
Baada ya kusimama kwa muda takribani miezi miwili sasa kesi inayomkabili Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, inatarajiwa kuendelea tena mwaka huu 2026.
Kuahirishwa kwa kesi hiyo kulitokana na ratiba ya kawaida ya Mahakama kuingia likizo ya mwisho wa mwaka, hali iliyositisha shughuli nyingi za usikilizwaji wa mashauri nchini.
Tundu Lissu ni mwanasiasa mkongwe wa upinzani na mmoja wa wakosoaji wakuu wa sera na utendaji wa serikali nchini Tanzania, anakabiliwa na mashtaka ya Uhaini ambayo anadaiwa kuyatenda mnamo mwezi Aprili 2025. Kesi yake imeibua mjadala mpana kuhusu uhuru wa kisiasa, nafasi ya upinzani na mwenendo wa haki katika masuala yanayogusa wanasiasa.
Tangu ilipoanza, kesi hiyo imekuwa ikipitia hatua mbalimbali za kisheria, zikiwemo vikao vya awali, kuwasilishwa kwa hoja za pande zote na maamuzi ya Mahakama kuhusu mwenendo wa shauri.
Katika vikao vilivyopita, upande wa mashtaka na ule wa mshtakiwa ambapo Lissu anajitetea mwenyewe uliwasilisha hoja zao mbele ya Mahakama, kwa muktadha tofauti ikiwemo uwepo wa mapingamizi kadhaa ambayo yameamualiwa na Mahakama. Lissu amekuwa akisisitiza haki ya kusikilizwa, uwazi na kwa wakati unaofaa, kama inavyotakiwa na Katiba na misingi ya utawala wa sheria.
Mahakama ilisikiliza hoja hizo kabla ya kuahirisha kesi mwezi Novemba 12,2025, ikieleza kuwa kuahirishwa huko kulisababishwa na kufungwa kwa shughuli za Mahakama wakati wa likizo ya mwisho wa mwaka.
-Kesi ilipoishia-
Kesi hii liahirishwa siku ya Jumatano Novemba 12,2025 kwa muda usiojulikana hadi itakapopangwa ratiba mpya ya mwendelezo wa shauri hilo.
Siku hiyo ilikuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji kwa hatua ya kusikiliza shahidi wa nne wa upande wa Jamhuri ambapo shahidi huyo ni wa siri.
Kabla ya ahirisho upande wa Jamhuri ulimtambulisha shahidi wao ambaye ni P11 aliyefichwa katika kizimba cha siri cha shahidi ambapo si wafatiliaji wala mtuhumiwa waliomuona.
Hatua hiyo ilimfanya mshatakiwa Lissu kupinga utaratibu huo akisema ni utaratibu unaokiuka tafsiri ya “kizimba maalum cha shahidi” kama ilivyoelezwa katika Kanuni ya Tatu ya Ulinzi wa Mashahidi.
Lissu alitumia hoja saba kupinga utaratibu huo akijikita katika tafsiri za kanuni za ulinzi wa mashahidi lakini pia akirejea uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu kuhusu ulinzi wa mashahidi katika ombi lililotolewa na Jamhuri mapema wakati kesi hii inaanza juu ya kwamba baadhi ya mashahidi wao watakua wa siri.
“Kwa mujibu wa kanuni hizo, kizimba maalum ni eneo ambalo shahidi haonekani na mtu yeyote isipokuwa majaji. Lakini hapa, majaji wenyewe hawawezi kumuona shahidi jambo ambalo halikubaliki kisheria,” alieleza Lissu.
Aidha, Lissu alihoji uhalali wa shahidi ambaye hata mahakama na mshtakiwa hawamfahamu, akitaka ufafanuzi wa aina ya shahidi anayelindwa kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi
“Shahidi anayelindwa ni yule aliye chini ya amri ya ulinzi inayotolewa na mahakama. Swali ni, unamlindaje mtu usiyemfahamu?” alihoji Lissu.
Katika hoja nyingine,Lissu alieleza kuwa amri ya awali ya ulinzi wa mashahidi iliyotolewa na Mahakama Kuu ina ukomo, na hivyo inapaswa kufafanuliwa upya huku Kanuni ya 7(1) inayozungumzia ukomo wa amri za ulinzi na athari zake.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kujua ni muda gani amri hizo zinadumu na kama bado zina nguvu kisheria katika hatua hii ya shauri.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, upande wa mashtaka wenye mawakili wanne wakiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga, ulieleza kwamba mapingamizi yaliyotolewa na mshtakiwa yanahitaji muda zaidi kujibiwa kwa kina, kwani yanagusa vifungu kadhaa vya sheria za ndani na za kimataifa.
