Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amefafanua mjadala ulioibuka hivi karibuni kuhusu upatikanaji wa huduma za matibabu kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, akisisitiza kuwa ushirikiano uliopo kati ya mifuko ya bima ya afya ya pande mbili za Muungano unaendelea kuruhusu wananchi kupata huduma bila ubaguzi.
Dkt. Nchemba alitoa ufafanuzi huo leo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Agnesta Lambert Kaiza (CHAUMA), kufuatia mjadala uliozuka baada ya kauli ya Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar Dkt Saada Mkuya, iliyotafsiriwa na baadhi ya wananchi kuwa inaeleza kwamba wasiokuwa Wazanzibari hawatatibiwa katika hospitali za Zanzibar hali iliyoonyesha ubaguzi.
Waziri Mkuu alisema suala la matibabu ni miongoni mwa maeneo yasiyo ya Muungano ambayo yanasimamiwa kwa ushirikiano wa kisera kati ya taasisi na wizara za pande zote mbili za Muungano.
Alieleza kuwa mifuko ya bima ya afya ya Taifa (NHIF) na Mfuko wa Bima ya Afya Zanzibar (ZHIF) ina makubaliano yanayowezesha wanachama wa mifuko hiyo kupata huduma za matibabu katika hospitali zilizoidhinishwa upande wowote wa Muungano.
“Mzanzibar mwenye kadi ya ZHIF anaweza kupata matibabu katika hospitali zinazopokea NHIF, na vivyo hivyo Mtanzania kutoka Bara mwenye kadi ya NHIF anaweza kupata huduma katika hospitali zinazopokea ZHIF,” alisema Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa wananchi wasiokuwa na bima za afya husika hulazimika kugharamia matibabu kwa fedha taslimu, utaratibu ambao unatumika kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Akizungumzia chanzo cha sintofahamu iliyozuka, Waziri Mkuu alisema mjadala huo ulitokana na utaratibu wa utoaji wa matibabu bila malipo kwa makundi maalumu ya wananchi wasiojiweza.
Kwa mujibu wa Dkt. Nchemba, Tanzania Bara ina mifumo ya kuwasaidia wananchi wenye uhitaji maalumu kupitia programu mbalimbali za kijamii ikiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), huku Zanzibar nayo ikiwa na taratibu zake za utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wanaostahili.
Alisema changamoto za utambuzi wa uraia na wakazi halali zipo katika pande zote za Muungano, jambo ambalo wakati mwingine huibua tahadhari katika utoaji wa huduma za kijamii zinazofadhiliwa na serikali.
“Wenzetu Zanzibar wanakabiliana na changamoto za watu kutoka mataifa mengine kupata nyaraka za ukaazi kwa njia zisizo halali ili kufaidika na huduma mbalimbali. Hili si suala la kutugawa kama Watanzania, bali ni changamoto ya kiutawala inayohitaji kushughulikiwa kwa pamoja,” alisema.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara katika sekta ya afya unaendelea kuimarika na hakuna sera inayowazuia wananchi wa pande mbili za Muungano kupata huduma za matibabu kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.