Taarifa hiyo ya ACT Wazalendo ambayo imetolewa leo Alhamisi Novemba 6, 2025, imeeleza kuwa matukio hayo si uvunjifu wa haki za binadamu tu bali pia mamlaka zimekosa utu kwa kutozingatia misingi ya utawala bora.
Chama cha ACT Wazalendo, kupitia kikao cha Kamati ya Uongozi Taifa, kimelaani vikali ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa dhidi ya wananchi kuanzia tarehe 29 Oktoba 2025, katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, kimelaani kwa nguvu zote vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyofanywa dhidi ya wanachama na wagombea wake katika mchakato wa Uchaguzi, ikiwamo kuuawa kwa mgombeawao wa udiwani wa kata ya Sirari Jimbo la Tarime (Mkoa wa Mara) Bi. Dafroza Jacob, ambaye inadaiwa ameuawa kutokana na mateso akiwa katika mikono ya Polisi baada ya kukamatwa jambo lililopelekea kifo chake tarehe 5 Novemba, 2025.
Taarifa hiyo ya ACT Wazalendo ambayo imetolewa leo Alhamisi Novemba 6, 2025, imeeleza kuwa matukio hayo si uvunjifu wa haki za binadamu tu bali pia mamlaka kukosa utu kwa kutozingatia misingi ya utawala bora.
“Tunatoa pole za dhati kwa familia za waliopoteza wapendwa wao, na tunawaombea majeruhi wote wapone haraka. Taifa letu limepoteza ndugu, watoto na wazazi ambao walikuwa na ndoto za kulitumikia taifa kwa namna zao. Maumivu haya ni yetu sote”- imesema taarifa hiyo ambayo imetolewa na Kiongozi wa chama hicho Dorothy Semu.
Pamoja na hayo ACT Wazalendo imetaka uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu matukio ya tarehe 29/10/2025 na siku zilizofuata na waliohusika kufanya mauaji dhidi ya waandamanaji kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
“Tunataka wote waliohusika waliotoa amri, waliotekeleza, au waliokaa kimya kuficha ukweli wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.Tunaitaka Serikali ikomeshe mara moja matumizi ya nguvu dhidi ya raia na ianze safari ya majadiliano ya kitaifa kwa kusikiliza kila sauti ya wananchi” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Kadhalika wametaka madai ya mageuzi kikatiba na kisheria kufanyiwa kazi haraka kama sehemu ya kulirejesha taifa pamoja.
“Madai yote ya mageuzi ya kikatiba, kisheria, kiutawala, kimfumo na kitaasisi ambayo yamekuwa yakitolewa na kupaziwa sauti tokea kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi yafanyiwe kazi haraka ikiwa ni sehemu na hatua za msingi zinazohitajika kulirejesha taifa letu pamoja”
Chama cha ACT Wazalendo ambacho ni chama cha upinzani cha pili kwa ukubwa, kimejizoelea umaarufu kwa haraka nchini Tanzania licha ya kuwa sio kikongwe kama vilivyo vyama vingine katika medani za siasa.
Chama hicho ambacho miongoni mwa waasisi wake ni aliyekuwa Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe, kilishiriki hatua zote za uchaguzi licha ya uwepo wa mazingira magumu, kwani kiliamini katika ushindi wa mabadiliko. Hata hivyo mgombea wake wa Urais kwa Tanzania Bara alikwaa kisiki kutokana na vikwazo kadhaa kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, hali iliyofanya ACT Wazalendo kukosa mgombea Urais wa Tanzania.