Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, imeendelea Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam kwa kusikilizwa kwa ushahidi wa shahidi wa 16 wa upande wa Jamhuri.

Shahidi huyo ni Kamishna Msaidizi wa Polisi, Amini Mahamba, ambaye ndiye mpelelezi mkuu wa kesi hiyo mwenye umri wa miaka 50, ambaye amesema amekuwa akifanya kazi katika Jeshi la Polisi tangu mwaka 2000 na kwa sasa anafanya kazi katika kitengo kinachoshughulikia makosa ya mtandao, maadili ya umma na makosa yanayohusisha usalama wa nchi.
Mahamba ameiambia Mahakama kuwa Aprili 2025 alipewa jukumu la kusimamia na kuratibu upelelezi wa jalada la kesi ya uhaini inayomkabili Lissu.
Amesema baada ya kufika Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alikutana na timu ya upelelezi na kupewa maelezo kuhusu hatua ambazo zilikuwa zimefikiwa.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, moja ya hatua walizochukua ilikuwa kuangalia video ya hotuba ya Lissu iliyokuwa imechapishwa katika akaunti ya YouTube ya Jambo TV.
Amesema video hiyo iliangaliwa kwa takribani saa mbili na kwamba baada ya kuichambua, timu ya upelelezi ilibaini kuwa baadhi ya kauli za Lissu zilikuwa na viashiria vya kuhamasisha uasi na kuvuruga uchaguzi.
Shahidi ametaja kauli ambazo, kwa mujibu wake, ndizo zilizowafanya wachunguzi kuhusisha hotuba hiyo na shtaka la uhaini.
Amesema Lissu alizungumzia kuzuia uchaguzi, kuhamasisha uasi na kwenda kuvuruga uchaguzi.
Mahamba ameieleza Mahakama kuwa kwa mtazamo wa timu ya upelelezi, kauli hizo zilionyesha nia ya kushinikiza Serikali ifanye kile ambacho Lissu alikuwa akitaka, kupitia hatua ambazo zingeweza kuzuia uchaguzi mkuu.
Shahidi huyo pia amesema baada ya kukusanya majalada ya uchunguzi kutoka maeneo mbalimbali nchini, timu yake iliwatambua baadhi ya watu waliokuwa mashahidi na kuwaelekeza wapelelezi kwenda mikoani kuwatafuta na kuwachukua maelezo.
Amesema Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 akiwa Mbinga mkoani Ruvuma, kisha akasafirishwa hadi Dar es Salaam ambako alifika Aprili 10 na kusomewa tuhuma zake.
Kwa mujibu wa shahidi, baada ya Lissu kukataa kuandika maelezo yake, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka iliandaa mashtaka na Lissu akafikishwa katika Mahakama ya Kisutu siku hiyo.
Katika maswaliya dodoso ambayo yameulizwa na Lissu, alilenga zaidi kuhoji uzoefu, uadilifu na namna shahidi huyo alivyofanya kazi ya upelelezi.
Lissu alimuuliza Mahamba kama anajiona kuwa afisa mpelelezi mwenye uzoefu mkubwa, jambo ambalo shahidi alikubaliana nalo.
Lissu pia alimuuliza kama amewahi kupanda vyeo kwa kutengeneza kesi za uongo au kwa kuwatesa watuhumiwa katika vituo vya polisi. Shahidi alikanusha madai hayo.
Katika hatua nyingine, Lissu alimuomba shahidi athibitishe hati iliyokuwa mkononi mwake, ambayo Mahamba alikiri kuwa ni maelezo yake aliyoyaandaa kwa ajili ya kutoa ushahidi mahakamani.
Hati hiyo iliingizwa kama kielelezo katika kesi.
Baada ya hapo Lissu alianza kulinganisha ushahidi ambao Mahamba alikuwa ameutoa mahakamani na maelezo yake ya awali.
Lissu alimuuliza kama katika maelezo hayo kuna sehemu aliyoeleza kwamba anafanya kazi katika Kitengo X kinachoshughulikia makosa yanayohusisha usalama wa nchi.
Shahidi alikiri kuwa taarifa hiyo ipo.
Lakini alipoulizwa kama maelezo yake ya awali yanaeleza kwamba alisomea katika Chuo cha Polisi Moshi, alisema hayapo.
Kadhalika, shahidi alisema maelezo kuhusu yeye kuwa msaidizi wa mkuu wa Kitengo X, majukumu yake mbalimbali ya upelelezi, mafunzo aliyopata na baadhi ya vituo alikowahi kufanya kazi hayakuwepo katika maelezo yake ya awali.
Lissu akaendelea kumuuliza shahidi kama tofauti hizo zinaonyesha kwamba baadhi ya mambo aliyoyaeleza mbele ya Mahakama yalikuwa hayakuwepo katika maelezo aliyoyatoa awali.
Mara baada ya maelezo hayo Mahakama iliahirisha shauri hilo mpaka kesho Agosti 11, 2026 saa tatu asubuhi kutokana na muda wa Mahakama kuisha, ambapo shahidi Amini Mahamba ataendelea kutoa ushahidi kwa maswali ya dodoso alipoushia leo.
Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, linalohusishwa na madai ya kuhamasisha wananchi kuzuia au kuvuruga uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025, Lissu amekuwa rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja kwa kuwa shtaka la uhaini ni miongoni mwa makosa ambayo hayaruhusu mshtakiwa kupata dhamana.
Kufikia Agosti 10, 2026, Lissu amekuwa rumande kwa siku takribani 488 tangu alipokamatwa.
Katika kipindi hicho, kesi imepitia hatua mbalimbali za kisheria, huku upande wa mshtakiwa ukiendelea kupinga baadhi ya hatua zinazochukuliwa na upande wa mashtaka.