Mshtakiwa wa kesi ya Uhaini Tundu Lissu leo alisimama mahakamani kupinga hatua ya upande wa mashtaka kuwasilisha vielelezo vya video na kifaa cha kuhifadhia taarifa (memory card na flash disk) kama sehemu ya ushahidi katika kesi ya Uhaini inayoendelea Mahakama Kuu, akidai kuwa vielelezo hivyo havijawasilishwa kwa kufuata utaratibu wa kisheria.
Lissu aliwasilisha hoja zake baada ya shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri kuendelea kutoa ushahidi wake kwa siku ya pili mfululizo, akihojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Thawabu Issa kuhusu uchunguzi wa kitaalamu alioufanya kwenye video inayodaiwa kumhusu Lissu.
Shahidi huyo, ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa vielelezo vya kidijitali kutoka Jeshi la Polisi, aliieleza Mahakama namna alivyopokea barua za maombi ya uchunguzi, maandalizi aliyoyafanya maabara, na taratibu za kisayansi alizozitumia kuthibitisha uhalisia wa video husika.
Hata hivyo, mara baada ya upande wa mashtaka kuomba vielelezo hivyo vipokelewe rasmi kama ushahidi wa Mahakama, Lissu alipinga vikali akitoa sababu nne za kisheria za kupinga hoja hiyo.
Akizungumza mbele ya majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo, Lissu alidai kuwa vielelezo hivyo “havina sifa za kupokelewa” kwa kuwa havikusomwa katika Mahakama ya Ukabidhi (Committal Court), hivyo vinakiuka kifungu cha 263 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA)
“Kifungu hicho kinataka nyaraka zote ambazo upande wa mashtaka unakusudia kuzitoa kama ushahidi, ziwasilishwe na kusomwa katika Mahakama ya Ukabidhi. Video hizi hazikusomwa Kisutu, kwa hiyo haziwezi kuletwa moja kwa moja Mahakama Kuu,” alisema Lissu.
Akinukuu maamuzi ya Mahakama ya Rufani katika kesi za Mussa Ramadhani Magaya dhidi ya Jamhuri na Remina Omary Abduli dhidi ya Jamhuri Lissu alisema kutosomwa kwa vielelezo hivyo hatua ya awali kunafanya ushahidi huo “kutokubalika kisheria.”
Katika hoja zake, Lissu pia alidai kuwa upande wa mashtaka umevuruga utaratibu wa ushahidi wa kitaalamu kwa kuanza na video badala ya taarifa rasmi ya mtaalamu.
“Ripoti ya kitaalamu ndiyo ushahidi halisi kwa mujibu wa vifungu vya 216 hadi 219 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Haiwezekani vielelezo viletwe kabla ya ripoti ya kitaalamu,” alisisitiza.
Aidha, alitilia shaka hadhi ya shahidi huyo kama “mtaalamu anayetambuliwa kisheria,” akidai hakuna ushahidi wa kuteuliwa kwake na Mkurugenzi wa Mashtaka au tangazo la Serikali linalomtambua kama mtaalamu wa video.
Sababu ya nne aliyotoa Lissu ni kuhusu mnyororo wa uhifadhi wa vielelezo (chain of custody), akidai haujaonyeshwa ipasavyo.
“Shahidi amesema alipokea video kutoka kwa Afisa wa Upelelezi, lakini hakueleza zilipotoka kabla ya hapo. Bila uthibitisho wa kimaandishi wa mnyororo huo, vielelezo hivi haviwezi kukubalika,” alisema.
Awali kabla ya pingamizi hilo, Wakili wa Serikali Thawabu Issa aliendelea kumuhoji shahidi huyo ambaye ni Mkaguzi wa Polisi Samweli Kahaya kuelezea ushahidi wake wa kitaalam alioanza kuutoa hapo jana.
Wakili Thawabu:Umefika maabara baada ya kuambiwa uendelee na uchunguzi, nini kilifuata?
Shahidi: Nilifanya maandalizi ya vifaa vyangu vya uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kompyuta maalum na printer. Nilipitia barua mbili nilizopokea, moja ikihusu uchunguzi wa taarifa za uongo mtandaoni, na nyingine kesi ya uhaini yenye kumbukumbu DA.223/476/01B/169.
Wakili Thawabu:Barua hiyo ilikuagiza ufanye nini?
Shahidi:Ilihitaji nichunguze chanzo cha picha mjongeo iliyoko kwenye flash disk na memory card, kuthibitisha uhalisia wa maudhui, na kulinganisha maudhui ya vifaa hivyo viwili. Pia nilitakiwa kuchunguza iwapo maneno haya yapo katika video: “Wanasema hivii msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli kabisa maana tutazuia uchaguzi hivyo tutahamasisha uasi hiyo ndiyo namna ya kupata mabadiliko tunaenda kukinukisha sanasana uchaguzi huu tutauvuruga maana tutaenda kukinukisha vibaya sana”
Wakili Thawabu:Ulitumia vifaa na programu gani katika uchunguzi huo?
Shahidi: Nilihakiki kompyuta maalum yenye Windows 11 na programu za uchunguzi za AMPED FIVE na AMPED AUTHENTICATE ambazo hutumika kuongeza ubora na kufanya uchambuzi wa picha na video. Pia nilitumia Kaspersky Antivirus kulinda vielelezo dhidi ya virusi.
Wakili Thawabu: Ulipata nini baada ya kufungua flash hiyo?
Shahidi: Niliona video yenye kichwa “Tundu Lissu Uso kwa Uso na Watia Nia Majimboni – No Reforms No Election Njia Panda” yenye muda wa saa tatu na dakika 38. Nilithibitisha video hiyo ni halisi, haina pandikizi wala “jump cuts”
Wakili Thawabu: Baada ya uchunguzi wa kisayansi, nini kilifuata?
Shahidi:Nilifanya “Clone Analysis” na “Noise Analysis” kuthibitisha uhalisia.
Baada ya kukamilisha, niliandika ripoti ya uchunguzi na kuiwasilisha kwa mamlaka husika tarehe 8, nikimkabidhi vielelezo kwa Assistant Inspector Michael Gyumi.
Wakili Thawabu:Unaweza kutambua vielelezo hivyo?
Shahidi: Ndiyo. Flash disk ina ukubwa wa GB 8 na sticker yenye maandishi “DM”. Memory card aina ya Aldeepo ina GB 32, rangi nyekundu na nyeusi, na ilikuwa na video clip 25.
Kesi imeahirishwa mpaka Oktoba 20,2025 Jumatatu saa tatu asubuhi ambapo upande wa Jamhuri watakuja kujibu hoja zilizoibuliwa kwenye pingamizi la Lissu kuhusu vielelezo kupokelewa kama ushahidi Mahakamani.
Tundu Lissu ambaye Mwenyekiti wa Chadema anaekabiliwa na shtaka la Uhaini analodaiwa kulitenda Aprili 3, 2025 akiwa jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.
Alikamatwa kwa mara ya kwanza mkoani Ruvuma mnamo Aprili 9, 2025 na kufikishwa Mahakama ya Kisutu Aprili 10,2025.