
Wizara ya Afya nchini Tanzania imetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu ongezeko la maambukizi ya mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 (COVID-19), na kuwataka Watanzania kuchukua hatua madhubuti za kujikinga dhidi ya magonjwa hayo.
Katika taarifa yake, Wizara imesema takwimu za ufuatiliaji wa mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa hewa kwa kipindi cha mwezi Novemba hadi Aprili zinaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa la maambukizi ya mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 nchini na duniani kwa ujumla katika kipindi hicho.
Wizara imewahimiza wananchi kuzingatia tahadhari mbalimbali ili kupunguza hatari ya maambukizi. Hatua hizo ni pamoja na kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, pamoja na kuepuka misongamano isiyo ya lazima.
Aidha, wananchi wametakiwa kuvaa barakoa wanapokuwa na dalili za mafua, wanapokuwa karibu na mtu mwenye dalili, au wanapokuwa katika maeneo yenye msongamano wa watu. Pia, Wizara imesisitiza umuhimu wa kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira, pamoja na kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata matibabu stahiki pindi dalili zinapojitokeza.
Wizara hiyo imeonya dhidi ya tabia ya kujitibu au kutumia antibiotiki bila ushauri wa wataalamu wa afya, ikieleza kuwa matumizi holela ya dawa yanaweza kusababisha madhara zaidi kiafya.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 huambukizwa kupitia majimaji yanayotoka kwenye mfumo wa njia ya hewa ya mgonjwa, ambayo husambaa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza.Vilevile, maambukizi yanaweza kutokea kwa kugusa mazingira yaliyochafuliwa na majimaji hayo.
Dalili za magonjwa hayo ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo na uchovu.
Wizara imeendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kushirikiana na mamlaka za afya ili kudhibiti kuenea kwa magonjwa hayo nchini.