
Safari ya kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, imechukua zaidi ya mwaka mmoja tangu alipokamatwa katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Aprili 9, 2025.
Kesi hiyo, ambayo imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu ndani na nje ya Tanzania, imepitia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama Kuu na kwa baadhi ya hatua Mahakama ya Rufani, huku kukiwa na pingamizi, maombi ya kisheria, ushahidi wa mashahidi wa kawaida na wa ulinzi maalumu, pamoja na mabishano kuhusu ushahidi wa kidijitali.
Sasa, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wake Agosti 17, 2026, Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam inajiandaa kutoa uamuzi kuhusu swali muhimu: Je, ushahidi uliowasilishwa na Jamhuri unatosha kumtaka Lissu aanze kujitetea, au hana kesi ya kujibu?
-Aprili 9, 2025: Kukamatwa Mbinga-
Safari ya kesi ilianza Aprili 9, 2025, wakati Lissu alipokamatwa katika wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara wa CHADEMA.
Mkutano huo ulikuwa sehemu ya kampeni ya chama hicho iliyohusishwa na kaulimbiu ya “No Reforms, No Election”, ambayo CHADEMA ilikuwa ikiitumia kushinikiza mageuzi ya mfumo wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Baada ya mkutano huo, polisi walimchukua Lissu na kumpeleka kituoni ambapo alishikiliwa kwa karibu saa 24 kabla ya kufikishwa mahakamani. Alisafirishwa kutoka Mbinga hadi Dar es Salaam, umbali wa zaidi ya kilomita 1,000.
Hatua hiyo iliibua mjadala mkubwa wa kisiasa na kisheria, hasa kuhusu mazingira ya kukamatwa kwake na muda aliokaa kabla ya kufikishwa mahakamani.
-Aprili 10: Lissu afikishwa Kisutu-
Siku iliyofuata, Aprili 10, 2025, Lissu alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Hapo ndipo umma ulipofahamu rasmi kwamba alikuwa akikabiliwa na shtaka la uhaini, pamoja na mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Hata hivyo, katika hatua hiyo Lissu hakuruhusiwa kujibu shtaka la uhaini, huku akikiri kutokuwa na hatia katika shtaka tofauti la kuchapisha taarifa za uongo.
Jamhuri ilidai kuwa msingi wa shtaka la uhaini ulitokana na kauli ambazo Lissu alidaiwa kuzitoa Aprili 3, 2025 katika mkutano wake na wanahabari jijini Dar es Salaam, akihamasisha wananchi kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Kwa upande wa Lissu, mashtaka hayo yalielezwa kuwa yana uhusiano mkubwa na shughuli zake za kisiasa.
-Kesi ya Kisutu na mapambano ya awali-
Katika hatua za awali, kesi iliendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya taratibu za awali kabla ya kupelekwa Mahakama Kuu.
Miongoni mwa masuala yaliyoibuka ni namna ushahidi wa Jamhuri ungetolewa na suala la utambulisho wa baadhi ya mashahidi.
Mahakama iliruhusu hatua za kulinda utambulisho wa baadhi ya mashahidi ambao Jamhuri ilisema walihitaji ulinzi.
Ikumbukwe katika nyakati zote hizo kesi ikiendelea, kesi hiyo ilikua ikirushwa mubashara na vyombo mbalimbali vya habari, kwa kutumia chaneli ya Mahakama ambayo ndio ikirusha matangazo hayo.
Agosti 18, 2025 mambo yakabadilika, Kisutu pia iliamuru kwamba ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri katika kesi hiyo usirushwe moja kwa moja kwenye vyombo vya habari, hatua iliyohusishwa na ulinzi wa mashahidi, hususan raia ambao hawakuwa maafisa wa usalama.
Hatua hiyo ikawa sehemu ya mjadala mpana kuhusu uwiano kati ya haki ya mshtakiwa kupata kesi ya wazi na ulinzi wa mashahidi.
-Wanasheria na wanaharakati nao waingia kwenye mkondo wa kesi-
Mwenendo wa kesi ya Lissu haukuishia mahakamani pekee. Katika hatua za awali, mazingira yaliyoizunguka kesi hiyo yalishuhudia pia kukamatwa kwa baadhi ya wanasheria, kuzuiwa kwa wanasheria waliokuwa wakitaka kumwakilisha Lissu na wanaharakati kuingilia kati wakitaka kuhakikisha haki zake za kisheria zinalindwa.
