Samia aunda Tume kuchunguza ghasia za uchaguzi, atoa wito wa maridhiano na kuahidi mchakato wa Katiba Mpya ndani ya siku 100

Katika hotuba yake ya kwanza mbele ya Bunge la 13 jijini Dodoma tangu kuanza kwa muhula wake mpya, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo ametoa msimamo mzito kuhusu masuala ya ghasia za uchaguzi, maridhiano ya kitaifa, nafasi ya vijana, na mwelekeo wa mageuzi ya kisiasa ikiwemo mchakato wa Katiba Mpya. 

Awali kabla ya kuanza hotuba yake, Rais Samia aliwataka wabunge wote kusimama kwa dakika moja kuwaombea wale wote waliofariki kutokana na vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29,2025.

Rais Samia amesema amesikitishwa na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoripotiwa kutokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi uliopita, na kusisitiza kuwa serikali haitayafumbia macho. 

Akitangaza hatua ya serikali kuunda Tume maalum ya uchunguzi, alisema uchunguzi huo utakuwa msingi wa kuelewa chanzo cha migogoro na kuchukua hatua za kurejesha maelewano ya kitaifa.

“Mimi binafsi nimeuzunishwa sana na tukio. Natoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao, na tunaomba Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani. Aidha, kwa majeruhi tunawaombea wapone haraka, na kwa wale waliopoteza mali zao tunawaomba wawe na uvumilivu. Serikali imechukua hatua ya kuunda Tume ya kuchunguza yaliyotokea ili kujua kiini cha tatizo. Taarifa hiyo itatuongoza kujielekeza katika kuleta mazungumzo ya maelewano na amani,” alisema Rais Samia.

Maandamano ya Oktoba 29,2025 yaliripotiwa kusababisha vifo vya watu kadhaa huku zaidi 500, wakishtakiwa kwa makosa ya Uhaini katika maeneo mbalimbali ya nchini.

Rais Samia ametoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao kufuatia ghasia hizo.

-Awataka vijana kutokubali kubomoa taifa-

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais Samia aliwataka vijana wa Tanzania kujiepusha na vitendo vya fujo, ushabiki usio na tija, au kushiriki katika matukio ya uvunjifu wa amani. Kwa lugha iliyojaa msisitizo,  Samia aliwakumbusha vijana kuwa wao ndio nguvu kuu ya kulijenga taifa.

“Kwa wanangu vijana wa Tanzania, sisi wazazi wenu kama tungeyafanya mliyoyafanya ninyi, nchi isingekuwa na mema na maendeleo. Hivyo niwasihi sana wanangu vijana wa Tanzania, nchi hii ni yenu. Kwa shida zozote zinazowakabili, msikubali hata siku moja… hili nawaomba mlikatae kwa nguvu zote. Ninyi ndiyo walinzi na wajenzi wa taifa hili. Nawashauri kamwe msije kuwa wabomoaji wa taifa lenu,” alisema Rais Samia.

Itakumbukwa kuwa katika maandamano hayo yaliyodumu kwa takribani siku tatu, vijana ndio walionekana vinara wakiishinikiza serikali iliyopo madarakani kuachia madaraka baada ya miaka 60 kutawala huku changamoto zikiwa lukuki.

– Aielekeza Ofisi ya DPP kuwaachia vijana waliokabiliwa na mashtaka ya uhaini-

Katika hatua isiyotarajiwa lakini iliyoonekana kama ishara ya maridhiano ya kisiasa, Rais Samia ameielekeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupitia upya kesi za vijana waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini katika matukio ya kisiasa. Ameeleza kuwa baadhi ya vijana waliingia katika makosa hayo kwa ushabiki au kufuata mkumbo bila ufahamu wa kutosha kuhusu uzito wake.

“Kuna wakati vijana hufuata mkumbo wa uhalifu kwa ushabiki. Ninatambua vijana wengi waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya. Nikiwa mama na mlezi wa taifa hili, ninaielekeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu. Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wawafutie mashtaka yao,” alisema.

Kauli hii imezua mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakiiita “hatua ya ujasiri” huku wengine wakitaka mabadiliko ya mfumo mzima wa sheria za makosa ya uhaini ambazo mara nyingi zimekuwa zikilalamikiwa kutumiwa vibaya kisiasa.

 

Asema walioandamana siku ya uchaguzi wengi hawakujua wanachofanya

“Ukiangalia clip zile za maandamano unaona kabisa kuna vijana walikuwa wameingia kwa kufuata mkumbo… wanaimba kwa kufuata ushabiki, hawakuwa wanajua wanalolifanya. Kwa hiyo, kama mlezi, kama mama, ndiyo maana nawaelekeza vyombo vya ulinzi na usalama, hasa Ofisi ya DPP, kuchuja viwango vya makosa. Kwa wale waliofuata mkumbo basi waseme nao, kisha wawaachie waende kwa wazazi wao,” alisema.

 

-Ataka taifa lijifunze kutokana na mapito ya kisiasa-

Katika ujumbe wake mpana zaidi kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini, Rais Samia alihimiza Watanzania kujifunza kutokana na changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizopita. Alisisitiza kuwa ingawa Tanzania inalizingatia misingi ya demokrasia, bado kunahitajika mwendelezo wa marekebisho na majadiliano ya kitaifa kuhusu namna ya kuimarisha mfumo huo.

“Ndugu zangu Watanzania, tujifunze kutokana na mapito yetu. Hapana shaka kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, ila neno ‘demokrasia kamili’ linaweza kutafsiriwa kwa mitazamo tofauti. Haina tafsiri moja. Kama taifa tunaendelea kujifunza na kujirekebisha. Hivyo sote kwa umoja wetu tunapaswa kutumia fursa hii kuendelea kujifunza, tujirekebishe, na tukubaliane jinsi ya kuendesha nchi yetu kidemokrasia kwa kuzingatia tamaduni, mila na desturi zetu – na sio za kuletewa,” alisema.

Katika kuhitimisha hotuba yake, Samia alisisitiza dhamira yake ya kuendeleza mkondo wa siasa za maridhiano ambazo amekuwa akizipigia chapuo tangu achukue hatamu za uongozi. Alisema kuwa kwa kuwa Watanzania wamempa ridhaa kuendelea kuongoza, hatosita kuendeleza juhudi za kuwajenga upya wadau wote wa kisiasa.

“Kwa kuwa wananchi wa Tanzania wamenipa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi hii, sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano. Ni matumaini yangu wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano ili kwa pamoja tujenge mazingira mwafaka kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema.