Mahakama Ya Afrika Leo Kutoa Hukumu Kesi Ya Uchaguzi Wa 2020 Wa Tanzania

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu inatarajiwa kutoa hukumu iliyosubiriwa kwa muda mrefu leo Ijumaa, Machi 6, 2026, katika kesi inayopinga mwenendo wa uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020.

Kesi hiyo iliwasilishwa kwa mara ya kwanza Novemba 2020 na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na mwanzilishi wa chama cha upinzani cha Civic United Front (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad. Baada ya kifo chake Februari 2021, kesi iliendelea chini ya Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa chama cha upinzani ACT Wazalendo, pamoja na waombaji wengine kutoka Tanzania.

Waombaji wanadai kuwa vitendo kadhaa vilivyotokea wakati wa uchaguzi wa 2020 vilikiuka haki za wagombea na wapiga kura. Miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa katika kesi hiyo ni kukamatwa kwa wagombea wa upinzani, kusimamishwa kwa shughuli za kampeni, kuondolewa kwa baadhi ya wagombea katika mchakato wa uchaguzi, pamoja na vikwazo vilivyowekwa kwa vyombo huru vya habari.

Waombaji pia wametaja madai ya kununua kura, kuhesabu kura kwa njia isiyo ya kawaida, pamoja na kukatizwa kwa huduma za mawasiliano, ikiwemo intaneti na majukwaa ya mitandao ya kijamii katika kipindi cha uchaguzi.

Uamuzi wa mahakama unatarajiwa kufafanua iwapo hatua zilizochukuliwa wakati wa uchaguzi wa Tanzania wa mwaka 2020 zilizingatia viwango vinavyotakiwa chini ya sheria za Afrika kuhusu haki za binadamu na uchaguzi.

Waangalizi wanasema kuwa uamuzi huo unaweza pia kuathiri mijadala ya baadaye kuhusu mageuzi ya uchaguzi na michakato ya kidemokrasia nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.

Kesi hiyo inamvuto mkubwa  kwa sababu inakuja miaka kadhaa baada ya uchaguzi wa 2020 na kufuatia mfululizo wa ucheleweshaji kabla ya mahakama kufunga mwenendo wa kesi na kupanga tarehe ya kutolewa kwa hukumu ya mwisho.Uamuzi wa Mahakama ya Afrika sasa unatarajiwa kutoa mwongozo kuhusu wajibu wa serikali wakati wa uchaguzi na ulinzi wa haki za kisiasa na kiraia za wananchi.