Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amesema kwamba ataitisha maandamano iwapo Rais Yoweri Museveni atahujumu uchaguzi unaotarajiwa kufanyika wiki hii, na akaeleza kuwa angekaribisha uingiliaji kati wa Marekani.

Mpinzani wake mkuu ni mwanamuziki aliyageukia siasa, Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 43 jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi anayegombea urais kwa mara ya pili baada ya kampeni yake ya mwaka 2021 kukumbwa na ukandamizaji mkali na madai ya kuchezewa kwa kura.
“Ikiwa Jenerali Museveni atahujumu uchaguzi, tutaitisha maandamano,” Wine aliiambia AFP akiwa nyumbani kwake katika mji mkuu Kampala.
“Tumewaambia watu wasisubiri maelekezo yetu,” aliongeza.
Umoja wa Mataifa na Shirika la Amnesty International ni miongoni mwa taasisi za uangalizi zinazoishutumu serikali ya Uganda kwa ukandamizaji kabla ya uchaguzi, ikiwemo kukamatwa kwa mamia ya wafuasi wa Bobi Wine.
Kumekuwa na ongezeko la misukosuko ya kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki huku idadi kubwa ya vijana wakipinga kudidimia kwa demokrasia na ukosefu wa ajira nchini Kenya, Tanzania na kwingineko.
Wine alikiri kuwa maandamano yanaweza kusababisha ukandamizaji zaidi.
“Ninajua serikali ya Jenerali Museveni hujibu kila kitu kwa vurugu… lakini pia najua kuwa hata tawala za kikatili huangushwa na maandamano,” aliiambia AFP.
“Hatujaahidi faraja. Hatujaahidi kwamba hawatatufanyia vurugu. Lakini tumesisitiza kuwa watu wetu lazima wawe wasio na vurugu kwa sababu tunajua kutotumia vurugu hushinda vurugu.”
Alipoulizwa kama angekaribisha uingiliaji wa moja kwa moja wa Marekani, kama ilivyofanyika kwa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, Wine alisema: “Ndiyo, ningekaribisha.”
“Ninaamini msaada wowote unaokuja kwetu ni wa manufaa. Hata hivyo, msaada huo haupaswi kuwa wa kuchukua mamlaka ya nchi yetu,” alisema.
“Ninaamini kwa dhati kuwa jukumu la kuikomboa nchi yetu, kuiongoza na kuisukuma mbele liko mikononi mwa wananchi wa Uganda.”
‘Bobi ndiye Yesu wetu’

“Bobi ndiye Yesu Kristo wetu,” wanaume wawili waliokuwa kwenye pikipiki walipiga kelele wakimsindikiza gari lake.
Maelfu ya watu walikusanyika karibu na Barabara ya Gadafi katikati ya Kampala. Umati huo, uliokuwa zaidi ya vijana wa kiume waliobanana sana, uliendelea kusubiri hotuba yake kwa shangwe licha ya mvua kubwa ya ghafla.
“Tunahitaji Uganda mpya inayofanya kazi bila rushwa, yenye uhuru na ajira kwa wote,” alisema mfuasi wake, Ssalongo Adam Mwanje, kwa AFP.
“Nataka kumpigia kura Bobi Wine ili alete Uganda mpya,” alisema Marsha Madinah.
Kwa vigelegele vikubwa, Wine aliwaambia: “Ikiwa bunge linakataa kuja getoni, basi geto litakuja bungeni.”
Uwepo mkubwa wa polisi na vyombo vya usalama uliwazuia watu kubaki hadi jioni ilipoingia, lakini hakukuwa na vurugu wakati umati ulipokuwa ukitawanyika.
“Museveni si mmoja wenu. Mimi ni ninyi, na ninyi ni mimi,” Wine alisema alipohitimisha hotuba yake.