Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam inatarajiwa kutoa uamuzi iwapo Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ana kesi ya kujibu au la, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili.

Pia Unaeza Soma hapa
Lissu: Jamhuri Imeshindwa Kuthibitisha Kesi, Naomba Mahakama Itamke Sina Kesi ya Kujibu
Hatua hiyo imefikiwa leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, baada ya upande wa mashtaka kusema kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi wake 17 unatosha kuthibitisha hoja zilizowasilishwa katika hatua za awali za kesi hiyo.
Kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, Jamhuri imeiambia Mahakama kuwa baada ya kupitia ushahidi uliokwisha kutolewa na kuuchambua pamoja na ushahidi uliokuwa umebaki, imejiridhisha kuwa hakuna sababu ya kuendelea kuwaita mashahidi wengine.
“Ushahidi ambao tayari umeshatolewa ni ushahidi toshelezi na kuleta ushahidi zaidi kuthibitisha hoja ambazo zilikubaliwa wakati wa “Preliminary Hearing” ni kinyume cha sheria,” Katuga alieleza Mahakamani.
Kutokana na msimamo huo, upande wa Jamhuri umeomba Mahakama iruhusu kufungwa rasmi kwa ushahidi wake, huku ukisema umefanya hivyo baada ya kujiridhisha kuwa mashahidi 17 waliokwisha kutoa ushahidi wametosheleza mahitaji ya upande wa mashtaka.
Haya yanajiri katika uwaailishwaji wa hoja za kwanini mshtakiwa asiwe na kesi ya kujibu au awe na kesi ya kujibu ama kwa lugha nyingine kwamba kwanini asijitete mbele ya Mahakama.
Baada ya Jamhuri kufunga ushahidi wake, Lissu amesema hana pingamizi kuhusu hatua hiyo, akisisitiza kuwa jambo linalofuata kisheria ni Mahakama kuamua iwapo ushahidi uliowasilishwa unatosha kumtaka yeye aanze kujitetea.
Lissu ameitaka Mahakama itumie kifungu cha 312(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), akisema kifungu hicho kinaelekeza hatua inayopaswa kuchukuliwa pale ambapo upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha.
“Mahakama itarekodi kwamba hakuna hatia kwa vile upande wa mashtaka umefunga kesi yao. Kilichobaki ni kunisikiliza mimi na mawakili hawa wa Serikali kujibu kama nina hatia au sina hatia,” alisema Lissu.
Lissu pia amesisitiza kuwa hatua ya kuwasilisha hoja ya “No Case to Answer”, yaani kwamba mshtakiwa hana kesi ya kujibu, si jambo geni kisheria na kwamba kifungu cha 312(1) cha CPA kinatoa msingi wa hoja hiyo.
Kwa upande mwingine, Jamhuri imeomba Mahakama ipewe nafasi ya kuwasilisha hoja zake kuhusu kwa nini inaamini Lissu ana kesi ya kujibu.
Katuga amesema ni kawaida kwa Mahakama kuamua kwa kuzingatia mazingira ya kila kesi na kwamba Lissu mwenyewe hakuwa amepinga ombi la Jamhuri kuwasilisha hoja zake.
“Tunaona mtuhumiwa hakatai ombi letu la kuwasilisha hoja… tunaiachiiia Mahakama yenu tukufu,” Katuga amesema.
-Lissu aomba Mahakama itamke kama hana kesi ya kujibu-
Lissu, hata hivyo, amesisitiza kuwa suala hilo halihitaji mvutano mkubwa wa kisheria, akitaka Mahakama iamue iwapo ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri umefikia kiwango cha kumtaka yeye ajitetee.
Katika hoja zake, Lissu amesema upande wa Jamhuri umeshindwa kuonyesha kile kinachojulikana kisheria kama Prima Facie Case yaani ushahidi wa awali ambao, endapo hautapingwa na upande wa utetezi, unaweza kuwa msingi wa Mahakama kumtia hatiani mshtakiwa.
Kwa mujibu wa Lissu, ikiwa ushahidi uliowasilishwa na mashtaka hauwezi, hata ukiachwa bila kupingwa, kusababisha hatia, basi hakuna msingi wa kumtaka mshtakiwa kuanza kujitetea.
Ametumia pia mifano ya maamuzi ya Mahakama za Tanzania na Afrika Mashariki katika kesi mbalimbali kueleza misingi ya kisheria inayotumika katika kuamua iwapo mshtakiwa ana kesi ya kujibu.
