Niffer na Chavala waachiwa huru baada ya DPP kuwafutia mashtaka ya Uhaini

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) amewafutia mashtaka na kuwaachia huru  Mfanyabiashara wa vipodozi nchini humo Jenifer Jovin (26) maarufu Niffer na Mika Lucas Chavala mwenye taaluma ya habari, ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya uhaini.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Disemba 3, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, baada wakili wa Serikali, Titus Aron kuileleza Mahakama hiyo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania( DPP) hana nia ya kuendelea na mashtaka shidi ya washtakiwa hao wawili.

DPP amewafutia kesi hiyo ya chini ya kifungu namba 92(1) Cha Sheria ya Makosa ya Jinai, Sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.

Itakumbukwa kuwa Niffer na Chavala walikuwa wanakabiliwa na kesi ya uhaini yenye mashtaka matatu, ambapo inadaiwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili Mosi na Oktoba 29, 2025 walikula njama za kutenda kosa la uhaini.

Katika shtaka la pili Niffer na wenzake wanadaiwa, Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali Wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano Tanzania walitengeza nia kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Wanadaiwa kuwa  walitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwenye mali za Sarikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.

Shtaka la tatu ambalo ni la uhaini linamkabili Niffer pekee yake.

Anadaiwa kati ya Agosti Mosi na Oktoba 24, 2025, alionesha nia ya kutenda uhaini kwa kuwahamasisha umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 na kwamba alithibitisha nia hiyo kwa kuwahamasisha watu kununua vifaa vya kujikinga na mambomu ya machozi dukani kwake.