Serikali ya Tanzania imeikosoa makala iliyochapishwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kupitia kipindi chake cha BBC Africa Eye, ikidai kuwa imewasilisha taarifa zisizo na uwiano kuhusu kesi inayomkabili kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, jana Julai 13, 2026, serikali imesema makala hiyo imeegemea upande mmoja, imekosa ushahidi wa kutosha na imeacha maelezo muhimu ambayo, kwa mtazamo wake, yalipaswa kujumuishwa ili kutoa taswira kamili ya suala hilo.
Makala ya BBC Africa Eye inaeleza safari ya kisiasa ya Tundu Lissu, kuanzia maisha yake katika kijiji cha Tanzania hadi kuwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa upinzani nchini. Makala hiyo pia inaangazia jaribio la mauaji dhidi yake mwaka 2017, kipindi alichoishi uhamishoni nchini Ubelgiji, kurejea kwake Tanzania mwaka 2023 na baadaye kukamatwa kwake mwaka 2025 kwa tuhuma za uhaini.
Kupitia mahojiano na mke wake Alicia Lissu pamoja na watu wengine wa karibu, makala hiyo inaeleza athari ambazo kesi hiyo imekuwa nazo kwa familia yake na kuibua mjadala kuhusu haki, demokrasia na mazingira ya kisiasa nchini Tanzania.
-Serikali yakosoa namna taarifa ilivyowasilishwa-
Katika taarifa yake iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo bwana Gerson Msigwa, Serikali ya Tanzania imesema BBC haikutoa nafasi ya kutosha kwa upande wa serikali kueleza msimamo wake, licha ya kuwa, kwa mujibu wa serikali, ilikubali kushiriki katika maandalizi ya makala hiyo.
Serikali imedai kuwa sehemu zilizojumuishwa zilihusisha mahojiano ya viongozi wawili pekee, huku maelezo mengine yaliyotolewa na taasisi za serikali yakiachwa nje ya makala.
Aidha, serikali imeeleza kuwa chombo hicho cha habari kimeendelea kuichafua Tanzania kwa kutoa taarifa ambazo, kwa mtazamo wake, hazikuzingatia viwango vya uandishi wa habari wenye uwiano na usahihi.
-Serikali yatangaza tathmini-

Kutokana na kile ilichokiita ukiukwaji wa maadili ya uandishi wa habari, serikali imesema inaanzisha tathmini ya kina kuhusu maudhui ya makala hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tathmini hiyo ikikamilika, serikali itachukua hatua ambazo imelenga kulinda heshima, usalama na maslahi ya nchi dhidi ya kile ilichokiita mashambulizi yanayofanywa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikufafanua hatua mahsusi zitakazochukuliwa dhidi ya BBC.
Katika taarifa hiyo, serikali pia imewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, mshikamano na utulivu huku ikisisitiza kuwa itaendelea kulinda maslahi ya taifa dhidi ya taarifa ambazo inaona zinaweza kuathiri taswira ya nchi.
Kwa upande wake, BBC kupitia makala yake ilisema iliiomba serikali kutoa maoni kuhusu madai yaliyomo kwenye uchunguzi huo na ilijumuisha majibu ya serikali kuhusu mazingira ya kisiasa, uhuru wa vyombo vya habari na kesi inayomkabili Tundu Lissu.
Serikali, kwa upande wake, ilisimama kwenye msimamo kwamba hakuna aliye juu ya sheria na kwamba haiwezi kujadili kesi hiyo kwa kuwa bado ipo mahakamani.
Kwa sasa, kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu inaendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania, huku serikali na chama chake cha CHADEMA wakiendelea kutofautiana kuhusu mazingira ya kisiasa na mwelekeo wa demokrasia nchini.