Shahidi wa kwanza katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu, ameanza kutoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, akieleza kwa kina namna alivyopokea taarifa kuhusu video iliyokuwa ikisambaa mtandaoni na baadaye kuanzisha uchunguzi uliosababisha kufunguliwa kwa kesi hiyo.
Shahidi huyo ambaye ni Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) George Wilbart Bagemu, mwenye umri wa miaka 48, ambaye ni afisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka ishirini katika taaluma ya upelelezi.
Katika ushahidi wake mbele ya Mahakama, ACP Bagemu aliieleza kuwa kwa sasa anahudumu kama afisa wa polisi wa ngazi ya Kamishna Msaidizi, cheo alichopata mwezi Juni 2025, baada ya kupanda kutoka ngazi ya Mrakibu wa Polisi.
Akijibu maswali ya Wakili wa Serikali Nassoro Katuga, shahidi huyo alieleza historia yake ya kikazi, akisema alijiunga na Jeshi la Polisi tarehe 28 Aprili 2003 kama polisi wa kawaida na baadaye alipandishwa vyeo kwa hatua mbalimbali kutokana na utendaji wake.
Mwaka 2006 alichaguliwa kwenda kwenye mafunzo ya ukaguzi wa polisi, na mwaka 2008 alipandishwa cheo kuwa Mkaguzi Kamili wa Polisi. Aidha, alifafanua kuwa elimu yake ya kipolisi aliipata katika Chuo cha Polisi Moshi, ambapo alipata mafunzo ya awali na ya juu kuhusu upelelezi wa jinai, usimamizi wa sheria na uongozi wa jeshi la polisi.
ACP Bagemu alisema kuwa siku ya tarehe 4 Aprili 2025, akiwa katika ofisi yake ya Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, alikaimu nafasi ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (ZCO), kwa kuwa aliyekuwa anashikilia wadhifa huo kwa wakati huo, Afande Faustine Mafwele, alikuwa nje ya mkoa kwa shughuli za kikazi.
Shahidi alieleza kuwa ilikuwa ni siku ya kawaida ya kazi hadi majira ya saa nne asubuhi, alipomtembelea ofisini kwake afisa wa doria mtandaoni, Assistant Inspector John Kahaya, ambaye alifika na taarifa muhimu alizozipata wakati akitekeleza majukumu yake ya kufuatilia shughuli za mitandaoni.
Kwa mujibu wa ushahidi wake, Kahaya alimwambia kuwa akiwa katika kazi zake aliona video katika mtandao wa YouTube kupitia kituo cha Jambo TV, yenye kichwa cha habari “Tundu Lissu uso kwa uso na watia nia: No Reform No Election”. Alisema maudhui ya video hiyo yalionekana kuwa na maneno ya uchochezi na kauli zilizokuwa na viashiria vya makosa ya jinai, jambo lililomsukuma kufika ofisini kwa bosi wake kumjulisha.
ACP Bagemu aliendelea kueleza kuwa baada ya kupokea taarifa hizo, alimwomba afisa huyo amuonyeshe video hiyo. Kwa kutumia simu yake janja, Kahaya alifungua mtandao wa YouTube na kuonesha kipande cha video kilichomuonesha Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Antiphas Lissu, akizungumza katika tukio la kisiasa. Alisema kuwa sehemu alizoonyeshwa zilihusisha maneno ambayo kwa maoni yake yalikuwa na viashiria vya uchochezi dhidi ya Serikali.
Katika ushahidi wake, ACP Bagemu alinukuu baadhi ya kauli zilizokuwa zikitolewa na Lissu ndani ya video hiyo, akisema kuwa alisikika akidai kwamba polisi hubeba vibegi vyenye kura feki na kwenda navyo katika vituo vya kupiga kura, na kwamba majaji wengi wa mahakama ni watu wa chama tawala CCM, wanaopendelea kwenda kwenye Tume ya Uchaguzi kwa sababu huko ndiko kwenye fedha.