Miongoni mwa matukio yaliyovuta zaidi hisia ni kukamatwa kwa mwanasheria wa Kenya na mwanasiasa wa upinzani, Martha Karua, aliyefika Tanzania kwa lengo la kumwakilisha Lissu. Karua alikamatwa baada ya kuwasili nchini na baadaye kurejeshwa Kenya, hatua iliyozua mjadala kuhusu nafasi ya mawakili wa nje katika kesi hiyo.
Baadhi ya mawakili wengine waliokuwa wakihusishwa na kesi hiyo pia walikumbana na vikwazo katika kutekeleza majukumu yao, huku upande wa Lissu ukilalamikia ugumu wa kupata nafasi ya kushauriana naye kwa faragha akiwa mahabusu.
Masuala hayo yalifanya kesi ya Lissu kuanza kuangaliwa zaidi ya mipaka ya mahakama. Mashirika ya kutetea haki za binadamu, wanaharakati na taasisi za kisheria nchini na nje ya Tanzania zilianza kutoa kauli zikieleza wasiwasi wao kuhusu mazingira ambayo kesi hiyo ilikuwa ikiendeshwa.
Mjadala huo ulihusisha masuala kadhaa, ikiwemo haki ya mshtakiwa kupata uwakilishi wa kisheria, uhuru wa mawakili kutekeleza majukumu yao, haki ya kukutana na mteja kwa faragha na haki ya kesi yenye mchakato unaoaminika.
Kwa upande wa mamlaka, hatua zilizochukuliwa dhidi ya baadhi ya watu waliohusika katika kesi hiyo zilihusishwa na masuala ya kiusalama na utekelezaji wa sheria.
Hata hivyo, kwa wanaharakati na mashirika ya haki za binadamu, matukio hayo yaliongeza maswali kuhusu nafasi ya mfumo wa haki katika kesi iliyokuwa ikimkabili kiongozi mkuu wa upinzani.
Kwa namna hiyo, kesi ya Lissu haikuwa tena suala la mashtaka dhidi ya mtu mmoja pekee. Ilianza pia kuwa mjadala mpana kuhusu haki ya kujitetea, uhuru wa wanasheria na nafasi ya asasi za kiraia katika kulinda haki za washtakiwa.
-Kesi yaelekea Mahakama Kuu-
Baada ya uchunguzi kukamilika, kesi ilifikia hatua ya committal proceedings katika Mahakama ya Kisutu.Agosti 18, 2025, Mahakama ilikamilisha hatua hiyo na Lissu akapatiwa taarifa za mashahidi na vielelezo ambavyo Jamhuri ilikusudia kuvitumia katika kesi Mahakama Kuu.
Jamhuri iliieleza Mahakama kwamba ilikuwa na mpango wa kuita mashahidi 30 na kuwasilisha vielelezo tisa katika kesi hiyo.
Hapo ndipo kesi ilipohamia rasmi katika hatua ya kusikilizwa na Mahakama Kuu.
-Mahakama Kuu: Kesi inaanza rasmi-
Kesi iliposikilizwa Mahakama Kuu, iliwekwa mbele ya jopo la majaji watatu.
Jopo hilo liliongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Jamhuri iliendelea na ushahidi wake, ikieleza kwamba Lissu alitoa kauli ambazo zililenga kuhamasisha wananchi kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025 na kwamba kauli hizo zilikuwa na nia ya kuasi au kutishia serikali.
Kwa upande wake, Lissu aliamua kutumia kwa kiasi kikubwa nafasi yake mwenyewe katika kuhoji mashahidi wa Jamhuri.
Hapo ndipo kesi ilipoanza kuchukua sura nyingine.
-Oktoba 2025: Lissu aanza kuwauliza maswali mashahidi-
Oktoba 6, 2025, shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Kamishna Msaidizi wa Polisi George Bagemu, alianza kutoa ushahidi.
Alikaa kizimbani kwa siku nne, huku Lissu akifanya sehemu kubwa ya cross-examination.
