Dk Mpango: Mahakama za Afrika zisipendelee

Makamu wa Rais nchini Tanzania, Dk Philip Mpango amesema mahakama za Afrika zinapaswa kuwa huru, zisizo na upendeleo na zenye kudhibiti rushwa na zinazozingatia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama).

Dk Mpango ameyasema  hayo jana wakati ufunguzi wa mkutano wa tano wa majadiliano ulioandaliwa na Umoja wa Mahakama za Afrika.

Alisema suala la mahakama kuwa huru na isiyo na upendeleo ni la msingi ili kujenga imani kwa wananchi, huku akitolea mfano wa namna ambavyo mihimili ya serikali ya Tanzania inavyoafanya kazi bila kuingiliana

“Kwa mfano, Katiba ya Tanzania inatenganisha utendaji wa mihimili ambayo ni mahakama, bunge na serikali na haviingiliani katika kazi zao,” alisema Dk Mpango.

Alisema ingawa Katiba humpa Rais wa Tanzania mamlaka ya kuteua majaji lakini wanapoteuliwa tu mikono yake hufungwa na kumuacha jaji husika kufanya kazi yake kwa uhuru.

“Inaonekana ule msemo maarufu kwamba wakili mzuri ni yule anayemjua jaji na si sheria ni wa kweli. Maana wapo mawakili wasio waaminifu wanaotumia majaji, mahakimu na makarani kwa faida ya wateja wao,” alisema.

Aidha alizitaka mahakama ziongeze uwazi na urahisi wa kufikika na pia zinapaswa kubadilika na kuanza kutumia tehama katika kuandaa, kuhifadhi nyaraka za mahakama na kusikiliza mashauri kupitia mikutano ya video.

“Kadri nilivyokua nasafiri sehemu mbalimbali nchini Tanzania nimekutana na vilio kutoka kwa wananchi kuhusu namna ambavyo hawaridhishwi na utendaji wa mahakama kama vile kesi kuahirishwa kwa muda mrefu au kutosikilizwa kwa muda mrefu,” alisema na kuongeza;

“Hii inaendana na msemo kwamba haki inayocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa. Lakini pia nilikutana na vilio kuhusu gharama kubwa za kesi lakini pia maamuzi ya kesi kuandikwa kwa lugha za kigeni, unyanyapaa dhidi ya wanawake, watu wenye ulemavu na masikini,” alisema.

Dk Mpango alikanusha madai kuwa Tanzania imejitoa uanachama katika Mahakama ya Haki za Binadamu na Watu isipokuwa imejitoa kwenye tamko la uanzishwaji wa mahakama hiyo, hatua inayoruhusu watu binafsi kuitumia.