Aidha, Shahidi aliendelea kusema Lissu alisikika akisema: “Ni kweli tunakwenda kuzuia uchaguzi, tunakwenda kuhamasisha uasi, kukinukisha sanasana, kuvuruga kwelikweli, kukinukisha vibaya sana.” Kwa mujibu wa shahidi, kauli hizi zilionekana kuashiria dhamira ya kuhamasisha wananchi kupinga au kukwamisha uchaguzi.
ACP Bagemu aliiambia Mahakama kuwa baada ya kushuhudia mwenyewe video hiyo, aliamua kuchukua hatua za haraka za kisheria kwa kufungua jalada la uchunguzi lililopatiwa namba DSMZ/CID/PE.101/2025, kwa lengo la kubaini uhalisia wa video hiyo na uhalali wa maudhui yake. Alisema sababu kuu ya kufungua jalada hilo ilikuwa ni kubaini kama video hiyo ilikuwa halisi au imetengenezwa kwa mbinu za teknolojia, na pia kutambua wahusika wa Jambo TV waliorekodi na kuchapisha maudhui hayo.
Baada ya kutoa maelekezo hayo, ACP Bagemu alisema aliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI) na kumtaarifu juu ya hatua aliyochukua.
Kwa mujibu wa maelezo yake, DCI alimwagiza aendelee na uchunguzi wa awali huku akiwasiliana na Kamishna Msaidizi wa Polisi Ramadhan Ng’anzi, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Jinai Mtandaoni. Hatua hiyo ililenga kuhakikisha uchunguzi unafanywa kwa ushirikiano kati ya vitengo husika vya polisi, ikiwemo idara ya uhalifu wa mtandaoni na upelelezi wa kawaida.
ACP Bagemu alieleza kuwa tarehe 6 Aprili 2025 alifanya mawasiliano na uongozi wa Jambo TV kutaka kujua kama video hiyo ilikuwa imerekodiwa na kituo chao. Kwa mujibu wa majibu aliyoyapata, video hiyo kweli ilikuwa imerekodiwa na mmoja wa wapiga picha wa kituo hicho aliyejulikana kwa jina moja la P( Shahidi wa siri) ambaye kwa wakati huo alikuwa Dodoma kikazi. ACP Bagemu alipewa namba ya simu ya mtu huyo na kisha akamjulisha Afande Ramadhan Ng’anzi kuhusu uwepo wake ili mawasiliano yafanyike kwa ajili ya kuchukua maelezo yake rasmi.
Siku iliyofuata, tarehe 7 Aprili 2025, ACP Bagemu alitoa maelekezo kwa Assistant Inspector John Kahaya kupakua video hiyo kutoka YouTube na kuihifadhi katika kifaa maalum cha memory card kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi wa makosa ya jinai. Video hiyo ilipelekwa kwa Assistant Inspector Peter Malugala, ambaye ni mtunza vielelezo wa Jeshi la Polisi, ili iandaliwe kama kielelezo cha ushahidi. Maelezo ya aliyerekodi video hiyo, yaani Bwana P, yalichukuliwa rasmi na kuandikwa na Assistant Inspector Michael Gyumi.
ACP Bagemu aliiambia Mahakama kuwa baada ya kupokea nakala ya video hiyo, aliitazama kwa makini na kubaini kuwa ilikuwa video halisi iliyorekodiwa bila uhariri. Alisema video hiyo ilikuwa na urefu wa takribani masaa matatu na ilikuwa na maudhui yanayoonesha hotuba ndefu ya Tundu Lissu mbele ya waandishi wa habari.
Baada ya kuchunguza video hiyo, ACP Bagemu alisema aliona kuwa kulikuwa na ushahidi wa wazi unaoashiria kosa la uhaini na kosa la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Shahidi huyo aliendelea kusema kwamba alielekeza kufunguliwa majalada mawili ya uchunguzi tofauti, moja likihusu kosa la uhaini lililopatiwa namba CDS/IR/727/2025, na jingine likihusu kosa la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni lililopatiwa namba CDS/IR/761/2025.
