Afrika yakabiliwa na upungufu wa dawa ya usingizi kwa upasuaji wa watoto

Hospitali nyingi barani Afrika zinakabiliwa na gharama kubwa mpya huku zikihangaika kutafuta mbadala wa dawa kuu ya usingizi (anaesthesia) inayotumika kwa upasuaji wa watoto, baada ya akiba ya dawa hiyo kutarajiwa kuisha ifikapo mwaka 2027.

Halothane bado inatumika kwa kiasi kikubwa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwapa watoto usingizi wakati wa upasuaji. Sababu kuu ni kwamba dawa hiyo ni nafuu zaidi, ikiwa na gharama mara saba hadi kumi chini ya mbadala wake wa kisasa, sevoflurane.

Hata hivyo, kampuni ya mwisho iliyokuwa ikitengeneza halothane nchini India ilisimamisha uzalishaji wake mwaka 2023, na akiba iliyopo Afrika inaendelea kupungua kwa kasi.

“Hatujui hasa lini itaisha, lakini sidhani kama kutakuwa na halothane yoyote iliyobaki kufikia mwisho wa mwaka 2027,” alisema Dkt. Elizabeth Igaga, daktari bingwa wa usingizi kutoka Uganda.

Igaga ni Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Programu katika shirika la Smile Train, ambalo hufanya zaidi ya upasuaji 100,000 kila mwaka kwa watoto wenye matatizo ya ufa wa mdomo na kaakaa, ambapo asilimia 90 ya wagonjwa hao ni watoto.

“Hali ya halothane ni jambo kubwa sana kwetu. Tumejitolea kuhakikisha watoto wanapata upasuaji salama,” alisema.

Wakati hospitali za kisasa tayari zimehamia kutumia sevoflurane, hospitali hizo ni sehemu ndogo sana ya vituo vya afya vilivyopo katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mabadiliko hayo yamefichua miaka mingi ya ukosefu wa uwekezaji katika huduma za usingizi wa upasuaji barani Afrika, huku vituo vingi vikigundua kwamba mashine zao zinahitaji kubadilishwa kwa gharama ya makumi ya maelfu ya dola.

Tangazo la kusitishwa kwa uzalishaji wa halothane lilisababisha “hofu kubwa nchini kote” Zambia, kwa mujibu wa Sompwe Mwansa, Rais wa Chama cha Madaktari wa Usingizi nchini humo.

“Tunalazimika kukimbizana na mahitaji ya vifaa na mafunzo,”Kwa kweli hiki kimekuwa kipindi kigumu sana cha mpito, hasa kwa vituo vilivyo mbali na maeneo ya mijini,” aliongeza.

Katika sehemu nyingi za Afrika, dawa za usingizi hutolewa na wahudumu wa afya ambao si madaktari, na hivyo wanahitaji mafunzo mapya kuhusu matumizi ya dawa mbadala ili kuepuka upotevu wa gharama kubwa, alisema Mwansa.

Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Madaktari wa Usingizi (WFSA) mwaka 2024 lilizitaka serikali za Afrika kutenga bajeti kwa haraka ili kufanikisha mabadiliko hayo.

Kwa mujibu wa Smile Train, mwito huo bado haujapata mwitikio unaohitajika kulingana na muda uliobaki.

Hata hivyo, mabadiliko hayo yanamaanisha ongezeko la matumizi ya mamilioni ya dola katika bajeti za afya ambazo tayari zimeelemewa. Hali hiyo imechangiwa pia na kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa misaada kutoka nchi za Magharibi katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

“Hii inaweza kusababisha kupungua kwa uwezo wetu wa kufanya upasuaji,” alisema Mwansa.

“Tayari huduma za usingizi zilikuwa sehemu iliyopuuzwa katika bajeti za afya, huku kukiwa na mahitaji mengine mengi yanayoshindania fedha. Hali hii inatia wasiwasi mkubwa,” aliongeza.

Wasiwasi huo unaongezeka kutokana na ukweli kwamba Afrika ina idadi kubwa zaidi ya watoto duniani. Umoja wa Mataifa unatabiri kuwa ifikapo mwaka 2050, mtoto mmoja kati ya wanne duniani ataishi Afrika, wakati viwango vya vifo vya watoto wachanga vikiendelea kuwa vya juu.

Shirika la Smile Train linaendelea kusaidia katika mchakato wa mpito, lakini linasisitiza kuwa haliwezi kufanya kila kitu peke yake na kwamba serikali za Afrika zinapaswa kuchukua jukumu kubwa zaidi.

“Tuko tayari kusaidia, lakini pia tunahitaji serikali ziwajibike na kuchukua hatua,” alisema Igaga.