“Mshtakiwa amewasilisha hoja nyingi za kisheria, zikiwemo rejea za kesi, mamlaka mbalimbali na tafsiri za kimataifa. Tunahitaji muda wa kutosha kuzifanyia uchambuzi wa kina,” alisema Wakili wa Serikali Mkuu Katuga.
Hata hivyo, alikumbusha kuwa kwa mujibu wa notisi chini ya kifungu cha 215, shauri hilo lilipaswa kumalizika siku hiyo ya Novemba 12, kwani ni siku ya mwisho ya vikao vya mahakama.
Kutokana na hali hiyo, Katuga aliomba ahirisho ili wakajipange kwa ajili ya kuja kujibu hoja za mshtakiwa ambazo amezitoa.
Baada ya kusikiliza hoja hizo jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, walikubaliana na hoja ya ahirisho huku akieleza kuwa kesi hiyo itaendelea mara tu ofisi ya Msajili itakapotoa ratiba nyingine ya mwenendo wa kesi ambapo haijajulikana ni lini ratiba hiyo itatolewa hivyo itakapotolewa pande zote zitajulishwa.
Itakumbukwa kuwa kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi Septemba 28, 2025 ambapo ilianza kwa mapingamizi hadi Novemba 12, 2025 ambapo kwa mujibu wa ratiba ya mtiririko wa kesi ilifika ukomo siku hiyo ambapo ratiba hiyo ilionyesha kwamba ndio siku ya hukumu.
Hata hivyo kwa kuwa kesi hiyo haikwenda kama ratiba ilivyopangwa kwa maana bado ushahidi haujamalizika basi itaendelea pindi ratiba mpya itakapotolewa.
-Kesi inaporejea-

Kwa mujibu wa taratibu za Mahakama, kesi hiyo inatarajiwa kurejea Januari mwaka huu ingawa mpaka sasa bado haijawekwa wazi ni lini itarejea baada ya shughuli za Mahakama kuanza tena rasmi. Kinachotarajiwa katika hatua hiyo ni kupangiwa tarehe mpya ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri.
Wachambuzi wa masuala ya kisheria wanasema kurejea kwa kesi hiyo kutafungua ukurasa mpya wa mwenendo wake, ingawa bado haijabainika iwapo Mahakama itaendelea na hoja zilizokuwa zinaendelea au kuanza hatua nyingine ya kisheria.
-Muktadha wa kisiasa-
Kesi ya Tundu Lissu imekuwa ikipewa uzito mkubwa kutokana na nafasi yake katika siasa za Tanzania. Kwa wafuasi wake, kesi hiyo inaonekana kama sehemu ya changamoto pana zinazowakabili wanasiasa wa upinzani nchini humo.
Serikali, kwa upande wake, imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa Mahakama ni huru na inafanya maamuzi yake kwa mujibu wa sheria, bila kuingiliwa na mamlaka za kisiasa.
Mashirika ya haki za binadamu na baadhi ya wadau wa kiraia wamekuwa wakitoa wito wa kesi hiyo kuendeshwa kwa uwazi, haki na bila kucheleweshwa pasipo sababu za msingi.
Kwao, namna kesi hii itakavyosikilizwa ni kipimo muhimu cha hali ya utawala wa sheria na demokrasia nchini, hasa katika kipindi kinachoelekea kwenye mijadala mikubwa ya kisiasa.
-Hatma bado haijulikani-
Kwa sasa, hatma ya kesi ya Lissu bado iko mikononi mwa Mahakama. Macho ya wengi yameelekezwa Januari, wakisubiri kuona mwelekeo wa hatua inayofuata.
Kilicho wazi ni kuwa kurejea kwa kesi hiyo kutarejesha tena mjadala mpana kuhusu haki, siasa na nafasi ya Mahakama katika masuala yanayogusa viongozi wa upinzani nchini Tanzania.
Itakumbukwa kuwa Lissu ambaye sasa anazaidi ya siku 260 gerezani, alikamatwa kwa mara ya kwanza Aprili 9,2025 wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wakati akiendelea na ziara ya chama chake. Baadaye alisafirishwa hadi Dar es Salaam ambako alifikishwa Mahakama ya Kisutu Aprili 10,2025 na kufunguliwa shtaka la uhaini, shtaka ambalo kisheria halina dhamana, na hivyo kumlazimu kuendelea kusalia gerezani tangu wakati huo.