Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, imewahukumu vijana wanne kifungo cha miaka saba jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo.
Wakati huo huo, washtakiwa wawili wameachiliwa huru kutokana na ushahidi kushindwa kuthibitisha ushiriki wao katika tukio hilo.
Waliohukumiwa ni Fredrick Nsato (21), askari mkazi wa Kibamba; Isaack Mwaifuani (29), bondia kutoka Kimara; Benki Mwakalebela (40), wakala wa mabasi katika Stendi ya Magufuli; na Bato Tweve (32), bondia mkazi wa Kimara Bonyokwa.
Waliyoachiwa huru ni Nelson Msela (24), dereva teksi, na Anitha Temba (27), baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Ramadhani Rugemalira alisema ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha bila kuacha shaka kuwa washtakiwa hao wanne walihusika katika jaribio la kumteka Tarimo, ingawa hawakufanikiwa kulitekeleza.
“Washtakiwa wote wanne mnahukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la kujaribu kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo, kwa kuwa ushahidi umeonyesha walikuwa kwenye harakati ambazo hazikufanikiwa,” alisema Hakimu Rugemalira.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu, upande wa mashtaka uliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa jamii. Kwa upande wao, washtakiwa waliomba kupunguziwa adhabu, wakidai walidanganywa na Nsato kwamba walikuwa wakishiriki katika kumkamata mtuhumiwa.
Itakumbukwa kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 11, 2024, katika eneo la Kiluvya Madukani, Wilaya ya Kinondoni. Inadaiwa washtakiwa walipanga kumteka Tarimo kwa kutumia mtego uliopangwa na Anitha Temba, ambaye alimshawishi mfanyabiashara huyo wakutane kwenye hoteli kwa mazungumzo ya kibiashara.
Baada ya Tarimo kufika katika eneo aliloelekezwa, alisubiri kwenye baa kama alivyoambiwa, ndipo washtakiwa walipofika kwa gari aina ya Toyota Raum lenye namba T 237 EGE na kujaribu kumteka, lakini mpango huo ukashindikana.