–Hoja ya msingi: Je, ushahidi unathibitisha uhaini?-
Katika hoja zake, Lissu ameielekeza Mahakama kwenye vipengele anavyosema vinapaswa kuthibitishwa ili kosa la uhaini litimie, akitaja pamoja na utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwepo kwa nia ya kutenda kosa hilo na uthibitisho wa nia hiyo kupitia maandishi au vitendo vya wazi.
Lissu amesema hana ubishi kuhusu suala la utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini amepinga madai kwamba upande wa Jamhuri umeweza kuthibitisha nia ya kutenda uhaini.
Amesema maneno yanayodaiwa kuwa ya kihaini katika kesi hiyo hayakutaja Serikali, Bunge au Mahakama, akisisitiza kuwa hata baadhi ya mashahidi aliowahoji walikiri kutokuwepo kwa maneno hayo.
Pia amepinga hoja kuhusu uchapishaji wa maneno hayo, akisema upande wa Jamhuri ulipaswa kuwasilisha ushahidi unaohusiana na chapisho au video iliyodaiwa kuchapishwa kupitia Jambo TV.
Kwa mujibu wa Lissu, shahidi wa 17 ndiye aliyekiri kurekodi mkutano huo na baadaye kupeleka video hiyo kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo amesema linapaswa kuzingatiwa na Mahakama katika kutathmini iwapo ushahidi uliowasilishwa unatosha.
–Jamhuri: Lissu ana kesi ya kujibu-
Kwa upande wake, Nassoro Katuga ameiomba Mahakama itamke kuwa Lissu ana kesi ya kujibu, akisema ushahidi wa mashahidi 17 umejenga msingi wa kuthibitisha vipengele vya shtaka.
Katuga amesema Jamhuri imejikita katika aina ya shtaka linalomkabili Lissu chini ya kifungu cha 39(2)(b) na kwamba hati ya mashtaka inaonyesha nia inayodaiwa kuwa nayo mshtakiwa.
Amesema Jamhuri imewasilisha ushahidi kuhusu vipengele vitatu vya msingi vya kosa hilo, ikiwamo suala la utii wa Jamhuri ya Muungano, nia ya kuchochea au kuitisha Serikali na hatua zinazodaiwa kuchukuliwa na Lissu kuonyesha nia hiyo.
Katuga amemtaja shahidi wa 17 kama mmoja wa mashahidi muhimu katika kuthibitisha kile kinachodaiwa kilitokea katika eneo la tukio, huku akisema ushahidi wa mashahidi wengine pia umeunga mkono hoja ya Jamhuri.
Wakili huyo amesisitiza kuwa katika hatua hii Mahakama haipaswi kuingia kwa kina katika suala la uzito au uaminifu wa ushahidi wa mashahidi, bali kuangalia kama kuna ushahidi wa kutosha unaounda msingi wa kumtaka mshtakiwa ajitetee.
Akitumia uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi ya DPP dhidi ya Philipo Joseph Mtonda Katuga amesema suala la kuamua kama kuna kesi ya kujibu linapaswa kutofautishwa na tathmini ya mwisho kuhusu uaminifu na uzito wa ushahidi.
-Uamuzi wa Mahakama sasa unasubiriwa-
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Dunstan Ndunguru, akiongoza jopo la majaji watatu, amesema Mahakama itachukua muda kupitia hoja zilizowasilishwa pamoja na ushahidi uliotolewa na mashahidi 17 wa upande wa Jamhuri.
Uamuzi huo ndio utakaoweka hatua inayofuata ya kesi hiyo.
Iwapo Mahakama itaona kuwa Jamhuri haijaweka msingi wa kutosha wa kesi ya kujibu Lissu anaweza kuondolewa katika hatua ya kujitetea na kesi hiyo inaweza kufikia mwisho kwa upande wake.
Lakini iwapo Mahakama itaamua kuwa kuna kesi ya kujibu Lissu atalazimika kuingia katika hatua inayofuata ya kesi na kuwasilisha utetezi wake dhidi ya mashtaka ya uhaini yanayomkabili.
Lissu amekuwa kizuizini kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kukamatwa kwake Aprili 9,2025, katika kesi ambayo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu kutokana na uzito wa shtaka la uhaini na nafasi yake kama kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania.
Kwa sasa, hatua inayosubiriwa kwa karibu ni uamuzi wa Mahakama kuhusu swali moja kuu: Je, ushahidi uliowasilishwa na Jamhuri unatosha kumtaka Tundu Lissu ajitetee, au hakuna kesi ya kujibu?
Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa Agosti 21, 2025 siku ya Ijumaa saa tatu asubuhi