Umoja wa Afrika (AU) umempongeza Peter Mutharika kwa ushindi wake katika uchaguzi nchini Malawi, na kuwashukuru wananchi wa Malawi kwa kampeni za amani.
Mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye aliwahi kushika madaraka kuanzia mwaka 2014 hadi 2020, amechaguliwa tena kwa kura karibu asilimia 57 ili kuongoza taifa hilo lenye watu milioni 21 wengi wao wakiwa maskini.
Ushindi huo mkubwa ulipatikana dhidi ya Rais aliyekuwa madarakani, Lazarus Chakwera, ambaye alipata kura asilimia 33, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya Malawi iliyotangaza matokeo jana Jumatano.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, alimpongeza Mutharika mwenye umri wa miaka 85. Kupitia taarifa aliyochapisha katika mtandao wa X, alisema anampongeza pia wananchi wa Malawi kwa ushiriki wao wa amani, wenye hamasa na uliofuata sheria katika mchakato huu wa kidemokrasia wa kuaminika.
Mutharika, anayejulikana kwa wafuasi wake kama “baba”, anatakiwa kuapishwa kuwa rais ndani ya siku kati ya saba na thelathini baada ya kutangazwa kwa ushindi wake.
Ameahidi kukuza uchumi na kumaliza tatizo la upungufu wa fedha za kigeni lililozuia uagizaji wa mafuta na mbolea.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wa Malawi wanaishi katika umaskini.