Mnyika Atumia Hotuba Ya Nyerere Utetezi Kesi Ya Lissu, Aibua Kifo Cha Akwelina

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, ameendelea kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, akirejea hotuba za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kesi iliyowahi kumkabili yeye pamoja na viongozi wengine 8 wa CHADEMA kufuatia kifo cha mwanafunzi Akwelina Akwilini, katika kuieleza Mahakama kwa nini anaamini kauli zinazodaiwa kuwa za uhaini dhidi ya Lissu hazikustahili kuchukuliwa kama tishio kwa Serikali.

Mnyika Atumia Hotuba Ya Nyerere Utetezi Kesi Ya Lissu, Aibua Kifo Cha Akwelina

Mnyika, ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa utetezi baada ya Lissu mwenyewe kuwa shahidi wa kwanza, ameendelea na ushahidi wake leo Jumatatu, Agosti 31, 2026, ikiwa ni mwendelezo wa ushahidi aliouanza Ijumaa, Agosti 28, 2026.

Akihojiwa na Lissu kuhusu maneno yanayodaiwa kutolewa katika mkutano wa Aprili 3, 2025, Mnyika amesema kwa ufahamu wake kauli hizo zilikuwa za kisiasa na zililenga kuonyesha matatizo yaliyopo katika mfumo wa uchaguzi nchini, badala ya kuwa tishio kwa Serikali.

Katika maelezo yake, Mnyika amesema Lissu katika hotuba hiyo alizungumzia mabadiliko yaliyohitajika katika mfumo wa uchaguzi, ikiwemo mgawanyo wa majimbo kwa kuzingatia idadi ya watu, uwepo wa Tume huru ya Uchaguzi, kuondolewa kwa mamlaka ya Rais katika uteuzi wa wajumbe wa Tume, Tume kuwa na watumishi wake huru badala ya kutumia watumishi wa Serikali, pamoja na kuwepo kwa uwezekano wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais mahakamani.

Mnyika amesema hoja hizo zilitokana na utafiti wa muda mrefu uliofanywa na Lissu pamoja na mapendekezo yaliyowahi kutolewa na waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa.

Lissu, anayekabiliwa na shtaka la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, akiwa raia wa Tanzania, alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Miongoni mwa maneno hayo ni pamoja na kauli inayodaiwa kusema: “Msimamo huu unaashiria uasi… tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi… kwa hiyo tunaenda kikinukisha… huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…”

Hata hivyo, Mnyika ameiambia Mahakama kuwa hakusikia Serikali ikitajwa katika maneno hayo, hivyo kwa ufahamu wake hawezi kusema kauli hizo zilikuwa tishio kwa Serikali.

Lissu alipomuuliza kuhusu kauli ya “kuhamasisha uasi”, Mnyika alirejea katika hotuba za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akisema aliwahi kumsikia akizungumza kuhusu vijana kuwa waasi dhidi ya mifumo kandamizi.

“Niliwahi kusikia kwenye hotuba ya Mwalimu Nyerere akisema anataka vijana wa Taifa hili kuwa waasi dhidi ya mifumo kandamizi, lakini sijawahi kuona kama alikamatwa,” amesema Mnyika.

Alipoulizwa kama kuna tatizo mtu kusema anahamasisha uasi, Mnyika amesema: “Hakuna tatizo lolote.”

Mnyika pia amesema kauli ya “tutazuia uchaguzi” haiwezi kutafsiriwa moja kwa moja kama tishio, kwa kuwa kuna njia mbalimbali za kidemokrasia za kuzuia au kupinga uchaguzi, ikiwemo kususia uchaguzi au kutumia njia za kisheria.

Akieleza chanzo cha msimamo wa CHADEMA wa “No Reforms, No Election”, Mnyika amesema msimamo huo haukuanzishwa na Lissu Aprili 3, 2025, bali ulitokana na mfululizo wa vikao vya chama vilivyofanyika baada ya kile alichokiita matatizo yaliyotokea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 27, 2024.