Miongoni mwa hoja zilizojitokeza ni tafsiri ya kisheria ya kauli zinazohusishwa na kuzuia uchaguzi.
Shahidi huyo alieleza kwamba kuzuia uchaguzi kwa njia halali si uhaini, lakini kwamba kujaribu kuzuia uchaguzi kwa njia zisizo halali, vitisho au kukiuka sheria kunaweza kuingia katika eneo la kosa la uhaini.
Lissu pia alimuuliza shahidi kuhusu historia yake ya kisiasa na nafasi yake katika harakati za demokrasia na haki za binadamu.
-Ushahidi wa video: Flash disk na memory card-
Moja ya sura zilizozua mjadala mkubwa katika kesi hiyo ilikuwa ushahidi wa video.
Jamhuri iliwasilisha flash disk na memory card zilizokuwa na video ambayo ilidaiwa kuwa na kauli za Lissu.
Shahidi wa tatu, Inspekta wa Polisi Samweli Eribariki Kaaya, ambaye ni mtaalamu wa picha za kiuchunguzi, alieleza namna alivyopokea vifaa hivyo kwa ajili ya uchunguzi.
Lakini Lissu alipinga kupokelewa kwa ushahidi huo.
Hoja yake ilikuwa kwamba shahidi huyo hakuwa na mamlaka au sifa zinazohitajika kisheria kuwasilisha baadhi ya ushahidi huo.Hilo likawa pingamizi ambalo kimsingi lilichukua siku kadhaa kujibiwa na Mahakama
Oktoba 23, 2025, Mahakama Kuu ilikubaliana na moja ya hoja hizo na kukataa ripoti iliyowasilishwa kuhusu uhalisia wa video hiyo, ikisema shahidi hakuwa na uwezo wa kisheria kuwasilisha ushahidi huo.
Uamuzi huo ukawa moja ya ushindi wa kisheria wa Lissu katika hatua hiyo ya kesi.
-Shahidi wa kificho aingia katika kesi-
Kadiri ushahidi wa Jamhuri ulivyoendelea, suala la mashahidi wanaolindwa likawa moja ya maeneo makubwa ya mabishano.
Jamhuri ilianza kuwasilisha mashahidi ambao hawakuonekana wazi kwa umma au mshtakiwa.
Mmoja wa mashahidi hao alitambulishwa kwa jina la kificho P5 na kutoa ushahidi akiwa katika eneo la kizimba maalumu lililomficha mbele ya umma na Lissu, huku majaji pekee wakiweza kumuona.
Jamhuri ilieleza kwamba hatua hiyo ilikuwa kwa ajili ya usalama wa mashahidi.Lakini Lissu alipinga namna utaratibu huo ulivyotekelezwa, akisisitiza kwamba ulinzi wa shahidi haupaswi kuathiri haki yake ya kupata kesi ya haki, hatua hiyo ilizua mabishano makali na hatimae pingamizi lingine likaibuka.
-Februari 2026: Mzozo kuhusu “kizimba” cha shahidi-
Mzozo huo ulifikia hatua nyingine Februari 2026, wakati Lissu alipinga muundo wa eneo la kizimba maalum lililokuwa linatumika kumficha shahidi.
Hoja yake ilikuwa kwamba kama shahidi amefichwa kwa kiwango ambacho majaji hawawezi kuona vizuri mwenendo wake, hilo linaweza kuathiri uwezo wa Mahakama kutathmini ushahidi wake.
Februari 11, 2026, Mahakama ilikubaliana kwa sehemu na hoja hiyo na kuagiza eneo hilo lifanyiwe marekebisho ili majaji waweze kumuona shahidi vizuri. Hata hivyo, Mahakama ilikataa baadhi ya pingamizi nyingine za Lissu kuhusu matumizi ya mashahidi waliolindwa.
Hivyo kesi ikaendelea, huku utaratibu wa kuwalinda mashahidi ukiendelea kutumika.
-Mashahidi wengine na hoja kuhusu uchaguzi-
Katika kipindi hicho, Jamhuri iliendelea kuita mashahidi wake.
