
Barabara zenye vumbi za Dar es Salaam, jiji kubwa zaidi nchini Tanzania, zinaficha siri nzito. Katika eneo la mbali la makaburi ya Kondo, kaskazini mwa jiji, lipo kaburi la pamoja lililofunikwa na utata na hofu. Miili ya waandamanaji waliouawa baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 ilizikwa kwa siri katika makaburi ya Kondo.
Uchunguzi wa CNN umefichua ukweli wa kutisha, ukionyesha mwenendo wa ukatili wa polisi na uwezekano wa ukiukwaji wa haki za binadamu. Picha za satelaiti zinaonyesha udongo uliochezewa, tofauti na utulivu wa maeneo jirani. Vyanzo vya ndani vinasema kuwa vijana walipewa fedha kuchimba na kuzika miili hiyo.
Waathiriwa, wengi wao wakiwa hawana silaha, walipigwa risasi na polisi, miili yao ikitupwa kama takataka. Mwanamke mjamzito ambaye alijikuta katikati ya vurugu alifyatuliwa risasi mgongoni wakati akijaribu kukimbia. Daktari aliyewahudumia majeruhi aliripoti muundo wa kutisha wa majeraha ya risasi, hasa kichwani, tumboni, kifuani na kwenye miguu.
Majibu ya serikali yamekuwa duni, huku Rais Samia Suluhu Hassan akidai kuwa waandamanaji walilipwa ili kusababisha vurugu. Samia pia anadai kuwa baadhi ya waandamanaji walitoka nje ya nchi.
CNN pia imepitia na kuthibitisha video na picha kadhaa zinazoonyesha raia wakiwa wamekufa kutokana na risasi, pamoja na picha za miili kuzidi uwezo wa kuhifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure jijini Mwanza na Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Wakati dunia ikishuhudia, watetezi wa haki za binadamu na viongozi wa dini wanaitaka serikali ya Tanzania kuwajibika kwa ukatili huu.
“Kaburi la pamoja katika makaburi ya Kondo ni ukumbusho mkali wa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini. Ni wakati wa haki, uwazi na uwajibikaji,” walisema watetezi wa haki za binadamu.
Kwa mujibu wa upinzani, zaidi ya watu 2,000 walipigwa risasi na kufa na polisi wakati wa wiki ya maandamano yaliyoanza Oktoba 29, 2025. Watu kadhaa walipata majeraha mabaya ya risasi, huku wengine hawajulikani walipo.
Chanzo CNN