Serikali imezindua rasmi Mkakati wa Taifa wa miaka 10 (2026/27–2036/37) unaolenga kukabiliana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili unaoendelea kuathiri jamii na taifa kwa ujumla.
Mkakati huo unaashiria dhamira mpya ya kujenga upya misingi ya maadili, kuimarisha taasisi ya familia, na kulinda utambulisho wa taifa katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya teknolojia na kijamii.
Uzinduzi huo umefanyika leo, Aprili 29, 2026, ukiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Makonda amesema mmomonyoko wa maadili umefikia hatua ya kuathiri kwa kiasi kikubwa familia na jamii kwa ujumla.
“Tatizo la mmomonyoko wa maadili linaweza kuonekana si kubwa kwa mtazamo wa juu, lakini uhalisia wake katika familia nyingi ni mbaya na wa kutia wasiwasi. Serikali imeandaa mkakati huu wa shirikishi kwa lengo la kujenga jamii yenye utu, uzalendo, mshikamano na uwajibikaji,” amesema.
Ameeleza kuwa pamoja na maendeleo ya teknolojia na mitandao ya kijamii kurahisisha upatikanaji wa taarifa, pia yamechangia kuenea kwa maudhui hatarishi yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya, vitendo vya ukatili, lugha chafu na kudhoofika kwa misingi ya familia.
Kutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti kulinda na kuendeleza maadili ya Kitanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema utekelezaji wa mkakati huo utasaidia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga jamii yenye maadili mema, nidhamu na rasilimali watu bora kwa maendeleo endelevu.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema changamoto kubwa si uandaaji wa sera bali ni utekelezaji wake, akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha mkakati huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa jamii.