Kwa mujibu wa ushahidi wake, kosa la uhaini lilitokana na maneno aliyoyatoa Lissu ambayo kwa tafsiri ya kisheria yalionekana kuwa na dhamira ya kuishinikiza serikali kufanya maamuzi nje ya utaratibu wa kikatiba, hasa kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu.
ACP Bagemu alisema kuwa kauli hizo zilitafsiriwa kama jaribio la kuchochea uasi dhidi ya serikali. Amesema kutokana na uzito wa tuhuma hizo, alimteua Assistant Commissioner wa Polisi Amini Makhamba kuongoza timu maalum ya upelelezi wa kesi hiyo.
ACP Bagemu aliendelea kueleza kuwa tarehe 9 Aprili 2025 usiku alipokea taarifa kutoka kwa DCP Ramadhan Ng’anzi kwamba mtuhumiwa Tundu Lissu alikuwa amekamatwa wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, na alikuwa akisafirishwa kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano rasmi. Alisema kuwa siku iliyofuata, tarehe 10 Aprili 2025, majira ya saa nne asubuhi, Lissu alifikishwa ofisini kwake akiwa katika hali nzuri kiafya. Baada ya muda mfupi, mawakili wake wanne walifika na kujitambulisha kuwa ni sehemu ya timu ya utetezi, akiwataja kuwa ni Dickson Matata, Hekima Mwasipu na Jebra Kambole, pamoja na mwingine ambaye hakukumbuka jina lake.
ACP Bagemu alisema kuwa baada ya utambulisho huo, alimuomba Lissu waende kwenye chumba cha mahojiano kilichoandaliwa kwa ajili ya kuchukua maelezo yake. Alisema alimtaarifu Lissu kuhusu makosa yanayomkabili kosa la uhaini chini ya kifungu cha 39(2d) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, na kosa la kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Aidha, alimjulisha kuhusu haki zake za kisheria, ikiwemo haki ya kupata wakili, ndugu au rafiki wakati wa mahojiano, na kumhakikishia kwamba hatalazimishwa kusema lolote. Alisema baada ya kumwuliza kama amezielewa haki hizo, Lissu alikubali kwa maandishi na kusaini fomu maalum ya uthibitisho.
Baada ya hapo, ACP Bagemu alisema alimpa Lissu karatasi na kalamu ili aandike mwenyewe maelezo yake au achague kuyatoa kwa maneno huku yeye akirekodi. Kwa mujibu wa ushahidi wake, Lissu aliamua kuandika mwenyewe na aliandika maneno mafupi yaliyosomeka: “Maelezo yangu nitayatoa Mahakamani.”
Wakati wa kuhojiwa zaidi na wakili wa serikali kuhusu maudhui ya video iliyosababisha kesi hii, ACP Bagemu alisema kuwa katika video hiyo Lissu alionekana akiwa amevaa mavazi ya kijeshi ya rangi ya kaki, nyuma yake kukiwa na bendera ya Taifa. Alisema mtuhumiwa alionekana akihutubia huku akitoa kauli zenye mwelekeo wa kuhimiza maandamano na uasi dhidi ya mamlaka.
Aliongeza kuwa kwa sababu video hiyo ilichapishwa na kusambazwa kwa makusudi kupitia mitandao ya kijamii, ilikuwa na lengo la kuwafikia Watanzania na hata watu wa nje ya nchi, jambo lililodhihirisha nia ya kuchapisha taarifa hizo kwa uenezi mpana.
Baada ya maelezo hayo upande wa Jamhuri ulihitimisha maswali kwa shahidi na kuiomba Mahakama ihairishe shauri hilo kutokana na muda kuwa sio rafiki na kwamba iendelee kesho kwa hatua ya maswali ya dodoso ambayo yatafanywa na upande wa mtuhumiwa anaejiwakilisha mwenyewe katika kesi hiyo.
Kesi imeahirishwa mpaka kesho Oktoba 7,2025 saa tatu asubuhi.