
Wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameelezea jinsi majirani walivyokatwa na kuuliwa na namna walivyowapoteza watoto katika machafuko walipokimbilia Rwanda kujinusuru na mapigano mapya licha ya mkataba wa amani uliosimamiwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
“Nina watoto kumi, lakini niko hapa na watatu tu. Sijui kilichowapata wale wengine saba, wala baba yao,” Akilimali Mirindi, mwenye umri wa miaka 40, alieleza akiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarushishi wilayani Rusizi, Rwanda.
Takribani Wakongo 1,000 wameishia katika kambi hii baada ya mapigano mapya kuzuka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mapema mwezi huu.
Kundi la waasi la M23, linaloungwa mkono na Rwanda, limeuteka eneo kubwa la mashariki mwa DRC katika mwaka uliopita na limeanza tena kupanuka, likitwaa mji mwingine muhimu, Uvira, hivi karibuni.
Maelfu wamekimbia huku raia wakijikuta tena katikati ya mapigano kati ya M23, jeshi la Congo na washirika wao.
Mirindi alikuwa akiishi Kamanyola karibu na mpaka wa Rwanda wakati mabomu yalipoanza kudondoka, yakiharibu nyumba yake.
“Watu wengi walikufa, vijana kwa wazee. Niliona miili ya watu tulipokuwa tukikimbia, tukiruka juu ya baadhi yao. Niliamua kuvuka kuingia Rwanda na wengine,” alisema.
Trump aliwaalika marais wa Rwanda na DRC, Paul Kagame na Felix Tshisekedi, tarehe 4 Desemba kwa ajili ya makubaliano ya kumaliza mgogoro, lakini mashambulizi mapya yalikuwa tayari yameanza hata walipokuwa wakikutana.
“Ni wazi hakuna uelewano kati ya Kagame na Tshisekedi… Ikiwa hawatafikia makubaliano, vita vitaendelea,” alisema Thomas Mutabazi, mwenye umri wa miaka 67, katika kambi ya wakimbizi.
“Mabomu yalikuwa yanatushukia kutoka pande mbalimbali— mengine kutoka FARDC (jeshi la Congo) na wanajeshi wa Burundi, mengine kutoka M23 walipokuwa wakirudisha moto,” alisema.
“Tulilazimika kuziacha familia zetu na mashamba yetu. Hatujui chochote, lakini mzigo wa vita unatuangukia sisi na familia zetu.”
– ‘Mabomu yakitufuata’ –
Kambi hiyo iko juu ya kilima kizuri chenye mashamba ya chai, ikiwa na msaada wa kutosha kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Chakula Duniani na mengineyo.
Kuna mabweni na uwanja wa mpira kwa watoto, lakini wanawake na watoto wengi waliopo kambini walisimulia jinsi nyumba zao na mashamba yao yalivyoporwa au kuharibiwa na wanajeshi.
Jeanette Bendereza, mwenye umri wa miaka 37, tayari alikuwa amekimbia nyumbani kwake Kamanyola mara moja mwaka huu wakati wa shambulio la awali la M23, alikimbilia Burundi mwezi Februari na watoto wake wanne.
“Tulirudi walipotueleza kuwa amani imerejea. Tulipofika tukakuta M23 wakiwa madarakani,” alisema.
Kisha vurugu zikaanza upya.“Tulikuwa tumezoea kusikia risasi chache, lakini ndani ya muda mfupi mabomu yakaanza kudondoka kutoka kwa wapiganaji wa Burundi. Hapo ndipo tulipoanza kukimbia.”
Burundi imetuma wanajeshi kusaidia DRC na sasa inahisi kutishiwa zaidi kadiri M23 inavyotekeleza miji na vijiji kando ya mpaka wake.
“Nilikimbia na majirani kuelekea Kamanyola… Tulisikia mabomu yakitufuata… Sijui mume wangu yuko wapi sasa,” Bendereza alisema, akiongeza kuwa alipoteza simu yake katika vurugu.
Olinabangi Kayibanda, mwenye miaka 56, alijaribu kustahimili Kamanyola wakati mapigano yalipoanza.
“Lakini tulipoanza kuona watu wakifa na wengine wakikatika viungo kutokana na mabomu… hata watoto wakifa, ndipo tulipoamua kukimbia,” alisema.
“Nilimuona jirani yangu akiwa amekufa baada ya nyumba yake kupigwa bomu. Alikufa pamoja na watoto wake wawili ndani ya nyumba. Alikuwa pia mjamzito.”