Leo Aprili Mosi, 2026, watumiaji wa vyombo vya moto wameshuhudia ongezeko kubwa la bei ya mafuta baada ya saa chache tu kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kutangaza ongezeko hilo la bei elekezi za mafuta nchini.
Katika Jiji la Dar es Salaam, bei ya petroli imepanda hadi shilingi 3,820 kwa lita kutoka shilingi 2,864 mwezi Machi. Dizeli imefikia shilingi 3,806 kwa lita, huku mafuta ya taa yakipanda hadi shilingi 3,684 kwa lita.
Ongezeko hili kubwa zaidi ya asilimia 33 kwa petroli na dizeli ndani ya mwezi mmoja linatokana na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati, kati ya Marekani, Israel na Iran, ulioonza tangu Februari 28, 2026.
Kwa mujibu wa EWURA, vita hivyo vimesababisha mashambulizi katika visima vya mafuta, maghala na mitambo ya kusafisha mafuta, huku kufungwa kwa Mlango wa Hormuz na Iran kukiwa na athari kubwa. Njia hii muhimu hupitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani.
Hali hiyo imesababisha upungufu wa meli za kusafirisha mafuta na kuongezeka kwa gharama za bima, jambo lililopelekea kupanda kwa bei za mafuta katika soko la Ghuba ya Uarabuni. EWURA imeeleza kuwa bei za FOB kwa Aprili zimeongezeka kwa asilimia 69.98 kwa petroli, asilimia 114.46 kwa dizeli na asilimia 120.81 kwa mafuta ya taa.
Athari za ongezeko hili zinakwenda moja kwa moja kwa wananchi wa kawaida na si hivyo tu bali ni kwa uchumi wa dunia.
Wakati wasiwasi ukiendelea juu ya ongezeko la nauli na gharama nyinginezo za uendeshaji, Serikali ya Tanzania imesema ina akiba ya kutosha ya mafuta yatakayohimili kwa takribani miezi mitatu ikiwa na zaidi ya lita milioni 563 za petroli na lita milioni 530 za dizeli.
Tofauti kati ya upatikanaji wa mafuta na bei zake nchini inatokana na mfumo wa soko la kimataifa, kwani Tanzania huagiza mafuta yote kutoka nje, hivyo bei za ndani hutegemea bei za dunia.
Aidha Serikali imeonya baadhi ya wafanyabiashara wanaoficha mafuta ili kunufaika na ongezeko la bei, ikisema hatua hiyo ni uhujumu uchumi na itachukuliwa hatua kali.
Ingawa serikali imehakikisha upatikanaji wa mafuta hadi Julai na kuunda kikosi kazi cha kufuatilia usafirishaji, changamoto ya bei nafuu bado ipo.