Kizza Besigye hawezi kuzungumza, hali yake bado ni dhaifu – mkewe

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini akiwa katika hali ya udhaifu mkubwa na hawezi kuzungumza, mke wake Winnie Byanyima amesema.

Besigye, mwenye umri wa miaka 70 na mpinzani wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Mulago mjini Kampala baada ya kuanguka ghafla wakati kesi yake ikiendelea mahakamani Julai 30.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya hospitali hiyo Jumatatu, Byanyima alisema alimkuta mumewe akiwa amedhoofika sana.

“Nilishtuka nilipomuona. Anaonekana dhaifu sana. Alikuwa amelala kwa muda mrefu. Alipofungua macho bado hawezi kuzungumza,” alisema.

Aliongeza kuwa Besigye pia hawezi hata kuandika kutokana na mikono yake kutokuwa imara.

“Nilijaribu kumuomba aniandikie ujumbe mfupi, lakini mikono yake haikuwa imara vya kutosha kufanya hivyo,” alisema.

Kwa mujibu wa Byanyima, hadi Jumatatu Besigye alikuwa akipatiwa lishe kupitia mirija ya dawa (dripu), lakini hali yake imeanza kuonyesha nafuu baada ya kuweza kunywa supu.

“Leo tumeona dalili za maendeleo,” alisema.

Besigye alianguka mahakamani muda mfupi baada ya kupinga uamuzi wa mahakama wa kumteua mawakili wa serikali kumwakilisha. Kabla ya tukio hilo, wakili wake mkuu Erik Lukwago alikuwa amekamatwa, huku aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Kenya Martha Karua, ambaye pia ni sehemu ya timu yake ya utetezi, akizuiwa kuingia Uganda.

Byanyima aliitaka serikali ya Uganda kuhakikisha haki za msingi za mumewe zinazingatiwa, ikiwemo haki ya kuishi, kupata matibabu stahiki na kusikilizwa kwa kesi yake kwa haki.

“Siombi upendeleo wala sheria ivunjwe. Ninachotaka ni Katiba ya Uganda iheshimiwe na itumike kwa usawa kwa Dkt. Kizza Besigye kama ilivyo kwa Waganda wengine wote,” alisema.

Besigye amekuwa rumande tangu mwishoni mwa mwaka 2024 baada ya kutekwa nchini Kenya na kurejeshwa Uganda, ambako anakabiliwa na kesi ya uhaini.

Daktari huyo ambaye aliwahi kuwa daktari wa Rais Museveni wakati wa vita vya msituni vya miaka ya 1980, baadaye aligeuka kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa rais huyo na amewahi kugombea urais mara kadhaa, akidai kukabiliwa na ukandamizaji katika harakati zake za kisiasa.