watatu ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 22, 2025 saa tatu asubuhi kwa ajili ya kuja kutolea maamuzi ya pingamizi hilo.