WFP yasitisha misaada katika kaunti ya Sudan Kusini baada ya msafara wao kushambuliwa

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesitisha shughuli zake katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Sudan Kusini baada ya msafara wa boti uliokuwa ukisafirisha tani 1,500 za misaada kushambuliwa na kuporwa.

Katika wiki za hivi karibuni, kumekuwepo ongezeko la ghasia kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na mpinzani wake wa muda mrefu, Riek Machar hasa katika jimbo la Jonglei ambako angalau watu 280,000 wamekimbia makazi yao, kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Jumanne.

WFP ilisema ilishambuliwa wiki iliyopita katika jimbo jirani la Upper Nile, eneo jingine linalochukuliwa kuwa ngome ya vikosi vya Machar.

“Msafara wa WFP wenye boti 12 uliokuwa ukisafirisha zaidi ya tani 1,500 za chakula muhimu cha msaada ulishambuliwa mara kadhaa na vijana wenye silaha,” ilisema katika taarifa.

Mzigo huo, ambao pia ulikuwa na vifaa visivyo vya chakula kutoka kwa washirika, uliporwa usiku kucha “bila uingiliaji wa kiusalama” kutoka kwa mamlaka za eneo hilo, WFP ilisema, licha ya ahadi zao za kuhakikisha usalama.

“WFP imesitisha shughuli zote katika Kaunti ya Baliet hadi pale usalama wa wafanyakazi wake, washirika na wakandarasi utakapohakikishwa,” ilisema, na hadi serikali irejeshe vitu vilivyoibwa.

“Mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu hayakubaliki kamwe,” WFP iliongeza.

Wiki iliyopita, WFP na shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) zililaani vikwazo vya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu katika Jonglei, huku MSF pia ikilazimika kuhamisha wafanyakazi wake kutoka kituo kimoja cha afya kutokana na mapigano ya silaha.

Sudan Kusini, nchi changa zaidi duniani, imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, umaskini na rushwa kubwa tangu ilipoanzishwa mwaka 2011.