Waandamanaji wa Madagascar waendelea licha ya kufutwa kwa serikali

Waandamanaji nchini Madagascar wameitisha maandamano mapya leo Jumanne, siku moja baada ya Rais wa nchi hiyo Andry Rajoelina kuvunja serikali yake kwa lengo la kutuliza ghasia zilizosababisha vifo vya watu 22, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Harakati hizi zinazoongozwa na vijana, na ambazo zimepata msukumo kutoka kwa maandamano ya kizazi cha “Gen Z” nchini Indonesia na Nepal, zimeelekeza lawama kwa utawala mbovu wa muda mrefu, zikichochewa na hasira kutokana na ukosefu wa maji na umeme unaojirudia katika taifa hilo la Bahari ya Hindi.

Jana Jumatatu, Rajoelina alivunja baraza lake lote la mawaziri na kuahidi kutafuta suluhisho kwa matatizo ya nchi.

“Wakati watu wa Madagascar wanapoteseka, nataka mjue kwamba mimi pia nahisi maumivu hayo, na sijalala usiku wala mchana nikitafuta suluhisho na kuboresha hali,” alisema.

Hata hivyo, hatua hiyo haikutosha kuzima maandamano, na waandaaji walitangaza mkutano mkubwa leo Jumanne saa tano asubuhi (0800 GMT) katika mji mkuu wa Madagascar

Maandamano ya awali yamekumbana na ukandamizaji mkali wa polisi, ambapo angalau watu 22 wameuawa na zaidi ya 100 kujeruhiwa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. Serikali imepinga takwimu hizo ikizitaja kuwa “hazijathibitishwa” na “zimeegemea upande mmoja”.

Wiki iliyopita maandamano katika mji mkuu Antananarivo yalifuatwa na uporaji ulioenea usiku kucha.

“Wanatuita kizazi cha TikTok, kizazi cha wajinga, na tukijaribu kuinuka, hawatupi nafasi ya kuzungumza,” alisema mwanafunzi mmoja aliyeshiriki maandamano Jumatatu, akiwa amevaa nguo nyeusi kulingana na mwito wa mitandaoni wa kuomboleza waliouawa.

“Bwana Andry Rajoelina, wakati wewe uliandamana, ulipewa nafasi, na ilikuwa sawa. Lakini sisi vijana tunapoinuka kupigania nchi yetu, mnataka kutunyamazisha,” aliongeza.

Rajoelina, ambaye aliwahi kuwa Meya wa Antananarivo, alipanda madarakani kupitia mapinduzi yaliyomng’oa rais wa zamani Marc Ravalomanana.

Baada ya kushinikizwa na jumuiya ya kimataifa kutogombea uchaguzi wa mwaka 2013, alirudi tena na kuchaguliwa mwaka 2018.

Madagascar ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani, lakini ndiyo muuzaji mkuu wa vanilla, kiungo ghali zaidi baada ya bizari (saffron).