Mnyika amesema Kamati Kuu ya CHADEMA ilifanya kikao maalum cha dharura Desemba 2 na 3, 2024, kwa ajili ya kufanya tathmini ya uchaguzi huo na kupitisha maazimio 10, likiwemo azimio kwamba hakukuwa na uchaguzi huru, wa haki na halali na kwamba kulikuwa hakuna uwezekano wa kuwa na uchaguzi huru katika mazingira yaliyokuwepo ya Kikatiba na kisheria.

Amesema chama kiliamua kuunganisha Watanzania kudai mabadiliko ya Katiba na sheria kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025, ndipo ulipoibuka msimamo wa “No Reforms, No Election”.

Kwa mujibu wa Mnyika, maazimio hayo yalipitishwa na Kamati Kuu, yakapelekwa Baraza Kuu na baadaye Mkutano Mkuu wa chama, ambao uliamua utekelezaji wake uanze mara moja.

Amesema Mkutano Mkuu huo baadaye ulimchagua Lissu kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, huku John Heche akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Bara na Said Mzee Said kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar.

Mnyika amesema baada ya hapo viongozi wa CHADEMA walifanya vikao Bagamoyo kuanzia Januari 31 hadi Februari 4, 2025, kwa ajili ya kupanga namna ya kutekeleza msimamo huo, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma, kukutana na wadau wa uchaguzi, viongozi wa dini, asasi za kiraia, waandishi wa habari, jumuiya za kikanda na kimataifa pamoja na watu mashuhuri.

Amesema katika utekelezaji huo walikutana na watu mbalimbali, akiwemo Sheikh Ponda Issa Ponda, viongozi wa Kituo cha Demokrasia, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na aliyekuwa Jaji Mkuu Joseph Warioba.

Pia amesema Machi 17, 2025, ujumbe wa CHADEMA ulikutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa ajili ya kueleza msimamo wa “No Reforms, No Election”, ambapo kwa mujibu wa Mnyika, Msajili alisema hakuona tatizo la kisheria katika msimamo huo na baadaye Aprili 10, 2025 akautaja kuwa kauli mbiu ya kisiasa ambayo haikiuki sheria.

Mnyika amesema Machi 23, 2025, CHADEMA ilianza operesheni katika Kanda ya Nyasa, ikihusisha Mbeya, Songwe, Iringa na Rukwa, na kwamba mkutano wa uzinduzi ulifanyika Mbeya ukiwa na Lissu kama mgeni rasmi.

Amesema baada ya Kanda ya Nyasa, chama kilipanga kuelekea Kanda ya Kusini, ikiwemo mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, na kwamba mkutano wa Aprili 3, 2025 ulikuwa sehemu ya utekelezaji wa mpango huo.

Mnyika amesema baada ya mkutano huo hakuchukua hatua yoyote ya kupeleka taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu maneno yaliyosemwa na Lissu, wala hakutoa maelekezo kwa wanachama kuhusu namna ya kuripoti hotuba hiyo.

Amesema pia hajui hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya waandishi wa habari waliokuwa kwenye mkutano huo na kuchapisha au kusambaza taarifa zake, wala hakuna mtu mwingine aliyeshtakiwa kwa kushiriki katika kupanga au kuandaa mkutano huo.

Katika sehemu nyingine ya ushahidi wake, Mnyika amekanusha shtaka linalodai kwamba Lissu ndiye aliyechapisha maneno hayo kwenye mtandao wa Jambo TV.

Amesema kama Katibu Mkuu wa chama, hakuhusika na shughuli za waandishi wa habari wala kutoa maelekezo kuhusu taarifa gani zichapishwe, na kwamba waandishi walikuwa huru kufanya kazi zao.

Mnyika amesema baada ya kusikia kuwa kulikuwa na madai kwamba maneno hayo yalichapishwa na Jambo TV, alifuatilia mtandao huo lakini hakuwahi kuona hotuba fupi iliyokuwa na maneno hayo pekee.

Amesema alichokiona ni video ya mkutano mzima uliodumu takribani saa tatu.

