Jaji Maraga awashambulia Ruto na Samia adai wanaleta udikteta Afrika Mashariki

Jaji Mkuu Mstaafu wa Kenya David Maraga,  amewakosoa Rais William Ruto wa Kenya na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kwa kile alichokieleza kuwa ni mazungumzo ya kupanga namna ya kuzuia sauti za upinzani katika nchi zao.

Katika siku ya kwanza ya ziara ya kiserikali ya Rais Ruto nchini Tanzania, Rais Samia alimuomba Ruto kushirikiana naye kuwaadhibu vijana wa kizazi kipya maarufu kizazi cha Gen Z wanaosababisha “fujo” katika nchi zote mbili kwa kukiuka sheria kwa kisingizio cha kuminywa kwa demokrasia.

“Hakuna haja ya kugawanyika, au kusherehekea vitendo viovu vinavyotokea upande wowote. Wakionekana Kenya, hao ni wetu pia, na tunapaswa kushughulikia kwa pamoja, na vivyo hivyo inapaswa kufanyika Tanzania,” alisema Rais Samia katika hotuba ya pamoja Ikulu ya Dar es Salaam jana Jumatatu.

Maraga ambaye sasa amekua ni mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Kenya ameeleza kuwa kauli hiyo ni jaribio la viongozi hao wawili kuanzisha mfumo wa kiimla katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Raia wa Afrika Mashariki lazima waseme. Mhimili wa udikteta unaojengwa na Marais Samia na Ruto unatishia kurudisha eneo letu kwenye utawala wa kiimla,” alisema Maraga.

Jaji Mkuu Mstaafu huyo alieleza kuwa kauli hizo ni za kushtua, hasa ikizingatiwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyoripotiwa nchini Tanzania wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.

Alitaja ripoti ya Tume ya Uchunguzi iliyobaini kuwa zaidi ya watu 518 waliuawa wakati wa kipindi cha uchaguzi nchini Tanzania.

Tume hiyo, iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, ilibaini kuwa wengi wa waliopoteza maisha walikufa kwa kupigwa risasi, huku wengine wakikumbwa na majeraha ya vurugu.

Maraga pia alikosoa ukimya kuhusu madai ya mateso dhidi ya mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi na mwanaharakati wa Uganda Agather Atuhaire.

Inadaiwa wawili hao waliteswa na kudhalilishwa kingono na polisi wa Tanzania kati ya Mei 19 na Mei 23, 2025.

Wakati huo, wanaharakati hao walikuwa wamefika Tanzania kama sehemu ya ujumbe wa Afrika Mashariki kufuatilia kesi ya uhaini ya kiongozi wa upinzani nchini humo Tundu Lissu.