Baadhi yao walieleza madai ya namna kauli za Lissu zilivyotafsiriwa na vyombo vya dola na jinsi vijana au makundi mbalimbali yalivyodaiwa kuhamasishwa kuelekea uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Shahidi mwingine, aliyetambuliwa kama P8, alitoa ushahidi akiwa katika kundi la mashahidi waliolindwa. Shahidi huyo alijitambulisha kama mwanachama wa CHADEMA lakini alieleza kwamba katika mazingira ya kesi hiyo hamtambui Lissu kama mwenyekiti wake.
Baadaye shahidi mwingine wa polisi alieleza kuhusu taarifa zilizodaiwa kupokelewa na polisi kuhusu vijana waliokuwa wakihamasishana kuzuia uchaguzi na kumuunga mkono Lissu.
Kwa kila shahidi, Lissu aliendelea kutumia nafasi yake ya kuhoji ushahidi wa Jamhuri.
-Lissu na maswali yake kwa mashahidi-
Katika sehemu mbalimbali za kesi, Lissu alitumia uzoefu wake wa sheria kuuliza maswali yaliyolenga kuonyesha tofauti kati ya taarifa za mashahidi walizotoa mahakamani na taarifa zao za awali.
Katika moja ya vipindi hivyo, alitumia hata Police General Orders kuwauliza maafisa wa polisi kuhusu namna walivyofanya uchunguzi, walivyoandika taarifa na hatua walizochukua katika majukumu yao.
Mchakato huo uliifanya kesi kuwa siyo tu ya kusikiliza ushahidi wa Jamhuri, bali pia kuwa uwanja wa Lissu kuhoji namna ushahidi huo ulivyokusanywa na kuwasilishwa.
-Pingamizi jingine: Jamhuri yataka kuongeza ushahidi-
Februari 18, 2026, Jamhuri ilijaribu kuwasilisha ushahidi wa ziada kupitia ACP Amin Mahamba, ambaye alihusishwa na timu ya uchunguzi wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Ombi hilo liliwasilishwa na upande wa Jamhuri chini ya kifungu cha 308 cha Sheria ya Makosa ya Mwenendo wa Jinai, sura ya 20 marejeo ya mwaka 2023
-Lissu alipinga ombi hilo-
Hoja yake ilikuwa kwamba kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinahusu ushahidi uliokuwepo wakati wa committal proceedings lakini haukusomwa, na si ushahidi mpya uliopatikana baadaye.
Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja hiyo Februari 24, 2026 na kuzuia Jamhuri kuingiza ushahidi huo wa ziada.
Akisoma uamuzi huo Jaji Ndunguru, alisema mahakama imepitia hoja za pande zote, vifungu vya sheria na kumbukumbu za mwenendo wa kesi, lakini kifungu hicho cha 308 kinafungua mlango wa kumuita shahidi na maelezo yake, lakini hakifungui mlango wa kuleta shahidi au ushahidi mpya ambao haukuwepo katika hatua za awali za kesi.
Uamuzi huo ukasababisha hatua nyingine ya kisheria.
-Jamhuri yaenda Mahakama ya Rufani-
Baada ya Mahakama Kuu kukataa ushahidi huo wa ziada, upande wa Jamhuri uliwasilisha ombi la mapitio katika Mahakama ya Rufani.
Hatua hiyo ilisababisha mwenendo wa kesi ya msingi kusimama kwa muda, huku suala la mamlaka ya Jamhuri kuwasilisha ushahidi huo likipelekwa katika Mahakama ya Rufani.
Lissu naye alipinga hatua hiyo, akisema uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa uamuzi wa kati ambao haukuwa umehitimisha haki za pande hizo na hivyo haukupaswa kufanyiwa mapitio kwa namna iliyotakiwa na Jamhuri.
Kwa sababu hiyo, kesi ya msingi ikawa imesimama kwa miezi kadhaa.
-Kesi yarudi Agosti 2026-
Baada ya kusuasua kwa siku takribani 160, kesi ilirejea Mahakama Kuu Agosti 10, 2026.
Wakati huo tayari Jamhuri ilikuwa imeita mashahidi 15, na Lissu akaendelea na hatua ya kuhoji mashahidi waliobaki.
Kesi ikaingia katika hatua yake ya mwisho ya ushahidi wa upande wa mashtaka.