Mnyika pia ameeleza matukio yaliyofuata baada ya Lissu kukamatwa Aprili 9, 2025, akidai kuwa siku hiyo hiyo kulikuwa na hatua nyingine za kisheria dhidi ya viongozi wa CHADEMA.

Amesema Aprili 12, 2025, Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi walitoa kauli kwamba CHADEMA haitaruhusiwa kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 na uchaguzi wa marudio hadi mwaka 2030, kwa madai kuwa Katibu Mkuu wa chama hakusaini fomu za maadili ya uchaguzi.

Pia amesema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliandika barua kwa chama ikitaka maelezo kuhusu uhalali wa Katibu Mkuu na wajumbe walioteuliwa na Baraza Kuu Januari 22, 2025.

Kwa mujibu wa Mnyika, baada ya mabadilishano ya barua, Msajili alitangaza Mei 15, 2025 kutengua nafasi ya Katibu Mkuu na wajumbe hao, na Mei 27, 2025 akatangaza kusitisha ruzuku ya CHADEMA kwa madai kuwa chama hakikuwa na Katibu Mkuu halali.

Katika kuunga mkono hoja yake kwamba kesi inayomkabili Lissu ni sehemu ya mfululizo wa mashtaka dhidi ya viongozi wa CHADEMA, Mnyika alirejea pia tukio la kuuawa kwa mwanafunzi Akwelina Akwilini mwaka 2018.

Amesema katika tukio hilo polisi walitumia risasi na kusababisha vifo na majeruhi, huku yeye pamoja na viongozi wengine wa CHADEMA wakishtakiwa kwa madai ya kufanya mkusanyiko usio halali, kusababisha ghasia na kuhusishwa na kifo cha Akwelina.

Mnyika amesema baadaye yeye pamoja na viongozi hao walihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela au kulipa faini ya Shilingi milioni 350, na wakaanza kutumikia kifungo kabla Watanzania kuchangisha fedha na kulipa faini hiyo.

Amesema walikata rufaa na Juni 2021 Mahakama Kuu, chini ya Jaji Mgeta, iliwakuta hawana hatia na kufuta hukumu hiyo.

Mnyika ameliambia Mahakama kuwa kesi hiyo ya zamani ina uhusiano na kesi ya sasa kwa sababu, kwa mtazamo wake, zote ni sehemu ya matumizi ya njia za kisheria dhidi ya viongozi wa CHADEMA na juhudi za kukwamisha mabadiliko ya kisiasa.

“Yana uhusiano kwa sababu hii kesi ni mwendelezo wa kuwabambikia viongozi wa CHADEMA kesi za uongo na mbinu za kukwamisha mabadiliko, ni matumizi yasiyo ya haki ya njia za kimahakama na kisheria dhidi ya wapinzani na CCM dhidi ya CHADEMA na viongozi wake,” amesema.

Mnyika amesisitiza kuwa anaamini mashtaka yanayomkabili Lissu ni ya uongo na yamebambikizwa, akitaja madai mbalimbali yaliyomo kwenye kesi hiyo, ikiwemo kumtuhumu Lissu kuandaa mkutano ambao, kwa mujibu wake, haukuandaliwa na yeye peke yake, kupanga njama peke yake wakati ulikuwa uamuzi wa chama, pamoja na madai ya kuchapisha maneno ambayo hakuyachapisha.

Mwisho, Mnyika amesema anamfahamu Lissu kwa zaidi ya miaka 23 na kwamba katika kipindi hicho amemwona kama mtetezi wa haki, mtu anayepigania mabadiliko na mwenye msimamo wa kusimamia kile anachoamini kuwa ni ukweli.

Kwa msingi huo, amesema anaamini mashtaka yanayomkabili Lissu hayaakisi aina ya mtu anayemfahamu na kwamba ni “gharama” anayolipa kutokana na msimamo wake wa kisiasa.

Kesi hiyo inaendelea mbele ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, ikisikilizwa na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na jaji Dunstan Ndunguru, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Mnyika amemaliza kutoa ushahidi wake wa msingi na sasa ni zamu ya kuanza kuhojiwa na upande wa Jamhuri kupitia maswali ya dodoso.

Kesi inaendelea