-Lissu amaliza kumuhoji mpelelezi mkuu wa kesi-
Katika siku za mwisho za ushahidi wa Jamhuri, Lissu alitumia muda mwingi kumuhoji mpelelezi mkuu wa kesi.
Maswali yake yalilenga, miongoni mwa mambo mengine, namna uchunguzi ulivyofanyika, taarifa za mashahidi na tofauti zilizokuwepo kati ya ushahidi wa mdomo na taarifa za maandishi.
Baadhi ya mahojiano hayo yalihusisha pia namna maafisa wa polisi walivyotekeleza majukumu yao wakati wa uchunguzi.
Hii ilikuwa hatua muhimu kwa sababu Lissu alikuwa amefikia mwisho wa nafasi yake ya kuhoji ushahidi wa upande wa Jamhuri kabla ya upande huo kufunga kesi kwa kumleta shahidi wa 17 ambaye alikuwa ni shahidi wa kificho mwenye taaluma ya uandishi wa habari na mfanyakazi wa Jambo Tv.
-Agosti 17, 2026: Jamhuri yafunga ushahidi-
Hatimaye, Agosti 17, 2026, upande wa Jamhuri ulifunga rasmi ushahidi wake.
Katika hatua hiyo, Jamhuri ilikuwa imewasilisha ushahidi kupitia mashahidi 17 kati ya 30 iliyokuwa imewaorodhesha awali.
Baada ya Jamhuri kufunga ushahidi, Lissu hakusubiri kuitwa kujitetea.
Badala yake, aliwasilisha hoja kwamba hana kesi ya kujibu.
Kwa maana nyingine, Lissu anaiomba Mahakama itathmini ushahidi uliowasilishwa na Jamhuri na kufikia hitimisho kwamba haujafikisha kiwango cha kumtaka yeye aanze kutoa utetezi. Pia ameomba aachiwe na Serikali iamriwe kumlipa fidia.
-Sasa nini kinafuata?-
Hapa ndipo kesi imefikia hatua yake muhimu zaidi tangu ilipoanza.
Mahakama Kuu sasa inapaswa kujibu swali moja la msingi:
Je, upande wa Jamhuri umeonyesha ushahidi wa kutosha wa kumtaka Tundu Lissu aanze kujitetea?
Kama Mahakama itaona kwamba Jamhuri haijaweka msingi wa kutosha, Lissu anaweza kutokuwa na kesi ya kujibu katika hatua hiyo na kesi inaweza kufikia mwisho bila yeye kuanza kutoa ushahidi wa utetezi.
Lakini kama Mahakama itaona kwamba ushahidi wa Jamhuri unatosha kumtaka ajibu, kesi itaingia katika hatua nyingine ya utetezi wa Lissu.
Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imesema itatoa uamuzi kuhusu suala hilo Ijumaa, Agosti 21, 2026.
-Zaidi ya mwaka mmoja baadaye-
Kesi ambayo ilianza kwa kukamatwa kwa Lissu Mbinga Aprili 9, 2025, imepitia zaidi ya mwaka mmoja wa mahabusu na hatua mbalimbali za mahakama.
Kutoka Kisutu hadi Mahakama Kuu, safari hiyo ya siku takribani 496 imehusisha mjadala kuhusu ushahidi, mashahidi wanaolindwa, ushahidi wa kidijitali, uwezo wa mashahidi kuwasilisha vielelezo, maombi ya kuongeza ushahidi, pamoja na masuala yaliyofikishwa Mahakama ya Rufani.
Kwa sasa, hata hivyo, hatua hiyo ya kwanza ya kesi imekamilika: Jamhuri imemaliza upande wake.
Kinachosubiriwa sasa ni uamuzi wa Mahakama kuhusu kama ushahidi uliowasilishwa unatosha kumtaka Tundu Lissu ajibu mashtaka ya uhaini.
Ni uamuzi ambao utaamua kama kesi itaishia katika hatua hii au itaingia katika sura nyingine.
Sura ya Lissu kuanza kujitetea dhidi ya shtaka linaloweza kubeba adhabu kubwa zaidi chini ya sheria za Tanzania, ambapo iwapo mshtakiwa atakutwa na hatia basi hukumu yake ni kifo.